Yanga hii hata Simba wamekubali

Muktasari:

  • Simba iliondoshwa na Al Masry ya Misri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwa kanuni ya bao la ugenini lakini Yanga juzi Jumatano ilifanya kweli kwa kuiondosha Welayta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1 na kutinga hatua ya makundi. Unaambiwa hata watu wa Simba wenyewe wameukubali muziki wa Yanga.

KILE Simba inafanya, Yanga inaweza kufanya zaidi. Siyo maneno ya mtaani bali ni takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba iliondoshwa na Al Masry ya Misri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwa kanuni ya bao la ugenini lakini Yanga juzi Jumatano ilifanya kweli kwa kuiondosha Welayta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1 na kutinga hatua ya makundi. Unaambiwa hata watu wa Simba wenyewe wameukubali muziki wa Yanga.

Yanga imerudia mafanikio ya mwaka 2016 walipofika hatua hiyo na kumaliza nafasi na nne katika kundi lao lililotoa bingwa msimu huo TP Mazembe ya DR Congo.

Mafanikio hayo ya Yanga yametokana na mapambano ya dakika 180 katika mechi mbili baina ya timu hiyo iliyoing’oa Zamalek ya Misri kwenye raundi ya kwanza. Yanga ilishinda 2-0 nyumbani na kupoteza 1-0 ugenini hivyo kufuzu kilaini tu.

Mwanaspoti ambayo ilikuwa hapo Hawassa ulipopigwa mchezo huo, inakuletea mambo yaliyoambatana na mchezo huo wa marudiano uliokuwa mkali na wa kusisimua.

Ushindi nyumbani

Yanga sasa inatakiwa kutambua umuhimu wa ushindi wa nyumbani, na somo hili haliishii kwa Yanga pekee ambapo nchi inatakiwa kulitambua hili na kuacha ushamba wa kuzomeana na kupata matokeo mabaya nyumbani. Kama Yanga isingeshinda nyumbani kwa mabao 2-0 basi juzi hali ingekuwa tofauti ni kama ungesema usiyempenda kaja.

Ushindi wa mabao hayo ndiyo ulioivusha Yanga lakini uzuri zaidi hawakuruhusu kufungwa bao la ugenini kwa Dicha. Kama Yanga ingeshinda 1-0 nyumbani maana yake wangelazimika kuingia hatua chungu kwao ya mikwaju ya penalti ambayo inawatesa sana lakini pia kama ingeshinda nyumbani 2-1 maana yake juzi Yanga ingekuwa imetolewa kwa faida ya bao la ugenini kwa Dicha kufuatia Waethiopia hao kushinda 1-0 wakiwa nyumbani.

Yanga yaficha jezi za njano

Yanga kwa mipango yao wanatumia jezi za njano nyumbani lakini pia zile za kijani ugenini. Kama ulikuwa hujui ni kwamba katika mechi zote mbili hizo Yanga imetumia jezi za kijani pekee ambazo zitabaki kama alama kwao kuwavusha hatua hii muhimu wakijihakikishia kupata kiasi cha sh600 milioni huku pia mabao yote yaliyowavusha yakifungwa kwa vichwa.

Makocha Yanga wasusiana benchi

Mchezo wa kwanza pale Uwanja wa Taifa Yanga ililazimika kuwa na makocha wawili pekee katika benchi lao kocha wao mkuu George Lwandamina na msaidizi wake wa makipa Juma Pondamali kufuatia makocha wake wawili wasaidizi wa kwanza Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila kuwa jukwaani.

Mwandila alitajwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa anatakiwa kukosa mechi ya kwanza dhidi ya Dicha wakati aliyetakiwa kusimamishwa ni Nsajigwa ambaye ndiye aliyefanya makosa katika mchezo dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Mchezo wa juzi ni kama makocha hao walipishana ambapo Lwandamina ametimka na kukosa mechi hiyo wakati Nsajigwa na Mwandila wakirudi kazini.

Njiwa atua na bao

Bao la Dicha juzi lilifungwa ndani ya dakika mbili za kwanza lakini kabla ya bao hilo wakati shambulizi la Dicha likifanyika na kuzalisha kona iliyozaa bao lililofungwa na mshambuliaji, Arafat Djako, njiwa mmoja aliyepakwa rangi alitua nyuma ya benchi la Yanga na kuzua hali ya wasiwasi.

Njiwa huyo alikuwa amepakwa rangi ya bluu na nyekundu kisha akafungwa kitambaa cha rangi ya jezi za Dicha mguuni wakati Yanga wakimshangaa ghafla bao linatinga wavuni kwao. Haraka komandoo mmoja wa Yanga Sudi Mrinda maarufu kwa jina la Sudi Tall’ alishindwa kumvumilia na kumkamata na kwenda kumtupa nje kitendo hicho hakikuwafurahisha mashabiki wa Dicha na kumuona kama adui wao ingawa hakuna walichomfanya.

Shangilia ya Dicha acha kabisa

Ukiondoa timu za Uarabuni basi taifa linalofuata kwa kushangilia ni Ethiopia. Wakati timu yako inashambuliwa kama una moyo mwepesi unaweza kuanguka. Mashabiki waliotazama mchezo huo walikuwa na hamasa kubwa kwa timu yao muda wote wa mchezo waliwazomea Yanga na kuwapa nguvu timu yao kitu ambacho kwetu hakifanyiki watu wanashangilia bao tu na kuzomea wachezaji wao.

TFF ilitisha sana

Mafanikio ya Yanga kutinga makundi mbali na timu hiyo kupongezwa pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya uongozi wa Rais Wallece Karia walicheza nafasi yao vyema kwa kuipa nguvu Yanga.

Hapa Ethiopia TFF iliwakilishwa na Kaimu Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani ambaye alitangulia mapema hapa kuweka maandalizi sawa lakini pia kikosi hicho kikawasili na mjumbe wa Kamati ya Utendaji kanda ya Dar es Salaam, Lameck Nyambaya ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara.

Viongozi hawa walikuwa msadaa mkubwa wa Yanga kila ilipotokea changamoto.