Yanga: Bora aondoke zake angetuchomesha tu

YANGA imefumba macho na kuwaachia Simba urahisi wa kumpata kiungo Haruna Niyonzima baada ya kutangaza rasmi kwamba hawataendelea naye baada ya kushindana katika mazungumzo ya kuongeza mkataba.

Uamuzi huo wa Yanga ulitangazwa jana na Katibu Mkuu, Charles Mkwasa yametokana na kugomea mambo mengi kimaslahi katika mazungumzo baina ya pande mbili. Suala hilo liliwagawa wajumbe wa kamati ya usajili kwa baadhi kuona nahodha huyo msaidizi ameshindwa kuiheshimu klabu yao huku wengine wakitaka kupambana kumbakiza. Mmoja wa vigogo wa usajili wa Yanga aliiambia Mwanaspoti jana kwamba; “Haruna amebadilika sana,bora aondoke angekuja kutuletea matatizo kwenye timu.”

Ilivyokuwa ni kwamba baada ya Niyonzima kurudi nchini Ijumaa Juni 16 akitokea kwao Rwanda Yanga ilikutana naye Jumamosi usiku na kufanya naye mazungumzo lakini vigogo hao wakagundua kwamba mke wa kiungo huyo ndiye aliyekuwa anaweka ugumu katika makubaliano hayo na shughuli nzima ilihamishiwa Jumatatu Juni 19 jioni.

Ilipotimu siku hiyo, Niyonzima alikutana na mabosi wa Yanga na kujifungia katika moja ya ofisi ya kigogo wa kamati hiyo ya usajili wakitumia masaa matano kujadili maslahi ya mchezaji huyo ambapo alikubali kushusha dau lake la awali kiasi cha Dola 70,000 (sh153 milioni) mpaka 60,000 (Sh 130 milioni) huku akitaka mshahara wake upande kutoka Dola 3,000 (Sh 6.4 milioni) hadi 4,000 (Sh 8.5) ambacho Yanga walikubaliana nacho.

Utata katika mazungumzo hayo uliibuka pale Niyonzima alipotaka apewe kiasi chote cha fedha Dola 60,000 na kugoma kupokea Dola 40,000 (Sh 85 milioni) taslimu alizowekewa mezani na kuwachefua viongozi hao ambapo wakamzuga wakimwambia watakutana tena kesho yake kuendelea na mazungumzo hayo kumbe pembeni wakakubaliana kumpiga chini.

“Tangu Niyonzima aijue Yanga hatujawahi kumpa fedha zote za usajili kwa miaka yote sita aliyocheza hapa lakini safari hii alionekana kuwa na msimamo mkali na wa tofauti kwamba hataki kupokea fedha nusu anataka fedha zote lakini ikumbukwe kwamba hajawahi kutudai wala kusumbuana naye katika kumlipa anachotakiwa kulipwa,”alisema kigogo mmoja aliyekuwa anapambana kumbakiza Niyonzima bila mafanikio.

Baadaye uongozi wa juu wa Yanga ukakubaliana kwamba waachane na mchezaji huyo ambaye tayari Yanga ilishanusa na kuona kwamba Niyonzima alikuwa tayari ameshakubaliana mambo mengi na watani wao Simba akitaka kuona Yanga washindwe ili akatue Simba kirahisi.

Habari zinasema kwamba Yanga walifika mbali katika ushawishi wa kumbakisha Niyonzima wakimpa ahadi nono ya kumsomeshea watoto wake watatu lakini bado ahadi hiyo haikufua dafu kwa kiungo huyo kutaka kupewa mzigo wote taslimu ili aweze kuishindanisha na ile ofa aliyopewa na Simba.

Wakati Yanga ikichukua uamuzi huo na kujipanga kuyatangaza baadhi ya majina ya wachezaji wake wakongwe waliunyooshea uongozi wao kidole kwa kuchukizwa na hatua ya kiungo huyo kuwekewa fedha nyingi na kushauri aachwe aende anapotaka na kuwataka mabosi hao kusumbua akili kutafuta mbadala wake haraka.

Wakati Yanga ikifikiria uamuzi wa kuachana na Niyonzima juzi walipata taarifa kwamba kiungo wao huyo ambaye mkataba wake unafikia kikomo Julai 21 mwaka huu tayari alishakubaliana kila kitu na Simba na wakati wowote baada ya mkataba huo kumalizika atasaini mkataba mpya na kutangazwa rasmi. Endapo Niyonzima atamalizana na Simba, Wekundu hao watakuwa wamefanikiwa kusawazisha bao nje ya uwanja kwa kuwatuliza mashabiki wao kufuatia awali Yanga kutangulia kupeleka maumivu kwa watani wao hao kwa kumalizana na mshambuliaji Ibrahim Ajib ambaye Mwanaspoti linauhakika msimu ujao atavaa jezi za Yanga.

Rwanda washangaa

Kwa mujibu wa beki wa Rayon Sport ya Rwanda, Munezero Fiston ambaye alifeli majaribio Simba, alisema mvutano uliokuwa unaendelea baina ya Simba na Yanga, kuwania saini ya Niyonzima umempa ujiko staa huyo kuonekana alifuata kazi Tanzania.

“Simba na Yanga, huku Rwanda, zinaonekana ni taswira ya soka la Tanzania, kitendo cha klabu hizo kumgombania Niyonzima, tafsiri yake ni kwamba ameliwakilisha taifa letu vizuri kwamba amefanya kazi iliyowagusa wengi,” alisema.

“Si jambo dogo kwa timu ambazo zinazofahamika ni wapinzani wakali kumwania Niyonzima ambaye amecheza kwa muda Yanga, anaonekana kama lulu ni heshima kwake na kwa taifa letu,” alisema.

“Ukipita kwenye mkusanyiko wanamzungumzia Niyonzima kama shujaa ambaye anathamini kazi yake na pia kuwakilisha taifa lao, kulionyesha lina vipaji kama kwa Tanzania alivyo Mbwana Samatta,” alisema.