Wizi mkubwa Kumbe EPL wanaibiwa mchana kweupe

Muktasari:

Dirisha la usajili lililopita kulikuwa na tetesi nyingi za usajili, nyingine zilifanikiwa na nyingine zilibaki kama zilivyo.

L0NDON ENGLAND.  MTAANI kuna ubishi unaendelea! Kuna mashabiki wanadai eti Ligi Kuu England ni wateja wa Ligi Kuu Hispania! Wanadai wachezaji wakali kutoka EPL hujiona wamekamilika baada ya kutia miguu pale Hispania! Hii ipo vipi? Cheki stori hapa chini;

Dirisha la usajili lililopita kulikuwa na tetesi nyingi za usajili, nyingine zilifanikiwa na nyingine zilibaki kama zilivyo. Kati ya watu ambao walikuwa wakitajwa kuondoka katika klabu zao walikuwa ni Philippe Coutinho wa Liverpool na Eden Hazard wa Chelsea, wote walikuwa wakisakwa na klabu za Hispania Barcelona na Real Madrid. Ilishindikana kwa kuwa Liverpool na Chelsea waligoma kuwatoa, ila si kwamba pesa ilikuwa ni tatizo kwa klabu za Hispania na kibaya ni kwamba, wachezaji wenyewe walitaka kuhama na walilalamika kwa nini walibaniwa. Lakini, timu hizo zinajipanga kwa nguvu na bila shaka hakutakuwa na wa kuwazuia pale Januari, ambapo ni siku 43 kuanzia leo.

Na si hao tu wanaotakiwa Hispania, Dele Alli, Alexis Sanchez, Kevin De Bruyne na Mesut Ozil nao wana dalili ya kutimkia katika Ligi ya Hispania katika dirisha la usajili la Januari. Vile vile baada ya Harry Kane kuonyesha soka la maana na kufunga mabao ya kutosha huku akifananishwa na wachezaji walioteka dunia, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo iliibuka minong’ono kwamba mchezaji huyo atasakwa na klabu kubwa na kweli Real Madrid wakamuibukia kwa lengo la kumsajili.

Hata hivyo, ikashindikana kutokana na kuzuiwa na klabu yake ya Tottenham, lakini mwenyewe alikuwa radhi kuondoka.

Hiyo inamaanisha kwamba, wachezaji wanapoonyesha kiwango cha maana kwa miezi kadhaa basi huonekana wanafaa kuwa katika klabu za Barcelona ama Real Madrid, na wale ambao wanaonyesha kiwango cha wastani huonekana kuwa wanafaa kubaki England.

Licha ya Ligi Kuu England kuwa na umaarufu, ukweli ni kwamba ligi hiyo huwa inashindwa kuhimili vishindo vya usajili nyota wakali duniani mbele ya Hispania. Msimu uliopita Manchester United ilijitahidi na ikaishinda Real Madrid katika kumsajili Paul Pogba kutoka Juventus, lakini Real imeweka rekodi ya dunia mara mbili kwa kunasa wachezaji kutoka katika klabu za Manchester United na Tottenham yaani Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.

David Beckham naye alipokuwa maarufu duniani kwa uwezo wake uwanjani, alionekana ameiva tayari kwa kupambana akiwa Real Madid na sio Man United. Real ikamsaka na baadaye ikamnasa mwaka 02003. Hali kama hiyo pia ilikuwa kwa Ruud van Nistelrooy, ambaye wakati akiwa Manchester United alikuwa mshambuliaji wa kutakata akifunga mabao 150 katika mechi 219 pale Manchester United. Mchezaji huyo pia aliuzwa kwenda Real Madrid kwa stori kama hiyo hiyo.

Vile vile nyota mkali za zamani wa Arsenal Thierry Henry alisajiliwa na Barcelona Juni 2007. Cristiano Ronaldo akafuatia Real 2009, hiyo ni baada ya kuwika vya kutosha na kuonekana kwamba ligi inayomfaa ni Hispania, na kweli akahamia huko ambapo amepata tuzo za kutosha, za klabu na binafsi.Kama hiyo haitoshi, mwaka 2014 wakati Luis Suarez akipiga kazi ya maana pale Liverpool, Barcelona ikafahamu huyo ndiye mchezaji wanayemtaka. Wakaibuka na kumsajili kiulaini.

Sasa kuna wachezaji wakali wa Ligi Kuu Engaland ambao wanasakwa, Hazard, Coutinho, Dele, De Bruyne na Kane wapo kwenye rada kali ya Ligi Kuu Hispania, nani anajua mwisho wao? Ni wazi kuwikia katika kiwango cha juu.

Hata Christian Eriksen wa Spurs kwa wakati huu akiwa kwenye kiwango bora kabisa ameanza kuwindwa na Barcelona.

Luka Modric na Bale walipokuwa bora waliondoka England na kwenda Hispania. Hilo lilitokea pia kwa Michael Owen. Kuna mashabiki ambao wamekuwa wakilalamika kwa nini timu za England hazifanyi vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini jibu ni moja tu, wanawezaje kuchanua wakati wachezaji wao wakubwa huwa wanakwenda Hispania? Baadhi ya sajili ambazo EPL inajivunia katika siku za karibuni ni De Gea wa Man United, ambaye hata hivyo anataka kurudi Hispania.

Tamaa ya mastaa wengi wanaotamba kwenye ligi mbalimbali wanataka kwenda Hispania. Ronaldinho alipokuwa moto PSG, aliamua kwenda Barca licha ya kwamba Man United ilimtaka. James Rodriguez aliichagua Real Madrid mbele ya timu za England na hata Pierre-Emerick Aubameyang ndoto zake ni kwenda Real Madrid baada ya sasa kufanya vizuri huko Borussia Dortmund. Ligi ya Hispania inanasa waliobora. Hata hivyo, kipindi ambacho Hispania ilichemsha na kuipa England wachezaji kama Juan Mata, David Silva, Santi Cazorla, Diego Costa, Sergio Aguero, Fernando Torres, Yaya Toure, Fabregas na Nicolas Otamendi, hawa waliondoka Hispania na kuleta utamu EPL.