Wenger alivyovumilia vipigo vya kudhalilisha

Muktasari:

Kwa mtazamo huo, kocha Arsene Wenger atakuwa na mechi zisizopungua nane za kucheza kabla hajafungasha virago vyake na kuachana na timu hiyo yenye maskani yake Emirates. Katika mechi hizo zilizobaki, hakuna ukakika kama Wenger atakutana na vipigo vingine vikubwa kama alivyowahi kukutana navyo kwenye maisha yake ya kuinoa Arsenal.

KWENYE Ligi Kuu England, Arsenal imebakiza mechi tano. Lakini, wana mechi mbili pia za hatua ya nusu fainali kwenye Europa League dhidi ya Atletico Madrid. Ikishinda kwenye nusu fainali hiyo itakayochezwa nyumbani na ugenini, ina maana kikosi hicho kitakuwa na mechi moja zaidi, itakayokuwa ya fainali.

Kwa mtazamo huo, kocha Arsene Wenger atakuwa na mechi zisizopungua nane za kucheza kabla hajafungasha virago vyake na kuachana na timu hiyo yenye maskani yake Emirates. Katika mechi hizo zilizobaki, hakuna ukakika kama Wenger atakutana na vipigo vingine vikubwa kama alivyowahi kukutana navyo kwenye maisha yake ya kuinoa Arsenal.

Vipigo vizito, ambavyo Wenger alikumbana navyo Arsenal na hawezi kuvisahau ni pamoja na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 10-2 kutoka kwa Bayern Munich. Ilikuwa kwenye mechi ya hatua ya 16 bora, ambapo Arsenal ilichapwa 5-1 huko Allianz Arena, kabla ya kuja kurudiwa tena kwa kipigo kama hicho huko Emirates kwenye mechi ya marudiano, miaka miwili iliyopita.

Wenger anaondoka Arsenal na vipigo vyake vizito ambavyo amewahi kukutana navyo taji alipoajiriwa mahali hapo mwaka 1996.

Man United 6-1 Arsenal, Februari 2001

Hii ilikuwa mechi ya Ligi Kuu England. Siku hiyo, Dwight Yorke alipiga hat-trick wakati mabao mengine yalifungwa na Roy Keane na Ole Gunnar Solskjaer kuwafanya Manchester United kuongoza 5-1 hadi kufikia mapumzika. Bao la Arsenal lilifungwa na Thierry Henry. Kipindi cha pili, Man United iliongeza bao jingine lililofungwa na Teddy Sheringham na hivyo kumfanya Sir Alex Ferguson kuibuka na ushindi mkubwa dhidi ya mpinzani wake huyo na kuweka pengo la pointi 16 kileleni.

Tottenham 5-1 Arsenal, Januari 2008

Hiki ni kipigo kinachouma zaidi kwa Arsenal kupigwa nyingi hivyo na mahasimu wao Tottenham Hotspur. Kipigo hicho si tu kiliwaumiza kuchapwa na wapinzani wao bali kiliwafanya watolewe kwenye michuano ya Kombe la Ligi. Katika mechi hiyo, Spurs ilifunga mabao yake kupitia kwa Jermaine Jenas, Nicklas Bendtner kajifunga, Robbie Keane, Aaron Lennon ma Steed Malbranque kukifanya kikosi hicho cha Spurs kilichokuwa kikinolewa na Juande Ramos kutinga hatua inayofuatia kwa jumla ya mabao 6-2.

Barcelona 4-1 Arsenal, Aprili 2010

Sare ya 2-2 nyumbani kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya iliamsha matumaini kwa Arsenal kwamba wanaweza kuwasukuma nje ya michuano hiyo Barcelona. Na mambo yalizidi kuleta uhakika baada ya Bendtner kuifungia bao la kuonngoza kwenye mechi ya marudiano huko Nou Camp. Lakini, kumbe kulikuwa na Lionel Messi uwanjani, ambaye alizipindua ndoto za Arsenal kwa kufunga mabao manne peke yake kuifanya Barca kushinda 4-1 kwenye mechi hiyo na hivyo kusonga hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 6-3. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kipigo kingine kizito ni kila alichokumbana nacho San Siro, Februari 2012 kwenye hatua ya 16 bora, ambapo Arsenal ilichapwa 4-0. Mabao ya AC Milan yalifungwa na Kevin-Prince Boateng, Robinho mawili na Zlatan Ibrahimovic kwa penalti.

Man United 8-2 Arsenal, Agosti 2011

Kipigo kingine kizito kwenye Ligi Kuu England Arsenal inakumbana nacho kutoka kwa Manchester United. Katika mechi hiyo, Wayne Rooney alipiga hat-trick, Ashley Young akapiga mbili, kisha mabao mengine mpira uliwekwa wavuni na Danny Welbeck, Nani na Park Ji-sung. Arsenal wao walipata mabao yao ya kujifariji kupitia kwa Theo Walcott na Robin van Persie na baada ya mechi hiyo Wenger aliingia sokoni kufanya usajili kuboresha kikosi chake, lakini ndiyo hivyo imebaki kwenye rekodi kwamba kipigo kilikuwa kizito.

Liverpool 5-1 Arsenal, Februari 2014

Liverpool ilianzisha kipindi kibaya kabisa kwa Arsenal baada ya kuwashushia kipigo kizito huko Anfield. Katika mechi hiyo, katika dakika 20 tu za mwanzo, Arsenal tayari walikuwa wamepigwa Bao Nne, kupitia kwa Martin Skrtel, aliyepiga mbili, Raheem Sterling na Daniel Sturridge. Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Sterling alifunga tena na kufanya ubao wa matokeo kusomeka 5-0, lakini ya vijana hao wa Wenger kufunga bao lao la kujifariji kupitia penalti ya Mikel Arteta.

Chelsea 6-0 Arsenal, Machi 2014

Mwezi mmoja baada ya kutokea kuchapwa 5-1 na Liverpool, Arsenal walikwenda kukutana na kichapo kingine kizito huko Stamford Bridge, walipokwenda kukumbana na kipigo cha Bao Sita Bila. Hiyo ilikuwa mechi ya 1000 kwa Wenger tangu aanze kuinoa Arsenal na bahati mbaya alikumbana na mbaya wake kwenye ligi, Jose Mourinho, aliyekuwa Chelsea kwa wakati huo. Hadi dakika 17, tayari Chelsea walikuwa mbele kwa mabao matatu, yaliyofungwa na Samuel Eto’o, Andre Schurrle na Eden Hazard. Arsenal walipomteza mapema tu beki Kieran Gibbs kwa kadi nyekundu, ambayo alistahili kuonyeshwa Alex Oxlade-Chamberlain kwa sababu ndiye aliyekuwa amedaka mpira makusudi uliokuwa unaelekea wavuni. Chelsea iliongeza mabao yake kupitia kwa Oscar, aliyefunga mara mbili na Mohamed Salah akahitimisha hesabu.