Wenger akitoka tu hawa wanaingia

Pep Guardiola

Pengine unaweza kuona hili linaweza kuwa gumu, lakini ukweli ni kwamba kama Manchester City haitachukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, Pep Guardiola hatakuwa na kitu cha kuendelea kukifanya kwenye kikosi hicho hasa kutokana na pesa alizotumia kusajili tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Etihad. Guardiola ni mmoja wa makocha bora kabisa duniani na hakika ni mmoja wa watu ambao, wataweza kuvaa vyema buti za Wenger katika kuendeleza makali au kuifanya Arsenal kuwa tishio zaidi kwenye Ligi Kuu England kama anavyofanya kwa sasa akiwa na Manchester City.

Carlo Ancelotti

Hana kazi na hivi karibuni alikatalia ofa ya kuinoa Italia. Ancelotti alifutwa kazi huko Bayern Munich baada ya timu hiyo kuwa matokeo ya hovyo, lakini uzoefu wake na umahiri aliokuwa nao ni kitu ambacho kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa Arsenal. Ancelotti ana uzoefu pia na soka la England, ambapo alibeba taji la Ligi Kuu England na Kombe la FA mwaka 2000 akiwa na kikosi cha Chelsea. Hata hivyo, Mtaliano huyo alifukuzwa kazi kwa aibu baada ya mechi ya mwisho ya msimu iliyofanyika nyumbani kwa Everton uwanjani Goodison Park. Baada ya hapo alikwenda kufanya kazi katika klabu za maana ikiwamo Real Madrid.

Guus Hiddink

Kocha huyo Mdachi alishawahi kufanya kazi Chelsea, hivyo ni mtu anayelifahamu vyema soka la Ligi Kuu England. Kwa jambo hilo, akitua Arsenal hakutakuwa na tatizo katika kuwabadili na kuwafanya kuwa matata kwenye soka lake. Kwa muda wake mfupi aliokuwa Stamford Bridge, Hiddink alitengeneza urafiki mzuri na wachezaji na mashabiki wa Chelsea wakati alipotua kuchukua mikoba ya Andre Villas-Boas. Hiddink ni kocha mwenye uzoefu mkubwa hivyo kuifanya Arsenal kuwa imara si kitu kigumu kwake.

Diego Simeone

Mambo yake si mazuri sana huko Atletico Madrid, hivyo halitakuwa jambo gumu kwake kama atafuatwa na mabosi wa Arsenal kwenda kufanya kazi katika timu hiyo. Huko nyuma, Simeone alishawahi kuhusishwa na mpango wa kwenda kuchukua mikoba ya Wenger, hivyo kwa kipindi hiki haitakuwa kazi ngumu sana kumshawishi kutua kwenye Ligi Kuu England ili kwenda kupambana na changamoto tofauti baada ya kusumbuana sana na Real Madrid na Barcelona kwenye Ligi Kuu Hispania. Muargentina Diego Simeone ameiongoza Atletico kwa mafanikio makubwa na kuwa mmoja wa makocha wenye hadhi kubwa barani Ulaya kwa sasa.

Ronald Koeman

Hana siku nyingi tangu alipofutwa kazi huko Everton. Hata hivyo, Koeman si kocha wa kubeza kwa sababu kazi yake imeonekana wazi kwenye klabu za Ligi Kuu England wakati alipozinoa Southampton na Everton. Amekuwa kivutio kwa kila mtu kutokana na kazi yake aliofanya St Mary’s tangu aliporithi mikoba ya Mauricio Pochettino kabla ya kwenda kuendeleza huko huko Goodison Park. Anafundisha staili ya soka ambalo hakika litawakosha mashabiki wa Arsenal hasa ukizingatia kocha huyo si bahili katika kutumia pesa kusajili.

Antonio Conte

Kwa sasa ni kocha wa Chelsea, lakini kwa siku za karibuni jina lake limetajwa sana kwamba si mtu atakayedumu kwenye timu hiyo kwa miaka mingi ijayo. Walau kwa sasa Chelsea imeanza kufanya vizuri kitu kinachoonekana kuokoa kibarua chake, lakini hali ikiwa tofauti tu basi suala la kufunguliwa mpango litamhusu. Hapewi nafasi kubwa ya kuendelea kubaki Chelsea, lakini kama ataondoka Arsenal hawatakuwa wamefanya makosa watakapoingia sokoni kuichukua nafasi yake akawe mrithi wa Wenger huko Emirates.

Laurent Blanc

Hakuna ugumu wowote wa kuipata huduma ya Blanc kwa sasa kwa sababu Mfaransa huyo hana kazi kwa wakati huu. Uzuri wa Blanc ni Mfaransa mwenzake, Wenger hivyo watakuwa na nafasi ya kufanya mazungumzo mazuri ya namna ya kuendeleza makali ya timu hiyo. Uwezo wake wa juu alionyesha kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa unampa nafasi Blanc ya kwenda kufanya vizuri Arsenal, huku akiwa na uzoefu wa Ligi Kuu England kwa sababu aliwahi kucheza katika kikosi cha Manchester United.

Joachim Low

Kwa sasa bado ana mkataba na timu ya taifa ya Ujerumani hadi fainali za Kombe la Dunia 2018, lakini ni mmoja wa makocha wanaofaa kabisa kwenda kurithi mikoba ya Wenger huko Arsenal. Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani tu hapo na kama Wenger atakuwa anaondoka wakati huo, basi halitakuwa jambo gumu kwa Low kukubali kibarua cha kwenda kuinoa Arsenal huko Emirates na kupambana na changamoto ya kutambua mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Didier Deschamps

Kocha huyo wa Ufaransa anatamba na timu ya taifa ya nchi hiyo kutokana na kuwa na vipaji vingi ambavyo anaamini watatesa kwenye michuano ya fainali za Kombe la Dunia 2018.

Baada ya kufika fainali ya Euro 2016, Deschamps ameendelea vizuri kwenye kikosi cha Ufaransa na ni wazi aliwahi kufanya kazi kwenye klabu, alipotamba na AS Monaco, Juventus na Marseille na Ligi Kuu England anaifahamu vizuri kwa sababu alishawahi kuichezea Chelsea.

Brendan Rodgers

Kocha huyo wa zamani wa Liverpool atashtua wengi kama atachaguliwa kuinoa Arsenal baada ya Wenger. Mtindo wake wa kuifundishaji na kupenda soka la pasi nyingi linamfanya Rodgers kuwa na nafasi ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Arsenal yenye maskani yake huko Emirates. Anafahamu vyema mikikimikiki ya Ligi Kuu England baada ya kuwahi kuwa Swansea City na Liverpool na aliwahi kuwa kocha wa timu ya vijana huko Chelsea.