Wanaovaa viatu vya Iniesta hakuna matata

Muktasari:

  • Mabao ya Edin Dzeko, Daniel De Rossi na Kostas Manolas, yalitosha kabisa kuimaliza Barcelona katika mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo AS Roma kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 4-4, kufuatia kina Iniesta kushinda mechi ya kwanza iliyofanyika Nou Camp, 4-1.

BAADA ya kushuhudia timu yake, iking’olewa Ligi ya Mabingwa Ulaya, nahodha wa Barcelona, Andres Iniesta, alisema anafikiria kutundika daluga mwishoni mwa msimu huu.

Mabao ya Edin Dzeko, Daniel De Rossi na Kostas Manolas, yalitosha kabisa kuimaliza Barcelona katika mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo AS Roma kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 4-4, kufuatia kina Iniesta kushinda mechi ya kwanza iliyofanyika Nou Camp, 4-1.

Kichapo hicho kimemfanya Iniesta ajione hana tena kitu anachoweza kukifanya kwenye timu hiyo ya Catalan na badala yake amedai atafikiria kuachana na wababe hao wa La Liga wakati msimu utakapomalizika.

Hilo tuliache tu liamriwe na Iniesta mwenyewe, lakini kitu cha kutazama ni hiki, kama staa huyo ataondoka kwenye kikosi hicho, nani wa atachukua mikoba yake?

Kuna wachezaji watano wanaotajwa kuweza kuvaa viatu vya Iniesta na hata kama vitawapwaya, basi haiwezi kuwa kwa kiasi kikubwa hivyo.

5.Carles Alena

Hafahamiki sana. Carles Alena ni Mhispaniola na ndiye nahodha wa Barcelona B. Mechi yake ya kwanza kuchezea kikosi cha kwanza ilikuwa kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Hercules kwenye Copa Del Rey. Baada ya hapo, Alena amecheza mechi tatu kwenye La Liga, lakini kwa bahati mbaya bado Kocha Ernesto Valverde hajampa nafasi kwenye kikosi chake. Kinda huyo ni fundi wa kupiga pasi na ni mtulivu pia katika kutupia wavuni. Uchezaji wake hauna tofauti sana na Iniesta. Anatokea La Masia pia.

4.Arthur

Kwa taarifa zilizopatikana katika mtandao wa Barcelona, Wahispaniola hao wameshakubaliana na Gremio ya Brazil kwa ajili ya kunasa saini ya staa mwenye umri wa miaka 2, Arthur. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Barca imekubali kulipa Euro 30 milioni na Euro 9 milioni nyingine italipa kutokana na maendeleo ya mchezaji huyo ndani ya uwanja. Arthur ana uwezo mkubwa sana wa kukokota mpira na kupiga pasi matata, huku akiwa mkali wa kupiga chenga. Ana kila sifa zinazostahili kabisa kuvaa buti za Iniesta huko Nou Camp.

3.Jean Michael Seri

Mwafrika pekee katika orodha hii. Jean Michael Seri, raia wa Ivory Coast, kwa sasa anatandaza soka lake katika klabu ya Nice, inashiriki Ligi Kuu Ufaransa.

Kiungo huyu wa kati, alikuwa mbioni kujiunga na Barcelona, katika dirisha la usajili la majira ya joto, lakini dili hilo lilishindikana katika dakika za mwisho, kutokana na pande mbili kushindwa kuelewana kuhusu dau lake. Nice ilitaka kulipwa Euro 40 milioni na hapo Barcelona ikaamua kuondoka kwenye kinyang’anyiro. Seri amehusishwa pia na Manchester United, lakini litakuwa dili zuri kama atakwenda kumrithi Iniesta Nou Camp.

2.Marco Verratti

Marco Verratti ni mmoja kati ya viungo bora barani Ulaya kwa sasa. Veratti anatambulika zaidi kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kasi na maamuzi ya haraka.

Sifa nyingine ni uwezo wa kupiga pasi za uhakika, miguu mepesi na jicho pevu. Mtaliano huyo ana wastani wa kupiga pasi 92.7 za uhakika kwenye Ligue 1 msimu huu. Anapiga chenga na ni hatari kwa pasi za mwisho. Barcelona iliwahi kuhusishwa na mpango wa kunasa huduma yake, lakini PSG ikaweka ngumu. Kwa sasa anaweza kupatikana baada ya mwenyewe kuonekana kuwa tayari kuihama timu hiyo.

1.Christian

Eriksen

Staa matata na anachokifanya Tottenham Hotspur. Christian Eriksen hakuna timu isiyomhitaji kwa Ulaya na Barcelona itakuwa kwenye mikono salama kama itamnasa akachukue mikoba ya Iniesta. Katika Ligi Kuu England ameshafikisha asisti 46. Ni staa mwenye ubora wa kutumia miguu yote miwili na jicho pevu katika kutoa pasi ambazo hakika Messi atakuwa na kazi moja tu ya kupasia mpira kwenye nyavu.