Wamebebwa na dirisha dogo

Muktasari:

  • Baadhi ya timu zimekuwa zikilitumia vyema kuweka mambo yao sawa ikiwa ni siku chache tangu kuanza kuona vikosi vyao vipya vina upungufu au uimara gani.

INGAWA wadau wa soka nchini wamekuwa wakilipinga dirisha dogo ambalo hufunguliwa wiki chache tangu Ligi Kuu Bara msimu mpya kuanza, lakini asikuambie mtu, limekuwa likizisaidia baadhi ya timu kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya timu zimekuwa zikilitumia vyema kuweka mambo yao sawa ikiwa ni siku chache tangu kuanza kuona vikosi vyao vipya vina upungufu au uimara gani.

Mwanaspoti linakudokolea kwa uchache baadhi ya klabu zilivyoweza kunufaika kupitia dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15 mwaka jana na kufungwa mwezi mmoja baadaye japo TFF iliamua kuongeza siku nyingine za ziada.

SIMBA

Asante Kwasi ndiye aliyeongezwa katika dirisha hilo akitokea Lipuli na ndiye anayedaiwa kuchangia TFF kuongeza muda wa kufungwa kwa dirisha hilo, japo ilitolea udhuru mfumo wa usajili wa njia ya kielektroniki kuzingua. Ilikuwa zuga tu! Beki huyo tayari ameanza kulipa mapema Simba kwa kuifungia mabao mawili, moja la Ligi Kuu dhidi ya Singida na jingine la Kombe la Mapinduzi.

Mghana huyo amekuwa msaada ndani ya kikosi hicho kutokana na kucheza nafasi nyingi na kuziba baadhi ya mapengo awapo uwanjani na ndio maana anafanikiwa kufunga licha ya kucheza kama beki na kiungo, akifukia shimo la Method Mwanjali.

YANGA

Faida kubwa waliyoipata Yanga, kumwongeza Yohana Mkomola aliyetua ili kufukia mashimo yaliyoachwa na mastraika nyota wa timu hiyo walikuwa na matatizo mbalimbali ikiwamo majeraha na mambo mengine binafsi.

Hata hivyo, umri wake ni wa kuhitaji mafanikio, hivyo amekuwa anajituma na kucheza kwa nidhamu, akiwa kashaifungia timu yake katika Kombe la Mapinduzi, huku akionyesha uhai katika Ligi Kuu, japo hajaonyesha yale makeke yake ya Gabon. Mchezaji mwingine aliyesajiliwa Yanga katika dirisha hilo alikuwa Mkongoman Fiston Kayembe aliyekwama kutua kwa sasa kwa sababu ya hati yake ya kimataifa.

AZAM

Walimsajili straika Mghana Bernard Arthur, ambaye ameongeza nguvu katika safu ya mbele, ingawa bado anatazamiwa katika mechi za mzunguko wa pili kuwa moto, lakini tayari ameanza makeke katika Ligi Kuu akiifungia bao moja, mbali na mengine kadhaa katika mechi za kirafiki na Kombe la Mapinduzi.

Mghana huyo alitua kuchukua nafasi ya nduguye, Yahaya Mohammed pia kutoka Ghana ambaye kwa muda aliokaa Azam alishindwa kuziba pengo la Kipre Tchetche.

LIPULI

Iliongeza wachezaji saba ambapo baadhi ni Alexandra Ansong kutoka Ghana, Jamal Mnyate (Simba), Adam Salamba (Stand United), Miraj Mwilange-(Kurugenzi Mafinga) Kembo Nelson (Ngorongoro Heroes), Steven Sylvester (Pamba) na Daruwesh Saliboko (Ashanti United).

Licha ya kuwaongeza nyota hao bado Lipuli haijawa na matokeo mazuri, japo kuna uhai fulani kulinganisha na mwanzo wa msimu na pengine kinachowaumiza ni pengo la Kwasi aliyewabeba kwa mabao yake muhimu wakati akiichezea.

MAJIMAJI

Ilimchukua Wazir Ramadhani kutoka Lipuli na kikosi hicho kimeweza kutoka sare mechi mbili kwenye uwanja wao dhidi ya Azam na Singida United, kuonyesha imeimarika tofauti na ilivyokuwa katika mechi za awali.

Timu hii pia iliachana na straika wake mkongwe, Danny Mrwanda aliyepelekwa kwa mkopo JKT Mlale inayokaribia kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.

KAGERA SUGAR

Iliwachukua nyota wawili kutoka Singida United, Atupele Green na Pastory Athanas, bado mchango wao haujaanza kuonekana kwa asilimia mia, ingawa Athanas timu hiyo imeonekana kubadilika licha ya kufungwa na Simba 2-0.

Huenda wachezaji hao wakafanya vema katika mechi za raundi ya pili kwani ndio kwanza wamecheza mechi mbili tangu usajili huo ufanyike kwani ligi ilisimama kupisha Mapinduzi. Lakini iliachana na Ame Ali ‘Zungu’ aliyetimkia Ndanda FC.

SINGIDA UNITED

Usajili wa Dirisha dogo, waliutumia kwa kuwaongeza nyota watano ambao ni Danny Lyanga (Fanja Oman), Papy Kambale (Rwanda), Issa Makamba (Serengeti Boys), Ally Ngazi (Serengeti Boys) na Assad Juma pia kutoka Serengeti Boys.

Wachezaji hao wanaonekana kuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na uwezo ambao wanauonyesha kuisaidia timu hiyo hasa alichokifanya Kombe la Mapinduzi na walitolewa na Azam FC, nusu fainali.

Singida haikuanza vema VPL, lakini ujio wa wachezaji hao kimeonekana kuongeza makali dhidi ya wapinzani wao, Lakini iliwaacha Atupele Green, Frank Zakaria, Mohammed Titi na Pastory Athanas.

NDANDA FC

Iliwaongeza wachezaji watatu, Mrisho Ngassa, Ame Ali ‘Zungu’ na Salum Telela wameonyesha mchango wao ndani ya timu. Kadri ligi itakavyosonga mbele huenda wakawa wakali zaidi.

MBEYA CITY

Bado haijawa na matokeo mazuri, licha ya kuongeza wachezaji watatu kupitia usajili wa dirisha dogo, ambao ni Abubakar Shaaban, Abel Ndongo na George Mpole, pia iliachana na Mrisho Ngassa na Abdallah Juma.

STAND UNITED

Ilisajili wachezaji sita kupitia usajili wa dirisha dogo ambao ni Selemani Ndikumana (Burundi), Tariq Tariq (Transit Camp), Frank Zakaria, Mohammed Titi kutoka (U-20 yao), Abdallah Juma (Mbeya City) na Bigirimana Bless (Rwanda).

Licha ya kuongezwa kwao bado kikosi hicho ni tia maji tia maji kwa maana bado mchango wao hajaonekana ingawa katibu wa timu hiyo,Kenny Nyangi alidai ujio wao uliwafanya washinde dhidi ya Ruvu na Mbao FC.

NJOMBE MJI

Kocha Mrage Kabange aliwaongeza chipukizi wawili kutoka Mtibwa Sugar ambao ni Nickson Kibabage na Muhsin Malima, Lakini bado kikosi chake hakijawa na matokeo mazuri zaidi ya kuambulia vipigo dhidi ya wapinzani wao.

MBAO FC

Licha ya kumwongeza mchezaji mmoja ndani ya kikosi hicho, Metacha Mnatta kutoka Azam FC, timu hiyo inayofundishwa na kocha Ettiene Ndayiragijie bado, ilikuwa na ushindani wa juu, hivyo ni ngumu kuona mchango wa mchezaji huyo.

Lakini kwa upande wa Mwadui FC, Prisons, Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar, hawakuongeza nguvu vikosi vyao na bado vinaendelea kuonyesha ushindani wa juu.