Walikuwa juu, ghafla wamepotea kimtindo

KAKOLANYA

Muktasari:

Hata Ulaya jambo hilo limekuwa la kawaida, kumbuka ishu ya Fernando Torres ama Radamel Falcao kipindi walipokuwa wakicheza katika Ligi Kuu England

WATU wanaoitwa wahenga, tuwaheshimu. Ni watu walioumiza vichwa kutafuta misemo na methali zinazoendelea  kuishi miaka yote licha ya wenyewe kusepa.

Fikiria tu misemo kama ‘Ivumayo haidumu’ ama ‘Mpanda ngazi hushuka’. Ukiisikia unaweza kuiona ni ya kawaida, lakini ina maana kubwa kiuhalisia.

Misemo hiyo unaweza kuichukua na kuiweka kwa wachezaji wetu wa soka. Wapo baadhi yao juzi kati tu walikuwa hawaishi kutajwa midomoni kwa umahiri wao uwanjani, lakini ghafla tu sasa wameanza kusahulika na kugunwa.

Si jambo la ajabu kwa wachezaji kupanda na kushuka viwango kutokana na sababu mbalimbali zinazochangia jambo hilo. Kuna wakati wachezaji wanachemka kwa kupata majeraha ya mara kwa mara, kushuka kiwango kwa kulewa sifa ama kuwa na migogoro na viongozi ama makocha wao na kufanya waporomoke.

Hata Ulaya jambo hilo limekuwa la kawaida, kumbuka ishu ya Fernando Torres ama Radamel Falcao kipindi walipokuwa wakicheza katika Ligi Kuu England jinsi walivyoshindwa kung’ara tofauti na walipotamba katika klabu zao za awali.

Katika Ligi Kuu Bara inayoelekea ukingoni kwa sasa, kuna baadhi ya wachezaji waliokuwa nyota na kutabiriwa makubwa, lakini kwa sasa wameyumba kiasi cha kuwa na kibarua cha kurejesha heshima zao.

Mwanaspoti inakuletea baadhi ya wachezaji wa namna hiyo.

Beno Kakolanya- Yanga

Misimu miwili iliyopita, kipa huyo aliyekuwa Prisons alikuwa gumzo kwa umahiri wake ulioisaidia Prisons kumaliza katika nafasi ya nne katika msimu wa 2015-2016 na kuifanya Yanga imnyakue kwa makeke ikiwazidi akili watani zao Simba.

Kakolanya alihenyeka mwanzoni mbele ya makipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kupewa nafasi katika mechi za mwishoni  msimu uliopita na kung’ara.

Ilitabiriwa angeendelea kung’ara, lakini ujio wa Youthe Rostand na kupata majeraha ya mara kwa mara kabla ya kuingia kwenye mgogoro na mabosi wake juu ya fedha zake za usajili, vimemfanya kipa huyo kupotea na sasa ana kazi kubwa Jangwani.

Licha ya upinzani wake na Mcameroon, Rostand, lakini Kakolanya anakabiliwa na changamoto nyingine toka kwa kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili aliyeanza kutesa.

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’- Simba

Beki huyu wa kushoto wa Simba, msimu uliopita alikuwa gumzo kweli kweli, lakini safari hii ni kama amezimika kutokana na ujio wa Asante Kwasi na mkongwe Erasto Nyoni anayecheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

Tshabalala kwa sasa anasugua benchi na hii imetokana na majeraha aliyoyapata mwishoni mwa msimu uliopita na kumweka nje, aliporejea akajikuta akitaabika.

Si kwamba Tshabalala kachoka kivile, lakini ushindani wa namba na mifumo anayotumia makocha wa klabu yake, unampa kazi ya ziada kupambana kweli kweli.

Nadir Haroub ‘Cannavaro’- Yanga

Beki wa kati na nahodha wa Yanga kwa sasa amekuwa zilipendwa kwani hana nafasi katika kikosi cha kwanza, licha ya kwamba bado wamo.

Mkongwe huyo amepotea uwanjani kutokana na majeraha ya mara kwa mara, huku ushindani wa namba ndani ya kikosi ukimpa changamoto kubwa kwani Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani na sasa Said Juma Makapu wanamzibia nafasi.

Umri unaweza kuwa kikwazo cha mkongwe huyo kurejesha makali yake, lakini pia majeraha yasiyomuacha yanamvurugia na kama vipi Cannavaro angeamua kustaafu kwa heshima ili kupata heshima ya umahiri wake na muda mrefu alioichezea Yanga.

Thabani Kamusoko- Yanga

Mashabiki wameshaanza kumsahau kutokana na kuwa kwake nje muda mrefu. Majeraha ya muda mrefu yamemfanya Mzimbabwe huyo kusahaulika kwani ni muda mrefu hajarejea uwajani, huku timu yake ikiendelea kupata matokeo yanayowafanya mashabiki wamchukulie poa.

Kiungo huyo ana kazi ya kurejesha heshima aliyokuwa nayo kwa misimu miwili tangu alipotua Jangwani akitokea FC Platinum ya Zimbabwe. Tayari ameanza mazoezi mepesi, lakini hakuna anayejua kama atakuwa fiti tena mapema.

Mrisho Ngassa-Ndanda

Winga huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, alikuwa tishio kwa umahiri wake uwanjani, lakini alianza kuzimika tangu alipoondoka Jangwani na kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini katika klabu ya Free Stars State.

Mashabiki wameanza kumsahau kwani hata aliporejea nchini msimu uliopita na kutua Mbeya City, hakuwa na jipya na sasa anapambana na hali yake akiwa Ndanda.

ilitarajiwa Ngassa angeng’ara katika timu hizo ndogo kwa vile hazina presha kubwa kama Yanga, Simba ama Azam alizowahi kuzichezea na kuacha alama, lakini mambo yamekuwa magumu kwake na sasa ana kazi ya kufanya kuendeleza libeneke.

Haruna Niyonzima- Simba

Kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda, alifunika bwana! Uwezo wake wa kumiliki mpira, chenga za maudhi na kutoa pasi murua akiwa Yanga zilimjengea jina kubwa, kiasi hata ilipoelezwa anajiunga na Simba, mashabiki wa Yanga walipagawa.

Ndio, wapo waliofikia hatua ya kuchoma jezi yake kuonyesha hasira dhidi yake kwa kuondoka na utamu wake, kwenda kuupeleka kwa mahasimu wao, lakini kilichopo sasa ni aibu. Niyonzima ni kama hayupo nchini kwa jinsi nyota yake ilivyofifia.

Hajafunga bao wala kutoa pasi ya kuzalisha bao kwa timu yake na sasa anahaha kurejea uwanjani kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu.

Hata akipata nafuu na kurudi uwanjani atakuwa amechelewa na si ajabu akatemwa Msimbazi kwani amekuwa kama mfanyakazi hewa katika kikosi hicho.

Waziri Junior- Azam

Nani asiyejua umahiri wa straika huyo chipukizi aliyewahi kupiga mabao manne pekee yake wakati akiichezea Toto Africans kabla haijashuka Ligi Kuu? Waziri Junior alitabiriwa angeendelea na moto wake aliokuwa nao Toto wa kufumania nyavu kwa vile ametua katika timu inayoendeshwa kisasa na inayowapa nafasi vijana.

Tatizo kubwa linalomkabili mchezaji huyo ni majeraha ya muda mrefu na kumfanya kuwa mchezaji wa nje ya uwanja. Kazi anayo kurejea kwenye mstari aliokuwepo.

Omar Mponda-Ndanda

Utasema nini kuhusu straika huyo wa Ndanda, jamaa alifunika kinoma kwa kutupia kambani kiasi cha kuanza kuhusishwa kutua katika klabu kubwa.

Mponda aliyekuwa akiibeba Ndanda kwa mabao yake ndani ya Ligi Kuu Bara na hata katika Kombe la FA misimu miwili iliyopita, amezimika kama hakuwahi kucheza nchini kwa sababu ya kuwa nje ya uwanja kwa msimu huu kutokana na majeraha.

Anayo kazi ya kufanya ili kurejesha makali yake ni kama mtihani aliokuwa nao, Atupele Green aliyewahi pia kupitia Ndanda kabla ya kupotea alipotua JKT Ruvu na sasa akichezea Kagera Sugar baada ya kutemwa Singida United.

Jamal Mwambeleko- Simba

Huyu ni kiraka, anacheza nafasi ya beki wa kushoto na pia anakamua wingi ya kushoto.

Aling’ara msimu uliopita akiwa Mbao FC kiasi cha kuzifanya Simba na Yanga kumpigia hesabu na Msimbazi kuwazidi kete watani zao wa Jangwani.

Tangu atue Simba, Mwambeleko ni kama amezimika kwa kukosa kufanya yale yaliyotabiriwa wakati akisainishwa Msimbazi, hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba, licha ya mechi chache alizopewa kuonyesha uwezo wake.