Wako wapi makocha waliopita Simba, Yanga? -2

Muktasari:

  • Simba na Yanga zimefanya mbadiliko ya makocha mara 38 kwa kipindi cha miaka 18 tangu mwaka 2000, kuna muda iliwalazimu kuwarejesha baadhi ya makocha wao ambao iliwatimua.

VITI vya makocha wa Simba na Yanga ni kama vina moto vile maana ni makocha wachache ambao wamekuwa wakisalia ndani ya klabu hizo kwa zaidi ya msimu miwili.

Simba na Yanga zimefanya mbadiliko ya makocha mara 38 kwa kipindi cha miaka 18 tangu mwaka 2000, kuna muda iliwalazimu kuwarejesha baadhi ya makocha wao ambao iliwatimua.

Makocha ambao walitimuliwa Yanga na baadaye kurejeshwa kwenye klabu hizo ni Kostadin Papic, Hans Van Pluijm na Jack Chamangwana kwa Simba ni Milovan Curkovic na Patrick Phiri.

Jana tulianza zoezi la kukuletea wanachokifanya kwa sasa makocha waliopita kwenye klabu za Simba na Yanga kwa miaka 18 iliyopita, wapo wanaoendelea kutesa na wangine ndo wamepotea hivyo, endelea nayo...

JAMES SIANG’A-SIMBA

Siang’a hatunaye tena kwa sasa ni marehemu. Kocha huyo wa zamani wa Simba aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67, Bungoma kwao, Kenya.

Kocha huyo ambaye enzi zake aliwahi kuwa kipa mahiri, pia aliifunisha Timu ya Taifa ya Kenya kati ya miaka ya 1999 hadi 2000 na kutua Tanzania ambapo alijiunga na Simba ambayo aliinoa kwa miaka miwili (2001–2003) na kutimuliwa.

Kiwango chake bora cha kufundisha kiliipeleka Simba hatua ya makundi ya klabu bingwa Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika) mwaka 2003 baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Pia, alipata kibarua cha kuinoa Taifa Stars, Siang’a aliipa ubingwa Simba, 2002 wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati.

Baada ya kuifundisha Taifa Stars kwa mwaka mmoja, alizinoa klabu nyingine kama, Moro United, Expres ya Uganda, Mtibwa Sugar na Gor Mahia ya Kenya kabla ya kupoteza maisha, Septemba 9, 2016.

JACK CHAMANGWANA-YANGA

Chamangwana ni miongoni mwa makocha kutoka Malawi ambao wanajivunia kupata mafanikio nje ya taifa lake, jamaa ameifundisha Yanga na kuipa mataji kadhaa kwa awamu mbili tofauti.

Mara yake ya kwanza kuifundisha Yanga ilikuwa 2002 hadi 2004 ambapo kibarua chake kiliota nyasi, akaenda kuzunguka huko na baadaye akarejeshwa tena, 2007 ambapo hakuchukua muda akatimuliwa tena.

Kucheza kwake mpira kwenye kiwango cha juu kule Afrika Kusini kulimsaidia kocha huyo kupata madili kibao baada ya kuondoka Yanga, alizifundisha Kaizer Chief na Mmabatho Kicks.

Hata hivyo, hakufanya vizuri Afrika Kusini ambako alitimuliwa na kurejea kwao kwenye klabu aliyoichezea enzi zake ya Be Forward Wanderers ambayo kaka yake kwa sasa ni marehemu, George Chamangwana alikuwa mwenyekiti.

Alipofanya vibaya hapakuwa na cha undugu wala nini kaka yake alishiriki kumtimua Chamangwana kwenye nafasi hiyo mwaka mmoja nyuma kabla ya kifo chake, 2017.

TROTT MOLOTO-SIMBA

Msauzi Moloto mara baada ya kutimuliwa kwenye klabu ya Simba, 2005 alirejea kwao Afrika Kusini ambako aliwahi kuzifundisha, Maritzburg United na Mamelodi Sundowns ambayo iliweka rekodi chini yake kwa kushinda michezo 11 mfululizo.

Moloto kwa sasa ni mchambuzi wa soka Afrika Kusini na mawazo yake ya kiuchambuzi yamekuwa yakitumiwa sana na Jarida la Kick Off linalo chapishwa na Media24.

CHARLES BONIFACE MKWASA - YANGA

Licha ya Mkwasa ‘Master’ kuucheza mpira kwenye kiwango cha juu kuanzia ngazi ya klabu yake ya Yanga hadi Taifa Stars, hajawa na mafanikio makubwa kwenye ufundishaji wake soka.

Mkwasa aliifundisha Yanga kwa mwaka mmoja, 2001 na kutimuliwa kama ilivyokuwa kwa waliomtangulia kwenye nafasi hiyo ya ukocha, lakini mbali na kuifundisha Yanga aliwahi pia kuzifundisha Ruvu Shooting na Prisons ya Mbeya.

Kabla ya kuwa katibu wa Yanga kwa sasa, Mkwasa alikuwa kocha wa Taifa Stars na alipoona jahazi linazama aliamua kuachia ngazi nafasi hiyo ambayo alipokewa na Salum Mayanga.

NEIDOR DOS SANTOS-SIMBA

Baada ya kutimuliwa kwa mara ya kwanza , Patrick Phiri mwaka 2005 mikoba yake ilibebwa na Mbrazili, Neidor ambaye naye hakudumu Simba kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Neidor alionekana mzugaji ndani ya mwaka huo, akatimuliwa na kujiunga na Timu ya Taifa ya Bahamas ambayo kwenye viwango vya ubora wa soka vya Fifa, inashika nafasi ya 207.

2010 hadi 2011 alijiunga na kuifundisha Village United ya Jamaica, ndani ya mwaka 2011 akajiunga na Montego Bay United ya nchini humo ambayo ilimtimua mwishoni mwa mwaka huo.

Neidor ambaye miaka ya hivi karibuni aliifundisha Saint George ya Ethiopia na kibarua chake kuota nyasi kwa kutimuliwa, ametajwa kurejea kwao Brazil.

Fuatilia zaidi katika toleo la kesho…