WANATOFAUTIANA: Mo Dewji, Manji ni tofauti kabisa

Muktasari:

  • Sasa kuna mabilionea wenye kiburi, nyodo na jeuri. Mabilionea ambao wanaonyesha jeuri ya fedha zao, hata kama sio nyingi sana. Hawa ndio kina Floyd Mayweather na wengineo.

DUNIANI kuna mabilionea wengi. Kuna watu wana pesa zao hadi wanakera. Ndio hawa akina Bill Gates na wengine. Wana pesa kama mchanga.

Sasa kuna mabilionea wenye kiburi, nyodo na jeuri. Mabilionea ambao wanaonyesha jeuri ya fedha zao, hata kama sio nyingi sana. Hawa ndio kina Floyd Mayweather na wengineo.

Mayweather anaweza kutandika pesa juu ya kitanda chake chote kicha akachukua tu video fupi ya kuweka kwenye Instagram. Anaweza kwenda benki kuchukua fedha kibao za kwenda kupigia picha. Ana nyodo vilivyo na pesa zake.

Sasa huku kwenye soka kuna mabilionea wa aina mbili. Kuna wenye pesa lakini ni wapole halafu kuna wenye nyodo. Mfano katika soka la Bongo kuna mtu anaitwa Said Salim Bakhresa. Yawezekana ndiye bilionea mpole zaidi Tanzania.

Ana pesa ndefu halafu ni mkimya. Utasikia tu kanunua meli mpya, anajenga bandari, kafungua kiwanda, kajenga hoteli, anajenga mji na mengineyo. Huwezi kumsikia sana kwenye mambo mengine. Ana timu yake ya Azam FC, imetulia pale Chamazi na inafanya yake kimya kimya.

Upande wa pili kuna mabilionea Yusuf Manji na Mohammed Dewji. Hawa ni mabilionea wanazi wa timu zao. Dewji anaipenda Simba halafu Manji anaipenda Yanga. Huwaambii kitu kuhusu timu zao.

Manji aliifanya Yanga kuwa timu tishio nchini kabla ya kujiweka pembeni mwaka jana. Baada ya hapo, Dewji ameanza kuifanya Simba kuwa tishio. Kila mmoja anatamba kivyake.

Pamoja na wote kuwa kwenye timu hizo kwa nyakati tofauti, Mwanaspoti inaangazia namna mabilionea hao wamekuwa wakiendesha mambo. Nani ni jeuri zaidi? Nani ni kiburi zaidi.

Mambo yafuatayo yanaonyesha tofauti ya Manji na Dewji kwenye soka la Bongo. Nani mbabe?

USAJILI WA NGUVU

Nani mwenye ubavu mkubwa kwenye usajili kati ya Dewji na Manji? Ni swali linalohitaji utulivu mkubwa sana kulijibu.

Mwaka jana Simba ilifanya usajili wa Sh1.3 bilioni. Ilitumia fedha nyingi kuliko timu nyingine yoyote Ligi Kuu. Je huu ndio usajili mkubwa zaidi kuwahi kufanywa nchini? Ni vigumu kusema.

Simba ilimsajili nani? Emmanuel Okwi, John Bocco na Haruna Niyonzima ndiyo wachezaji ghali zaidi waliotua Simba. Aishi Manula na Shomary Kapombe walikuwa ghali pia. Wengine ni kawaida. Kuna mchezaji mmoja wa Simba aliyegharimu Dola 100,000? Hakuna.

Ni kweli Dewji anatumia fedha kwenye usajili lakini hajamfikia Manji. Tathmini inaonyesha hivyo.

Manji huwa anatumia fedha nyingi zaidi. Amewahi kumsajili Obrey Chirwa kwa dau linalotajwa kufikia Dola 100,000 (Sh220 milioni). Aliwahi kulipa fedha nyingi pia kwa kina Donald Ngoma, Kpah Sherman na wengineo.

Bilionea huyo anatajwa kama mtu aliyeharibu zaidi soko la usajili hapa nchini. Aliwafanya wachezaji kuwa ghali. Mpaka leo hakuna timu nchini imewahi kumpa Okwi pesa nyingi kama aliyopewa na Yanga wakati ule inamsajili mwishoni mwa 2013 au alivyomwaga pesa kwa Juma Kaseja hadi akamng’oa Simba.

Kwa Manji, Dewji anatakiwa kuendelea kutumia zaidi. Simba inatakiwa kusajili wachezaji mahiri zaidi Afrika. Mpaka sasa kwenye usajili, Manji ndiye kiboko.

MISHAHARA JUU

Hapa ndipo kwenye upinzani mkubwa sasa. Manji enzi zake alifanya wachezaji kuwa na mishahara ya maana zaidi nchini. Yanga ilizidiwa tu na Azam iliyokuwa inawalipa fedha nyingi kina Kipre Tchetche na Sergie Wawa.

Yanga ya Manji ilikuwa timu ya pili kwa orodha kubwa ya mishahara nchini. Nasikia kwa sasa MO amepindua meza na kuifanya Simba kuwa juu zaidi. Kwa hili, ametisha sana.

Dewji anaweza asiwe amefanya usajili mkubwa kama wa Manji, ila kwa mishahara amefunika. Simba iko vizuri zaidi kwenye sekta hiyo. Manji akirejea Jangwani, ni lazima amwage mkwanja zaidi ili kushindana na Simba ya sasa.

THAMANI YA NEMBO YA KLABU

Watu wa masoko wananielewa vizuri zaidi kwenye eneo hili la brandi. Ni namna unavyoitambulisha bidhaa yako sokoni. Ni namna unavyoifanya bidhaa yako iwe ya kipekee zaidi sokoni na kuwa juu.

Kwa hili Dewji amepambana zaidi ya Manji. Simba imejitofautisha na kuwa brandi kubwa sokoni. Imeizidi Yanga ya Manji.

Japo baadhi ya vitu vilianza kufanyika kabla ya uwepo wa Dewji, lakini naye amekazia mambo. Mfano kabla yake kulikuwa na Simba Day pamoja na Simba APP ambayo inatoa habari mbalimbali za Simba.

Alichokifanya Dewji ni kuviongezea nguvu vitu hivyo. Simba Day inakuwa nzuri zaidi kama kuna usajili mkubwa umefanyika. Kwa hilo amefanikiwa.

Kwa upande wa Simba APP wameanzisha utaratibu wa mchezaji bora wa kila mechi pamoja na mchezaji bora wa msimu. Simba APP inaendesha kura za kuwapata hawa. Brandi yao ni kubwa sana.

Dewji amemaliza kazi kwa kuanzisha MO Awards. Hakukuwahi kuwa na kitu kama hicho hapo awali. Manji alishindwa katika nyakati zake, lakini MO Dewji ameweza. Huyu jamaa siyo wa mchezo mchezo.

USIMAMIZI WA TIMU

Kwenye eneo hili utampenda zaidi Manji. Aliifanya Yanga kuwa taasisi makini. Kuna wakati alihakikisha mapato na matumizi yamekaa vizuri na ripoti yake inatengenezwa na kubandikwa klabuni hapo. Hakutaka fedha yake ipotee.

Alifanya mambo ya Yanga kuendeshwa kisomi. Aliwatuliza watendaji wote wenye kimuhemuhe. Aliajiri watendaji wenye hadhi kubwa kama Jonas Tiboroha na wengineo. Yanga ilikwenda kwa weledi.

Manji alikuwa na mamlaka. Vitu vyote vya Yanga vilifanyika kwa kufuata utaratibu. Yanga iliweza kutunza siri kwa kiwango kikubwa. Wajanja wajanja wote waliwekwa pembeni.

Kwa Dewji bado hajafikia kiwango hicho. Pengine akiwa na mamlaka kamili na timu anaweza kufanya hilo. Kwa sasa bado yupo nje, hawezi kulaumiwa sana.

Simba bado ina wajanja wengi. Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘TryAgain’ amejitahidi kuwapunguza ila wengine bado wapo. MO akipata mamlaka kamili anapaswa kuwaondoa watu hawa. Yanga ya Manji iliweza, Simba ya Dewji nayo inapaswa kuweza.

HAMASA YA MECHI

Hivi kuna mtu amewahi kutoa ahadi za fedha nyingi kwenye soka kama Manji? Haijawahi kutokea. Kipindi cha nyuma Manji amewahi kutangaza dau la Sh100 milioni kwa wachezaji wa Yanga kama wataifunga tu Simba. Amefanya hivyo mara nyingi.

Japo mara nyingi alirejea na fedha zake maana Yanga haikuwa na miujiza yoyote mbele ya Simba. Kwa Manji kuahidi pesa na kutoa kwake sio jambo kubwa.

Wakati fulani alilipia viingilio ili mashabiki wa Yanga waingie bure uwanjani. Mwaka juzi tu hapa alitoa ofa kama hiyo kwenye mechi ya Yanga na TP Mazembe. Manji sio mtu wa mchezo.

Kwa upande wa MO Dewji ameweza kuwa na utaratibu mzuri pia wa hamasa, japo hajafikia kiwango cha Manji. Dewji huwa anachangia nusu ya posho zinazotolewa katika kila mechi ambayo Simba inashinda.

Huwa anaongeza kulingana na ukubwa wa mechi. Mfano Simba inapocheza na Yanga huwa anatoa nyingi zaidi, japo hawezi kumfikia Manji. Watu wa Yanga huwa wanasema, kwenye suala la kutoa Manji hana bajeti.

MFUMO WA MABADILIKO

Pengine kama Manji atakubali kuendana na matakwa ya mfumo wa sasa, lakini mapendekezo yake ya awali hayakuwa na matunda mazuri.

Wakati ule MO akitaka kununua hisa 51% za Simba kwa dau la Sh20 bilioni, Manji alitaka kuikodi Yanga kwa miaka 10 ili afanye biashara halafu akipata faida awe anawapa asilimia 25. Mfumo huo ulifeli kabisa.

Ulionekana kama mfumo wenye dosari nyingi na usioeleweka japo ulipelekwa haraka. Baadhi ya watu wa Yanga waliupinga hadharani.

Mo kwa upande wake aliendelea na harakati zile zile na sasa amekaribia kupata hisa asilimia 49 kwa fedha ile ile. Kwa hali ilivyo sasa, kuna uwezekano mkubwa mchakato wa MO ukakamilika mapema kabla ya Manji ambaye alitangaza kujiengua Yanga kabla ya kupingwa na wanachama, hajatafakari kitu kipya cha kufanya.