Vichwa vilivyonaswa kwa pesa nyingi Man United

Muktasari:

  • Hii hapa orodha ya wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye kikosi hicho cha Mashetani Wekundu katika zama zao za Ligi Kuu England.

MANCHESTER United kamwe haijawahi kuogopa kutumia pesa nyingi kusajili wachezaji inaowaamini wana viwango vikubwa vinavyokidhi haja ya klabu hiyo yenye maskani yake pale Old Trafford.

Hii hapa orodha ya wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye kikosi hicho cha Mashetani Wekundu katika zama zao za Ligi Kuu England.

PAUL POGBA,

PAUNI 89.25 MILIONI

Ndio usajili unaoshikilia rekodi ya uhamisho kwa sasa duniani ukimfanya Pogba kuwa mchezaji ghali kuliko wote baada ya uhamisho wake wa kutoka Juventus kutua Manchester United kuigharimu timu hiyo Pauni 89.25 milioni.

Man United ilitumia pesa nyingi kumsajili mchezaji ambaye awali alitokea kwenye akademi yao na kisha wakamwacha na kwenda Juventus mahali alikokwenda kupandisha kiwango chake cha soka na hivyo kumnunua kwa pesa nyingi.

ANGEL DI MARIA,

PAUNI 63.75 MILIONI

Staa wa Kiargentina, Angel Di Maria, alitua Manchester United akitokea Real Madrid kipindi hicho miamba hiyo ya Old Trafford ilipokuwa chini ya Kocha Luois van Gaal.

Kabla ya ujio wa Pogba, Di Maria alikuwa akishikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyesajiliwa kwa pesa nyingi zaidi klabuni Man United. Hata hivyo, staa huyo alidumu kwa msimu mmoja tu Old Trafford na kuuzwa kwenda Paris Saint-Germain ya Ufaransa.

ANTHONY MARTIAL,

PAUNI 51 MILIONI

Man United imeendelea kuonyesha kwamba wao hawana shida katika kutumia pesa baada ya kuweka rekodi kwenye uhamisho wa mchezaji kinda kwa kumlipia pesa nyingi wakati ilipomnasa staa wa Ufaransa, Anthony Martial kutoka AS Monaco.

Kwenye dili la kumnasa mchezaji huyo lililofanywa kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2015, Man United iliripotiwa kukubali kulipa Pauni 51 milioni kupata huduma ya fowadi huyo, imelipa pesa kidogo na itamalizia nyingine zilizobaki taratibu.

VICTOR LINDELOF,

PAUNI 40 MILIONI

Man United imekubali kulipa pesa nyingi kwa mara nyingine kumnasa beki wa kati kutoka Sweden, Victor Lindelof. Huu ni usajili wa kwanza kwenye dirisha hili la uhamisho wa wachezaji katika klabu hiyo na kwamba amekubali kutua kwenye timu hiyo akitokea Benfica kwa ada ya Pauni 40 milioni na hivyo kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa pesa nyingi waliosaini kuvaa jezi za Man United. Victor anaweza pia kucheza nafasi za beki wa pembeni na kiungo mkabaji.

RIO FERDINAND,

PAUNI 39.1 MILIONI

Beki Mwingereza, Rio Ferdinand alitua Man United akitokea Leeds katika majira ya kiangazi ya mwaka 2002. Kusaini kwake kuliifanya Man United kuvunja rekodi ya uhamisho wa wachezaji ndani ya Uingereza baada ya kutumia Pauni 39.1 milioni kwa beki huyo wa kati mwenye uwezo pia wa kucheza beki ya kukaba.

Ferdinand alicheza kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Man United na kuunda kombinesheni matata kabisa ya mabeki sambamba na Nemanja Vidic. Amebeba mataji 17 yakiwamo sita ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu 12 aliyokuwa hapo.

JUAN MATA, PAUNI 38.02 MILIONI

Mhispaniola, Juan Mata, ni usajili wa kocha David Moyes kwenye kikosi hicho cha Man United wakati alipomsajili kutoka Chelsea kwenye dirisha la usajili wa Januari mwaka 2014.

Mata alitokea Chelsea akiwa mchezaji bora wa mwaka kwa misimu miwili mfululizo, lakini baada ya ujio mwingine wa Jose Mourinho huko Stamford Bridge alifungua milango ya kiungo huyo kuondoka kwenda Old Trafford kabla ya yeye mwenyewe kwenda kuungana naye huko huko Man United na msimu uliopita walikuwa pamoja na kusifia kiwango cha kiungo huyo fundi wa mpira.

JUAN SEBASTIAN VERON, PAUNI 36.21 MILIONI

Alihesabika kuwa mmoja wa viungo mahiri kabisa waliowahi kutokea kwenye soka wakati Man United walipokwenda kuivamia Lazio kumnasa mwaka 2001.

Akatua Old Trafford kwa uhamisho uliokuja kuweka rekodi ndani ya Uingereza kwa kipindi hicho.

Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri kwa Muargentina huyo na akaondoka Man United kwenda Chelsea, ambako pia soka la Ligi Kuu England liliendelea kumkataa na kuamua kurudi kwao huko Argentina.

HENRIKH MKHITARYAN,

PAUNI 35.7 MILIONI

Maisha yake Old Trafford yalianza kwa kasi hafifu kabla ya kuuwasha moto na kuonyesha kwamba ulikuwa usajili bora wa Man United kutoka Borussia Dortmund kwenye dirisha la uhamisho wa wachezaji la majira ya kiangazi mwaka 2016.

Staa huyo wa Armenia, ameonyesha kwamba yeye ni mmoja wa viungo mahiri kabisa ndani ya Ulaya na uwezo wake wa kufunga mabao matata umemfanya kushinda tuzo ya Bao Bora la Mwezi kwenye Ligi Kuu England msimu uliomalizika.

DIMITAR BERBATOV, PAUNI 32.3 MILIONI

Straika huyo wa Bulgaria alijiunga na Man United akitokea Tottenham mwaka 2008 katika siku ya mwisho ya kufunga dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Siku hiyo, Berbatov aliwakacha Manchester City na kwenda kujiunga na mahasimu wa timu hiyo Man United na baada ya kutua Old Trafford akaripotiwa kuwa mrithi wa Eric Cantona kutokana na kuwa na kipaji kikubwa na kontroo za hatari.

Katika miaka yake minne aliyodumu kwenye kikosi cha Man United amebeba Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Klabu Bingwa Dunia.

ERIC BAILLY,

PAUNI 32.3 MILIONI

Huu ulikuwa usajili wa kwanza wa Jose Mourinho klabuni Man United baada ya kuwa kocha wa timu hiyo wakati alipomnasa Muivory Coast, Eric Bailly, kutoka Villarreal Juni 2016.

Beki huyo wa kati kwa haraka sana aliyazoea mazingira ya Ligi Kuu England na kumfanya awe mmoja wa usajili bora kabisa uliofanyika kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana na msimu ujao atakuwa na pacha mwingine baada ya Old Trafford kumnasa beki mwingine wa kati, Victor Lindelof, kutoka Benfica.