Uzoefu uliwabeba Simba Kambarage

Muktasari:

  • Mwanaspoti iliyokuwa mubashara ikifuatilia mpambano huo mwanzo mwisho na kukuainishia namna dakika 90 za mtanange huo ulivyokuwa bab’ kubwa japo wageni walibebwa na uzoefu wao, huku Mwadui wakionyesha kubadilika kimtindo.

JUZI Alhamisi Simba ilikuwa mjini hapa kwa mchezo wao dhidi ya wenyeji, Mwadui katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na timu hizo kushindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.

Mwanaspoti iliyokuwa mubashara ikifuatilia mpambano huo mwanzo mwisho na kukuainishia namna dakika 90 za mtanange huo ulivyokuwa bab’ kubwa japo wageni walibebwa na uzoefu wao, huku Mwadui wakionyesha kubadilika kimtindo.

Okwi atoa gundu

Straika huyu wa Simba, raia wa Uganda juzi alitoa mkosi mguuni mwake kwa kufunga bao nje ya jijini la Dar es Salaam. Kabla ya bao lake la penalti kwenye mchezo huo, Okwi alikuwa hajafunga bao lolote nje ya jiji la Dar na kufanya wapinzani wake kumbeza.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa Okwi akiandikisha bao lake la 14 msimu huu kwa mkwaju wa penalti, likiwa ni bao la pili kwa timu yake na lilipatikana katika dakika ya 67 baada ya kuangushwa na beki wa Mwadui, Joram Mgeveke ndani ya 18.

Bao hilo bila shaka limewanyamazisha waliokuwa wakimkejeli, kwani katika mechi tano za awali za mikoani, straika huyo alitoka kapa kwa kushindwa kufunga. Kabla ya bao hilo na hata baadaye, Okwi alionyesha uchu wa kutaka kukata mzizi wa fitina ugenini na juhudi zake zilimbeba kiaina.

Rekodi ya Simba

Simba ndio vinara wa Ligi Kuu ikiwa na alama 42 na juzi waliendeleza ubabe wao kwa kucheza mechi ya 18 bila kupoteza mchezo na sare ya juzi ilikuwa ni ya sita.

Licha ya mkwara wa Kocha, Ally Bizimungu wa Mwadui kuwa lazima awatulize Simba, uzeofu uliwabeba vijana wa Msimbazi na kuwanyamazisha Mwadui uwanja kwao kwa sare hiyo. Mwadui walilazimika kuchomoa bao la pili dakika za lala salama.

Mechi ya juzi ilikuwa ya 18 kwa Simba, ni sawa na dakika 1,620 bila kupoteza ikiwa timu pekee iliyolinda rekodi kwani Azam na Yanga waliokuwa wakienda nao pamoja kukwama mapema njiani wakipoteza mechi zao.

Mabao ya kideoni

Moja ya vitu ambavyo vilivutia mchezo huo ni jinsi mabao matatu yalivyofungwa kifundi kwa pande zote, lakini zaidi yale ya Mwadui kwa namna yalivyokuwa ya kiufundi zaidi.

Simba ndio walitangulia kupata bao dakika ya tisa lililofungwa na John Bocco kwa kichwa akiunganisha mpira wa faulo uliochongwa vyema na Shiza Kichuya, bao hilo lilikuwa tamu kwa kweli.

Ukiachana na bao la Bocco, David Luhende alionyesha uwezo wake kwa shuti la moja kwa moja alilonyoosha hadi wavuni, shuti ambalo lilikuwa ni mpira wa adhabu mita chache tu kutoka eneo la hatari ikiwa ni dakika ya 59.

Lakini mabao yote hayo ya Bocco na Luhende yalizimwa kabisa na lile la dakika ya 89 lililonyooshwa vyema na Paul Nonga na kupigiwa makofi uwanjani mzima.

Straika huyo aliyewahi kuichezea Yanga, aliunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa tena na Luhende na kuisawazishia timu yake, huku mashabiki wakiamini kuwa Simba inaondoka na ushindi wa mabao 2-1.

Bao hilo lilionekana kuwashangaza na kuwakera mashabiki wa Simba na benchi la ufundi, huku wakereketwa wa Mwadui wakijimwaya mwaya uwanja mzima pamoja na benchi la ufundi chini ya Kocha wake, Ally Bizimungu likirukaruka.

Mwamuzi kituko

Licha ya pambano kuwa na nguvu sawa kwa timu zote kuonyesha uwezo wao, hasa kwa mchezaji mmoja mmoja, lakini burudani uwanjani ilikuwa ni Mwamuzi, Shomari Lawi kutoka Kigoma. Mwamuzi aligeuka kituko kwa kusimamisha pambano hilo ili kupoza koo kutokana na jua kali lililokuwa likiwaka mjini hapa.

Refa huyo alianza kusimamisha mpira kwanza na kusogea karibu na kibendera na kunywa maji, huku mashabiki wakishangilia na wengine kumzomea kuwa jua limemuingia, wakati huo jua lilikuwa la ukweli.

Kali zaidi kwa refa huyo, alipotoa penalti kwa Simba huku Mgeveke akionekana wazi aliingiliwa na Okwi ‘kiufundi’ bila mwamuzi kumuona na Mganda huyo kutumia uzoefu kumdanganya mwamuzi aliyetoa adhabu iliyolalamikiwa.

Ukiangalia adhabu hiyo ni kwamba Mgeveke hakudhamiria kumchezea vibaya Okwi, kwani hakuwa mbele yake wakati akijiandaa kuanua mpira langoni mwake.

Kituko kingine ni wakati akitaka kumaliza mchezo, kwani aliudaka mpira ukiwa unaelekea kwenye lango la Simba na kupuliza kipyenga akiashiria mechi imeisha na kuzua kelele kwa watazamaji wakishangaa na kumshangilia kwa kitendo hicho.

Bocco aliinyima Simba pointi tatu

Kitendo cha nyota wa Simba, John Bocco kutolewa uwanjani baada ya kuumia, kilionekana kuwadhohofisha Simba, kwani hata alipoingia Laudit Mavugo, eneo la ushambuliaji lilipwaya kwa kiasi kikubwa.

Bocco alikuwa akishirikiana vema na Okwi, huku Kichuya na Said Ndemla wakigawa mipira, ilikuwa ni pigo kwao mara alipotolewa kwani mipira mingi ilikuwa ikiharibika tu.

Yale mahusiano yaliyokuwapo kati ya Okwi na Bocco mwishoni, yalikata ghafla kwani hata Mavugo alionekana kukwama asilimia zote sambamba na Okwi wake.

Pia safu ya ulinzi ya Simba ilionekana kuwa butu, haswa alipotolewa Juuko Murshid dakika ya 84 ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea Luhende rafu. Kitendo cha kutoka beki huyo tu, kilipeleka kilio kwa Msimbazi kwani faulo aliyopiga, Luhende ndio ilizaa bao la pili na la kusawazisha kwa Mwadui FC.

Luhende mzuka tu

Beki huyu wa kushoto alionekana kuwa na nyota wa Mwadui kwa namna alivyohusika na mabao yote mawili, akifunga la kwanza na kusababisha la pili.