Uhusiano wa Paul Pogba na Mourinho linaelekea ICU

Muktasari:

  • Nilimuuliza Mzee mmoja mtaalamu wa masuala ya usalama sababu ya yote haya wakati wangeweza kumlinda Rais wao chini ya bajeti. Akanijibu kwamba wakati mwingine wanataka kuonyesha ukubwa wao. Wanataka kuonyesha utawala na ubabe wao.

RAIS wa Marekani akija katika nchi ya dunia ya tatu basi utaanza kuona zinaanza kupaki Manowari za kijeshi. Watatua FBI, kisha CIA. Watazima mitambo mbalimbali ya nchi yenu. Watafunga barabara na watahakikisha wanakoroga mfumo wote wa ulinzi wa nchi yenu. Wataonyesha ukubwa wao na mwishowe itakuja ndege ya Rais, Air Force One.

Nilimuuliza Mzee mmoja mtaalamu wa masuala ya usalama sababu ya yote haya wakati wangeweza kumlinda Rais wao chini ya bajeti. Akanijibu kwamba wakati mwingine wanataka kuonyesha ukubwa wao. Wanataka kuonyesha utawala na ubabe wao.

Ipo katika soka. Ipo Real Madrid na pia kuna Barcelona. Wapo radhi uwafunge, lakini wanataka kuonyesha ubabe wao. Hawataki unyonge kabisa. Hawawezi kucheza mechi wakaweka mbele kipaumbele cha kujihami. Wanataka kukuonyesha Real Madrid ni nini. Wanataka kukuonyesha Barcelona ni nini.

Sir Alex Ferguson alikuwa anaonyesha hiyo Old Trafford au popote alipokwenda. Ndio maana halisi ya timu kubwa. Jose Mourinho sio kocha wa aina ya jeshi ya Marekani. Anaishi kwa hofu kuliko kuhofiwa.

Jose ametumia zaidi ya Pauni 300 milioni kwa miezi 24 tu iliyopita pale Old Trafford. Katika pesa hizo, kiasi kikubwa kwa mkupuo aliwekeza katika mwili wa Paul Pogba kutoka Juventus wakati dirisha la majira ya joto mwaka 2016. Pauni 89milioni sio pesa ya kitoto kabisa.

Mechi mbili kati ya tatu zilizopita benchi limemuita Pogba. Mechi dhidi ya Tottenham na mechi dhidi ya Newcastle United. Mchezaji bora zaidi wa United katika misimu hii miwili ni Pogba. Tulianza kushangaa dau lake, baadaye tukakubali kwamba hata kama hastaili, lakini ana kipaji maridhawa.

Kwanini benchi lilimuita Pogba katika mechi hizi mbili? Alikuwa fiti kabisa lakini Mourinho anataka kumpa Pogba majukumu mengine nje ya kile kipaji chake. Anataka Pogba awepo katika majukumu makubwa ya ulinzi kisha awepo katika ushambuliaji.

Pogba ninayemuelewa zaidi siku hizi ni yule ambaye anakabwa zaidi. Ana macho ya ziada katika pasi za mwisho. Lakini, pia ni mtawala wa eneo la kati kwa maana ya matumizi ya nguvu na akili. Pogba ni wa kuchungwa zaidi uwanjani na sio wa kuchunga zaidi.

Tatizo la Jose ametumia pauni 300 milioni na bado ameshindwa kuitengeneza United inayofanana na safari za Rais wa Marekani katika nchi ya dunia ya tatu. Wakati aliposema kwamba United haiwezi kushindana na Manchester City mpaka matajiri wa United waongeze pesa zaidi katika kikosi watu wengi tulishangaa.

Pesa ambayo Mourinho ameshatumia katika kikosi chake mpaka sasa inatosha kukimbizana na City. Tatizo la City sio pesa iliyotumika, hapana, ni staili ya Pep Guardiola katika kufundisha soka la kumtawala adui mpaka ajisikie mnyonge.

Kikosi ambacho Mourinho anacho, Pep angeweza kutwaa nacho ubingwa wa England bila ya pesa. Ni suala la staili na falsafa. Mechi zote mbili dhidi ya Tottenham na Newcastle, usingeweza kuona Jose anazifanya hizo timu zijisikie wanyonge. Ilikuwa kama vile anacheza na timu ambazo zina matumizi sawa sokoni. Pep sio kocha wa aina hii. Alifungwa na Liverpool, lakini wote tuliona jinsi ambavyo bado timu yake ilitawala mechi na kumaliza ikiwa shujaa uwanjani huku wakiwa katika kasi kubwa ya kutawala mechi na kujaribu kuchomoa bao la nne.

Kama una Pogba, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku, Antonio Valencia, Anthony Martial wote wanacheza kwa wakati mmoja, adui inabidi akimbizwe mpaka akohoe damu. Lakini badala ya hilo kutokea, unamtoa Pogba kwa madai anashindwa kukaba vema. Haiingii akilini.

Pogba ameshaanza kupata joto la Mourinho. Kipaji chake kinaanza kudhibitiwa na badala yake anapewa kazi ya kuwafukuza watu. Pogba na United ya leo inapaswa kucheza kama vile Jeshi la Marekani linapoingia nchi fulani. Wanapaswa kutawala kila kitu katika mechi. Labda mechi chache dhidi ya Real Madrid, Barcelona au Man City wanaweza kwenda kwa tahadhari kubwa zaidi. Hata hivyo, Jose ndivyo alivyo. Aliwahi kugombana na Juan Mata pale Chelsea kwa sababu hiyo. Amewahi kugombana na Cristiano Ronaldo pale Bernabeu, amewahi kugombana na Kevin de Bruyne pale Chelsea, amemtema Henrikh Mkhitaryan kwa sababu hiyo. Na sasa nahisi imewadia zamu ya Pogba. Bahati mbaya vita hii haitamsaidia sana Jose. Pogba inabidi aonyeshe kipaji chake. Ana uwezo wa kutawala mpira na kutawala timu. Jose atafute namna ya kuifanya United itawale kijeshi zaidi hasa dhidi ya timu kama Tottenham na Newcastle ambazo zipo chini ya uwezo wake.