UTATA: Umri na sura zao ni vitu tofauti

Muktasari:

  • Unajua hii ilitokana na nini? Dogo huyo kipindi hicho akiwa na miaka 17 tu, alikuwa akionekana kama mtu mwenye miaka 40 na kuzua utata mpaka alipofanyiwa vipimo na kubainika ni kweli alikuwa yanki tu, sema maisha yalimpiga tangu udogoni.

UNAIKUMBUKA ile ishu ya Joseph Minala na utata wake wa umri? Ishu hii ilitokea miaka minne iliyopita baada ya kiungo huyo Mcameroon aliyekuwa Lazio kuwababaisha wasimamizi wa soka wa Italia juu ya umri sahihi aliokuwa nao.

Unajua hii ilitokana na nini? Dogo huyo kipindi hicho akiwa na miaka 17 tu, alikuwa akionekana kama mtu mwenye miaka 40 na kuzua utata mpaka alipofanyiwa vipimo na kubainika ni kweli alikuwa yanki tu, sema maisha yalimpiga tangu udogoni.

Utata wake ulianza baada ya chombo kimoja cha habari nchini Italia kutumia sura yake ya kizee na kusisitiza dogo alikuwa amedanganya umri aliokuwa nao na kuungwa mkono karibu dunia nzima kabla ya Chama cha Soka cha Italia kumaliza utata na Minala kupona.

Sasa kama ilivyotokea kwa Minala miaka minne iliyopita, kwa sasa hapa nchini mashabiki wa soka wamekuwa kama waliopigwa ganzi kutokana kushindwa kuamini umri wa baadhi ya wachezaji wanaokipiga katika Ligi Kuu Bara.

Hii inatokana na ukweli wachezaji hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa na umri mdogo, ila ukiziangalia sura zao hazitofautiani sana na ile ya ‘Minala’.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya baadhi ya nyota hao ambao mwonekano wa sura zao hauendani na umri walionao.

AMISSI TAMBWE- YANGA

Straika huyo mkali aliyetua nchini mwaka 2013 na kufunika kwa umahiri wake wa kutupia kambani, ni kati ya wachezaji wanaoshangaza mashabiki.

Achana na uwezo wake wa kufumania nyavu akitumia miguu yote pamoja na kichwa kwa ufasaha, lakini utata wa umri wake ni jambo jingine linalosisimua mashabiki wengi.

Tambwe aliyesajiliwa Simba akitokea Vital’O ya kwao Burundi kisha kuhamia Yanga na kufanikiwa kutwaa Kiatu cha Dhahabu cha Ufungaji Bora mara mbili, muonekano wake unamfanya aonekane kibabu, japo ukichungulia vyeti vyake vinaonyesha ndio kwanza anajiandaa kufikisha miaka 30 tangu azaliwe.

Kwa sasa umri wake unasomeka miaka 29 na hadi Oktoba 24 ndio atatimiza 30 kamili.

EMMANUEL

OKWI- SIMBA

Straika huyu matata wa Simba naye anashangaza mashabiki kutokana na kuanza kung’ara muda mrefu tangu aanze safari zake za kuja na kutoka nchini kuanzia mwaka 2010 hadi leo akiwa anakipiga kwa Wekundu wa Msimbazi.

Ukimwangalia vema Okwi unaweza kudhani kibabu, lakini umri wake unasomeka miaka 25 na atatimiza miaka 26 wakati Wakristo duniani wakisherehekea Sikukuu ya Krismasi, kwani vyeti vyake vinaonyesha kazaliwa Desemba 25, 1992.

Usishangae, kusikia eti kwa mujibu wa vyeti Okwi ni mdogo kuliko John Bocco anayecheza naye Simba ambaye Agosti mwaka huu atatimiza miaka 29.

ELIUTER MPEPO-

SINGIDA UNITED

Nyota huyu mpya aliyesajiliwa na Singida United akitokea Prisons baada ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Kibongo ambao wanaduwaza mashabiki kwa mwonekano wake usiendana na umri alionao.

Cheti cha kuzaliwa cha Mpepo kinaonyesha alizaliwa Machi 3, 1999 hivyo kumfanya kwa sasa awe na umri wa miaka 19 tu, lakini sura na muonekano wake unaonyesha kuwa umri wake ni zaidi ya miaka 25.

KENNEDY WILSON- SINGIDA UNITED

Anatajwa kuwa mmoja wa mabeki wa kati wenye nguvu na stamina ya kiwango cha juu anayewapa ugumu washambuliaji wasumbufu pindi wakutanapo na timu yake.

Ukimtazama beki huyo kwa haraka haraka unaweza kudhani ana umri wa zaidi ya miaka 30 lakini cheti chake cha kuzaliwa na hati yake ya kusafiria vinaonyesha kuwa kwa sasa ana miaka 24.

ASANTE KWASI-

SIMBA

Kiraka wa Simba aliyesajiliwa katikati ya msimu uliopita akitokea Lipuli, naye wamo. Beki huyo wa kati anayemudu pia kucheza kiungo na mshambuliaji aliyetua nchini na kuanza kukipiga Mbao FC, ukimuangalia kwa haraka unaweza kudhani ni ‘Minala’.

Hata hivyo vyeti vyake buana vinamuonyesha kama mchezaji kijana mwenye umri wa miaka 22 na panapo majaliwa Agosti 13 atatimiza miaka 23. Unashangaa nini? Kwasi ana umri huo, japo muonekano wa sura yake ni kama anayejiandaa kuingia miaka 40.

PAUL BUKABA- SIMBA

Kabla ya kutua Msimbazi, hakuwa maarufu japo alishawahi kucheza Toto Africans miaka ya nyuma na kutimka zake nchini jirani za Burundi na DR Congo.

Beki huyo aliyejengeka vema kimichezo na aliyekuwa vikwazo kwa mastraika nyota katika mechi za Ligi Kuu Bara na michuano mingine akiwa na Simba, naye amekuwa gumzo kwa muonekano wake kutofautiana na umri alionao.

Kwa sasa mchezaji huyo mwenyeji wa Kanda ya Ziwa, umri wake kwa mujibu wa vyeti ni miaka 20 jambo linaloweza kumfanya hata Kocha wa Kilimanjaro Heroes’ kuweza kumtumia katika kikosi chake cha wachezaji wenye umri chini ya miaka 23, japo kimuonekano anaonekana ni mchezaji aliyevuka umri wa miaka 25.

WENGINE

Orodha ya wachezaji wenye kujitambulisha kuwa na umri mdogo, lakini kwa kuwaangalia na kufuatilia rekodi zao za nyuma zinakufanya ushtuke ni ndefu kweli, japo kuna baadhi wanabebwa na sura ya kitoto ‘Babyface’.

Miongoni mwa mastaa wanaochanganya mashabiki kwa kuwa na sura ya kitoto, lakini wakionekana kula chumvi za kutosha kwa mfano kama Juma Kaseja ambaye kwa sasa ndio kwanza ametimba miaka 33 tangu azaliwe amaMrisho Ngassa ambaye vyeti vyake vinaonyesha ana miaka 29, huku akicheza Ligi Kuu tangu 2005 akianzia na Kagera Sugar.