UKIWAHI TU, UMEWABEBA

Muktasari:

Klabu za Ligi Kuu England zitakuwa bize kupishana angani kwenda kuwashawishi mastaa hao wa ng’ambo ili kwenda kujiunga na timu zao kwa sababu itakapofika mwakani, huduma zao zipatikana bure kabisa.

LONDONENGLAND. ISHU ni kuchangamkia fursa tu na wanachosema watu ni kwamba, ujanja kuwahi!

Klabu za Ligi Kuu England zitakuwa bize kupishana angani kwenda kuwashawishi mastaa hao wa ng’ambo ili kwenda kujiunga na timu zao kwa sababu itakapofika mwakani, huduma zao zipatikana bure kabisa. Ujanja ni kuwahi tu.

Mario Balotelli (Nice)

Kwenye miaka 27, Mario Balotelli hawezi tena kujihesabu katika orodha ya mastaa watakaotamba kuutikisa ulimwengu na kubeba tuzo ya ubora wa dunia, ameshapita huo wakati. Kwenye Ligi Kuu England ni mchezaji anayefahamika vyema baada ya kucheza kwa mafanikio Manchester City kabla ya kwenda kufulia Liverpool. Kwa sasa kiwango chake kimeonekana kurudi akiwa na Nice ya Ufaransa, ambapo amefunga mabao 26 katika mechi 42 alizoichezea timu hiyo. Ripoti zinafichua kwamba staa huyo atapatikana bure tu msimu ujao, kazi iliyopo ni klabu za England tu kuchangamkia fursa.

Franck Ribery (Bayern Munich)

Winga huyo wa kushoto mwenye miaka 34 ni miongoni mwa wachezaji bora kabisa waliopata kutamba Ulaya ndani ya muongo mmoja uliopita. Soka lake limeleta mafanikio makubwa huko Bayern Munich. Tatizo la maumivu ya goti yametibua soka lake kwa siku za karibuni na kutia shaka juu ya hatima yake katika kikosi cha Bayern ambapo, mkataba wake umebakiza miezi tisa tu kufika mwisho. Kama hakutakuwa na dili jipya, basi staa huyo atapatikana bure kabisa msimu ujao na ukweli ni kwamba, miguu yake bado kuna kitu inachoweza kufanya ndani ya uwanja.

Leon Goretzka (Schalke)

Leon Goretzka, umri wake ndiyo kwanza miaka 22 tu na tayari amecheza mechi 12 katika timu ya taifa ya Ujerumani, akifunga mara sita akitokea kwenye kiungo katika soka la kimataifa. Alikuwa kwenye kikosi cha Ujerumani kilichobeba ubingwa wa Kombe la Mabara na katika kikosi chake cha Schalke tayari ameshafunga mara mbili katika mechi nane alizocheza msimu huu. Kiwango bora cha kiungo huyo tayari kimewavutia vigogo wa Ligi Kuu England kama Arsenal, Tottenham, Manchester United na Liverpool wakimtolea macho na kama hajasaini dili jipya, basi atapatikana bure tu msimu ujao.

Arjen Robben (Bayern Munich)

Winga asiyechuja kabisa, anapokuwa na mpira mambo yake si ya mchezo. Arjen Robben anaendelea kufanya mambo yake makubwa huko Bayern Munich, huku ubora wa pasi zake ukiendelea kuwa silaha tosha kwa mabingwa hao kuwaangamiza wapinzani wake kwenye Bundesliga. Baada ya kuachana na soka la kimataifa siku za karibuni, Robben sasa amewekeza nguvu zake katika soka la klabu tu, lakini kwa sababu mkataba wake unaelekea ukingoni na dalili za kuongeza dili jipya ni ndogo, hii ni nafasi kwa klabu za Ligi Kuu England kuchangamkia fursa ya kumsajili mchezaji huyo ili arudi England.

Giorgio Chiellini (Juventus)

Beki wa kiwango bora kabisa katika soka la dunia. Giorgio Chiellini ni beki wa kati mwenye kipaji kikubwa kutoka Italia, ambaye uchezaji wake umekuwa ukizifanya timu anazozicheza kuwa salama katika mechi zake. Mkataba wake wa sasa huko Juventus upo kwenye miezi ya mwisho na hali ilivyo baada ya kudumu Juventus kwa misimu 12, akicheze mechi 447, beki huyo hana kitu kingine cha ziada cha kuendelea kukifanya akiwa na timu hiyo ya Turin. Kwenda kwenye Ligi Kuu England pengine kitakuwa kitu kizuri kwenye mipango yake na kwa timu kama Arsenal na Liverpool zenye matatizo kwenye safu ya ulinzi, wakimpata Chiellini atawasaidia.