Tutabamba kinoma kimataifa tukiitengenza kesho ya soka

Muktasari:

  • Ubelgiji ilikuwa moja kati ya timu saba ambazo Brazil walikutana nazo na kuzifunga zote kwenye mashindano hayo, hadi wakatwaa ubingwa.

MWAKA 2002, Brazil waliifunga Ubelgiji mabao 2-0 katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia kule Korea Kusini na Japan.

Ubelgiji ilikuwa moja kati ya timu saba ambazo Brazil walikutana nazo na kuzifunga zote kwenye mashindano hayo, hadi wakatwaa ubingwa.

Kwa kufanya hivyo, Brazil ikawa timu ya kwanza, tangu 1970, kutwaa Kombe la Dunia kwa kushinda mechi zote, bila kutoa sare hata moja, achilia kupoteza. Cha kufurahisha zaidi ni, hata huo mwaka 1970, wao ndio waliofanya hivyo.

Hapa hatuzungumzii ushindi wa penalti baada ya sare katika muda wa mchezo, kama ilivyokuwa 1994 kwa Brazil, 2006 Kwa Italia au 1998 Ufaransa ambao walitinga nusu fainali kwa matuta dhidi ya Italia.

MICHEL SABLOM

Kwa Ubelgiji, kipigo kile kutoka kwa Brazil ni kama kilitonesha kidonda cha miaka miwili iliyopita pale walipokuwa wenyeji wa Euro 2000 (kwa kushirikiana na Uholanzi) na kujikuta wakiyaaga mashindano katika hatua ya makundi.

Aibu hii ikamfanya Rais wa Chama cha Soka cha Ubelgiji (KBVB), Michel D’Hooghe, akae chini na kutafakari kwa ajili kuandaa timu ya baadaye itakayokuwa mkombozi wa soka la nchi yao. Akampa kazi Michel Sablom, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa KBVB kuangalia namna ya kiufundi ya kulisogeza taifa mbele kisoka.

Sablom ni mtu aliyelijua vyema soka la Ubelgiji akianza kama mchezaji katika klabu ya Merchtem ya mjini Brussels na baadaye akawa sehemu ya benchi la ufundi la timu ya taifa kama Kocha Msaidizi kwenye Kombe la Dunia la 1986, 1990 na 1994.

Sablom alianza kwa kutengeneza falfasa ya kitaifa na kupendekeza mfumo wa 4-3-3 utumike kwenye akademi zote nchini humo.

Katika kufanikisha hilo, aliviomba Vyuo Vikuu vya Leuven, Ghent, Louvain-la-Neuve na Liege kufanya utafiti na kuchora ramani ya maendeleo ya soka kwa kulingana na mazingira ya nchi yao. Akamfuata Professa Werner Helsen wa Idara ya Elimu ya Viungo na Michezo ya Chuo Kikuu cha KU Leuven kumwomba aandae mfumo bora wa kisayansi wa uchezaji.

Helsen na wanafunzi wake sita wakaifanyia utafiti mikanda ya mechi mbalimbali kwa saa 1,500 wakiangalia muunganiko wa mchezo, pasi fupi fupi, idadi kuugusa mpira kwa kila mchezaji, utengenezaji mashambulizi na mipira mirefu.

Tafiti hizi zikaanza kuonyesha dalili ya matunda mwaka 2007, pale Eden Hazard na Christian Benteke walipokuwa kikosi cha vijana chini ya miaka 17 cha Ubelgiji kutinga Fainali ya Mataifa ya Ulaya na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 7-6 dhidi ya Hispania.

Mwaka 2008, timu ya vijana chini ya miaka 23 ikiwa na akina Vincent Kompany, Thomas Vermaelen, Marouane Fellaini, Jan Vertonghen na Mousa Dembele wakatwaa medali ya Shaba y Michezo ya Olimpiki za Beijing.

Eden Hazard, Vincent Kompany, Kevin De Britney, Christian Benteke na wengine kama wanavyoonekana kwenye nakala ya gazeti hilo, ambayo ilikuja kufukuliwa 2013.

Vijana 11 katika wale 15, wapo kwenye kikosi cha sasa cha Ubelgiji kilichotinga nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 kwa kushinda mechi zote huku wakiiondoa Brazil kwenye robo fainali.

SOMO KWA TANZANIA

Tanzania imeshafanya tafiti nyingi ambazo hazikufanyiwa kazi vya kutosha kuweza kutuletea maendeleo tuliyoyahitaji.

Dk Mshindo Msola alipokuwa Kocha wa Taifa Stars, alishawahi kufanya utafiti na kutoka na mapendekezo kadhaa ikiwemo kuzitumia kambi zetu za JKT katika kulea vipaji. Akapuuzwa!

Leodegar Tenga, katika siku zake za mwisho katika ‘Ikulu ya Karume’ akizindua mpango wa kiufundi wa maendeleo ya soka ulioandaliwa na mtaalamu Sunday Kayuni. Ukatupwa!

Wakati Sablom alishirikiana na baadhi ya vyuo vikuu vya Ubelgiji kuandaa kesho ya soka lao, sisi tunavitenga vyuo vyetu huku tukibahatika kuwa na watu kama Dk Jonas Tiboroha ambaye angeweza kufanya kazi kama ya Professa Werner Helsen na kutuletea falsafa moja itakayotutoa hapa tulipokwama.

Tuna cha kujifunza kutoka Ubelgiji!