Team Ronaldo de Lima noma

KOMBE la Dunia sasa zimebaki siku chache sana kabla ya kuanza kutimua vumbi. Wakati dunia ikitarajia kwenda kutazama vikosi vyenye mastaa wa aina tofauti wakionyesha ubabe, supastaa wa zamani wa Kibrazili, Ronaldo Luis Nazario de Lima, ameamua kutaja kikosi chake cha kwanza ambacho mwenyewe anaamini ndicho bora zaidi kuwahi kutokea duniani katika mchezo huo wa soka.

Akiwamo kwenye kikosi hicho, Ronaldo hakumpa nafasi Mbrazili mwenzake Neymar, wala Cristiano Ronaldo huku akiwapiga chini pia washambuliaji wengine makini kama Harry Kane, Antoine Griezmann na viungo wengine kama Andres Iniesta, Paul Pogba, N’Golo Kante na kuweka majembe ambayo, hakika kama yangepelekwa kwenye fainali hizo za Russia, suala la kubeba ubingwa isingekuwa kitu kigumu kwao. Hata Ronaldinho na Kaka hawapo unaambiwa!

1.Kipa: Gianluigi Buffon

Ametajwa kuwa kipa bora kwenye kikosi cha wachezaji wa kulipwa duniani mara tano tofauti. Buffon alitajwa pia kuwa kipa bora wa karne ya 21. Yote hayo yanamhusu Mtaliano huyo, ambaye aliwahi pia kunyakua medali ya ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Italia. Kwa Ronaldo, Buffon ndiye kipa mahiri zaidi kuwahi kutokea kuliko yeyote yule hapa duniani.

2.Beki wa kulia: Cafu

Hajawahi kutokea beki wa kulia matata kabisa kama Mbrazili, Cafu. Wakati sasa mabeki wa pembeni wakitumika kwenye kushambulia, Cafu alikuwa akicheza soka la mtindo huo miaka hiyo kabla ya 2000. Hakika alikuwa mchezaji aliyevutia kumtazama kwa kile alichokuwa akifanya uwanjani akiwahi pia kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Brazil.

3.Beki wa kushoto: Roberto Carlos

Marcelo anaonekana kufuata makali yake, lakini tofauti yake na Mbrazili huyo mwenzake, Roberto Carlos alikuwa mahiri kwenye kukaba na kushambulia, hapo hapo alikuwa hatari kwa kupiga mipira ya adhabu. Alikuwa akipiga pia kona na Ronaldo anadhani hakuna beki wa kushoto aliyekamilika zaidi na kuwa na vitu vingi kama alivyokuwa Carlos.

4.Beki wa kati: Paolo Maldini

Asikwambie mtu, kama taifa ambalo liliwahi kuwa na mabeki mahiri wa kati basi ni Italia. Kulikuwa na mabeki visiki hatari. Mmoja wao ni Paolo Maldini, ambaye alifanya mambo makubwa huko AC Milan alikodumu kwa miaka 25 kabla ya kustaafu mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 41. Alibeba mataji 26 akiwa na Milan na hakika Maldini hajapata kutokea mwingine.

5.Beki wa kati: Fabio Cannavaro

Mtaliano mwingine kwenye kikosi cha Ronaldo. Fabio Cannavaro siku za karibuni aliripotiwa kuwa huko China akikinoa kikosi cha Guangzhou Evergrande. Cannavaro alikuwa nahodha wa Italia wakati walipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2006, fainali zilizofanyika Ujerumani. Mashabiki wa Italia walimpachika jina la “Il Muro di Berlino” kwa maana ya ukuta wa Berlin kwa jinsi alivyokuwa akikaba.

6.Kiungo wa kati: Andres Pirlo

Pirlo lilikuwa suala la kawaida tu kwake kucheza kiungo mchezeshaji, lakini kwenye eneo la chini zaidi kwenye timu yake ya taifa na klabu. Kwenye kikosi hiki cha Ronaldo hakuna suala la kukaba sana, hao mabeki wa nyuma wanatosha kufanya kazi hiyo na hivyo kumchagua Pirlo kwenye kiungo ya kati kufanya timu yake kuwa na ufundi mwisho. Ulichopaswa kufanya ni kumpa tu mpira Pirlo.

7.Kiungo wa kulia: Diego Maradona

Diego Maradona kwa mgongo wake aliisaidia Argentina kubeba ubingwa wa dunia mwaka 1986. Alibeba pia mataji ya Copa America akiwa na kikosi hicho, lakini kubwa zaidi ni jinsi alivyokuwa akicheza soka la kiwango cha juu sana. Ronaldo anamsimamisha Maradona kwenye kiungo ya kulia, na anaamini ufundi wake utazidi kuifanya timu yake kuwa bora ndani ya uwanja na kutoa burudani kali.

8.Kiungo wa kati: Zinedine Zidane

Zidane alikuwa mmoja wa wachezaji mafundi wa mpira na wenye ujuzi mzuri wa kubadili mchezo wakati wowote kuwahi kutokea duniani. Kiungo huyo Mfaransa hawezi kusahaulika na Wabrazili kwa kile alichowafanya kwenye fainali ya Kombe la Dunia 1998 na 2006. Uhodari wake ulianzia akiwa mchezaji hadi kwenye ukocha alikoweka rekodi ya kubeba mataji ya Ulaya mara tatu mfululizo.

9.Mshambuliaji: Pele

Ukitaka kufahamu Pele hakuwa mtu wa kawaida kwenye soka cheki hadi makipa wanaofanya vyema, utasikia watu wanasema amecheza kama Pele pale, wakati mhusika mwenyewe hakuwa kipa. Hiyo ina maana mambo yote matamu kwenye soka yalikuwa yakifanywa na staa huyo wa Kibrazili, ambaye ameacha alama zake kibao kwenye soka la dunia, akiifungia Brazil mabao 77 katika mechi 92.

10.Mshambuliaji: Ronaldo

Sio Cristiano Ronaldo bali ni Ronaldo mwenyewe orijino. Amefunga mabao 247 katika mechi 343 alizocheza kwenye ligi. Alishinda Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia na amebeba ubingwa pia wa michuano hiyo, huku akiwahi kushikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa mabao mengi katika fainali hizo kabla ya Mjerumani Miroslav Klose kuja kutibua rekodi yake. Aliitwa El Phenomenon.

11.Kiungo wa kushoto: Lionel Messi

Ronaldo kimsingi hapa amejibu swali la Cristiano na Lionel Messi nani zaidi. Ameamua kumjumuisha Muargentina Messi kwenye kikosi chake na kumtosa Ronaldo wa Ureno kwamba hana nafasi kwenye timu hiyo. Messi amebeba tuzo tano za Ballon d’Or na atakuwa huko Russia kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia kujaribu kusaka rekodi ya kunyakua ubingwa wa michuano hiyo.