Soka la Tanzania ni mdogo mdogo mwendo wa kobe

WASWAHILI husema ‘Kawia ufike’ na pia wana usemi mwingine unaofanana kimaudhui na huo usemao ‘Mwenda pole hajikwai’. Katika maudhui hayo hayo, Waingereza wanasema ‘Slow but sure’.

Misemo hii na mingine mingi ya aina hiyo, inajaribu kutuonyesha kuwa ni vema ukachelewa, lakini ukawa na umakini wa kutosha katika kutenda jambo, shughuli, kazi au kutekeleza mpango wowote wa maendeleo.

Kiuhalisia kuna mahali nadharia hii na misemo hii inaweza kukubalika kutumika na ikawa na msaada kiasi cha kufanikisha malengo.

Lakini kwa dunia ya sasa ya utandawazi, iliyojaa ushindani katika mambo mbalimbali, si sahihi sana kuegemea kwenye misingi ya kuchelewa. Hizi si nyakati za kutembea polepole kwa hofu ya kujikwaa, lakini pia si nyakati za kuruhusu utendaji usiozingatia kasi na viwango.

Yaani unafanya mambo taratibu ili mradi ukiamini kwamba kwa vile upo kwenye mchakato wa kwenda mbele hata kama kasi ni ndogo unaweza kupata kile unachokihitaji, sio sahihi.

Sayansi na tekinolojia inajaribu kukinzana na nadharia hizo au misemo hii kwa sababu dunia ya sasa inazidi kurahisisha mambo kwa msaada wa matumizi ya nyenzo za kielectroniki katika nyanja mbalimbali ili kuharakisha kufika kule tunakotaka kwenda.

Maendeleo ya mpira hapa nchini yamekuwa kama jiwe linalosukumwa kupanda mlima badala ya kuteremka licha ya historia nzuri ya nchi yetu kuruhusu shughuli za michezo na burudani kuanzia tulipopata uhuru wetu mwaka 1961.

Kwa miaka yote hii sekta ya michezo imekuwa katika harakati mbalimbali za kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Kwa bahati nzuri, kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi hii ya Awamu ya Tano, zimehakikisha kuna wizara inayoshughulika na michezo, ndani yake ndipo lilipo Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) pamoja na vyama vingine vya michezo.

Watanzania ni miongoni mwa wanaoupenda sana mpira wa miguu, lakini hawajapata furaha inayofanana na mapenzi waliyonayo katika soka. Kisa ni kuendelea kufanya vibaya kwa timu zao.

Kufanya vibaya huko kunasababishwa na mambo mengi nje ya uchumi unaotajwa kuwa ndio chanzo. Kuna suala la usimamizi na uendeshaji wa soka lenyewe pia. Ninachokiona hapa kuna vitu tunavikosea ama havipo kabisa.

Kwa umri wa nchi yetu, tulistahili kuwa miongoni mwa mataifa kumi bora kwa soka Afrika.

Kwa misingi ya kufanya mambo ili tupige hatua, tunatakiwa tukiri kwamba mapungufu ni mengi kuliko viwango vya weledi katika usimamizi wetu wa mchezo huu.

Tangu tujitawale, Tanzania imeshindwa kabisa kuwa kwenye ubora wa soka katika Afrika, hii ni kuanzia klabu zetu hadi timu za taifa. Kila inapotolewa orodha ya ubora wa soka barani Afrika, mara nyingi Tanzania tunajitokeza nafasi za karibu na mwishoni.

Katika kudhihirisha kutofanya vizuri huko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alithibitisha hilo wakati wa kukabidhi kikombe na medali kwa wachezaji wa Simba waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Magufuli pia aliwapa mkono wa pongezi Serengeti Boys waliochukua ubingwa mbele ya vijana wenzao (wa umri chini ya miaka 17) wa Afrika Mashariki na Kati na timu yetu ya wasichana wanaoishi kwenye mazingira magumu walioshika nafasi ya pili kwenye Kombe la Dunia baada ya kuingia fainali na kufungwa na Brazil bao 1-0.

Kauli na maelekezo aliyotoa Rais, yanaonesha ni kiasi gani mwenendo wetu bado ni wa mashaka. Magufuli alionyesha wazi kwamba kinachoonekana si kinachotakiwa kuonekana. Unyonge na udhaifu wetu katika soka barani Afrika ni mkubwa.

Licha ya kutopendelea kwenda kushuhudia mchezo huu viwanjani, lakini Rais amethibitisha amekuwa ni mfuatiliaji mzuri wa maendeleo ya soka. Moja kati ya mengi yanayoathiri maendeleo ya soka ni timu zetu kuendelea kupata matokeo mabaya mara kwa mara.

Kimsingi hiki ndio chanzo cha kudorora mahudhurio ya watazamaji katika viwanja vyetu. Tumeshuhudia mechi nyingi za ligi mbalimbali hapa nyumbani zikikosa msisimko, viwanja havijai watazamaji. Ni dhahiri mapenzi ya mpira yanazidi kupungua. Hakika maswali ni mengi kuliko majibu.

Tatizo la kukosekana kwa kasi ya maendeleo ya kutosha katika soka letu linaonekana kuwa sugu. Yapo mambo yanayoendelea kuutafuna mpira wetu kama vile uzembe, kujisahau, malumbano na migogoro ya ajabu ajabu, matumizi mabaya ya ofisi na mambo mengine kama hayo, ambayo Rais Magufuli hakusita kuyagusia pia.

Katika awamu zote za uongozi wa TFF misukosuko haipungui. Zipo juhudi zinazofanyika za kuondoa tofauti na mikanganyiko, lakini bado tunasikia mapya yakiibuka. Matokeo yake muda mwingi unatumika kusuluhisha badala ya kuweka nguvu katika kubuni, kupanga mikakati na kuratibu maendeleo ya mpira wenyewe.

Kwa upande mwingine mnyumbuliko wa sera za maendeleo ya mpira kwenye shirikisho kulingana na mahitaji ya wakati uliopo, nalo ni jambo jingine la kutazamwa vizuri.

Itaendelea Ijumaa ijayo.