Siri ya Guardiola Kubeba Ubingwa wa Ligi 2018

MANCHESTER, ENGLAND

MANCHESTER City imechukua ubingwa wa Ligi Kuu England kwa staili ya aina yake. Sifa nyingi ziende kwa kocha wao, Pep Guardiola ambaye anajulikana kote kwa timu anazofundisha kucheza kandanda la kuvutia. Kuna uchawi mwingi ambao Guardiola anautumia kupata mafanikio. Kuna mambo ya nyuma ya pazia ambayo mengine hayafikii katika sikio la shabiki. Baadhi ya mambo ni haya hapa.

Muziki ndani ya Etihad

Kama uchawi hivi. Guardiola alihakikisha kwamba anawaunganisha wachezaji wake kwa umoja mkubwa. Moja kati ya uchawi wake ilikuwa ni kuhakikisha kuna wimbo maarufu wa kundi la Oasis unaoitwa Wonderwall unapigwa wakati wachezaji wakiingia katika vyumba vya kubadilishia nguo Etihad. Guardiola alitaka wachezaji wajisikie mashujaa na marafiki.

Apunguza urefu wa nyasi Etihad

Wakati Guardiola alipojiunga na City katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016 aliitisha mkutano wa wafanyakazi Etihad huku akiagiza kwamba nyasi za viwanja vyote vya mazoezi kuanzia timu za vijana hadi wakubwa kupunguzwa hadi milimita 19. Huu ni utaratibu wake hata wakati akiwa na Barcelona na kisha Bayern Munich. Kwa kufanya hivyo anaamini kwamba mpira unatembea kwa haraka zaidi

Azima mitandao ya simu

Akiwa mazoezini Guardiola alionekana kama vile yupo nyumbani. Wakati mwingine alikuwa anatembea katika korido za Etihad akiwa pekupeku. Aliamuru kuzimwa kwa Internet, au Wifi, katika baadhi ya maeneo ya mjengo wa Etihad kwa sababu alikuwa anataka wachezaji wasitumie simu na badala yake waongee zaidi wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya kujenga urafiki. Kwa namna hiyo hiyo, Guardiola aliwaamuru matajiri wa timu hiyo kutengeneza meza moja kubwa ya chakula ambayo iliwafanya wachezaji watazamane na kuongea wakati wa kula. Haishangazi kuona kwamba wachezaji wa City walikuwa na maelewano makubwa ndani na nje ya uwanja.

Mlo wa uhakika ulizingatiwa zaidi

Guardiola alikuwa mkali sana katika suala la mlo. Wakati alipotua City alimuonyesha mlango wa kutokea Samir Nasri kutokana na unene wake. Wachezaji ambao walikuwa wanarudi kwa maandalizi ya msimu mpya wakiwa wameongezeka uzito huwa wanafanyishwa mazoezi ya peke yao. Mara nyingi wachezaji wanakula pamoja baada ya mechi na kabla ya mazoezi. Guardiola amemuajiri mtu wa lishe aliyekuwa naye Barcelona, Silvia Tremoleda kwa ajili ya masuala ya chakula cha timu. Tremoleda huwa anaangalia pia hata lishe ya wachezaji kama Kevin De Bruyne, Ilkay Gundogan na Kyle Walker ambao wameajiri wapishi wao wenyewe.

Lugha ni Kiingereza tu

Kundi la wachezaji wa Manchester City lina wachezaji wengi wa mataifa mbalimbali lakini Guardiola ameamuri kwamba wachezaji wote lazima wafundishwe kwa lugha moja tu ya Kiingereza. Wachezaji kama Nicolas Otamendi na Aymeric Laporte wameendelea kujifunza lugha ya Kiingereza kwa kasi kwa sababu ndio njia pekee ya mawasiliano baina yao linapokuja suala la soka uwanjani.

Familia ni muhimu kuliko timu

Licha ya ukweli kwamba mastaa wa City wanalipwa mishahara mikubwa, lakini Guardiola amekuwa mtu mwenye upendo mkubwa kwa familia kiasi kwamba anaamini kwamba bila ya wachezaji kuwa karibu na familia zao hawawezi kumpatia mafanikio. Wachezaji wa Manchester City huwa wanalala na familia zao siku moja kabla ya mechi. Lakini pia Pep huwa anazijali familia kwa maana ya mchezaji mmoja mmoja. Msimu huu, kiungo David Silva alipata watoto mapacha waliozaliwa kabla ya muda nchini kwao Hispania na Guardiola alimruhusu Silva kwenda Valencia msimu mzima kila anapojisikia.

Wachezaji

Guardiola amekuwa na mbinu za ajabu za kurudisha ari kwa wachezaji baada ya vichapo., wakati hasimu wake, Jose Mourinho akijulikana kwa kubwatukia wachezaji wake ovyo baada ya vichapo, Guardiola huwa hafanyi hivyo. Baada ya kutolewa na vibonde Wigan katika michuano ya FA Februari mwaka huu, Guardiola aliwapa ruhusa wachezaji wake kwenda kwenye shindano ya kuchora. Msimu uliopita, baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Everton, yeye mwenyewe aliwachukua na kuwapeleka kutazama Sinema ya La La Land. Katika sherehe za Krismasi mahususi kwa ajili ya wachezaji na Wafanyakazi, Guardiola alicheza muziki kwa pa,moja na wafanyakazi wa kawaida klabuni hapo. Na licha ya kutwaa mataji 21 katika miaka yake saba pale Barcelona na Bayern Munich, Lakini Pep aliandaa sherehe maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wake kwa kumsaidia kutwaa taji lake la kwanza England wakati walipoichapa Arsenal na kutwaa kombe la Ligi Februari mwaka huu.

Mabosi ni washkaji zake

Wakati katika baadhi ya klabu makocha wamekuwa hawana uhusiano mzuri na mabosi wao, Pep ana uhusiano mzuri na Mtendaji mkuu wa City, Ferran Soriano pamoja na Mkurugenzi wa ufundi, Txiki Begiristain ambao wote aliwahi kufanya nao kazi Barcelona. Kwa mfano, licha ya kushindwa kuwanyakua, Alexis Sanchez na Riyad Mahrez katika dirisha la Januari, bado hakukuwa na tatizo baina yao. Kumbuka jinsi ambavyo Jose Mourinho alivyowabwatukia mabosi wa Manchester United akilalamikia kuhusu usajili baada ya kutolewa na Sevilla katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Wanaojua wamejua zaidi

Guardiola ametumia pesa nyingi tangu afike kwa ajili ya kuitengeneza Manchester City hii. Amewanunua Ederson, Mendy, Walker, Danilo, Laporte, Gundogan, Gabriel Jesus, Leroy Sane na Bernardo Silva, ambao wote wamepandisha viwango vyao kutoka walikotoka. Guardiola anaamini zaidi katika wachezaji kuimarika. Hata wachezaji aliowakuta wameimarika zaidi baada ya yeye kutua. Wachezaji kama Sergio Aguero, David Silva na Kevin de Bruyne wameimarika zaidi kuliko awali. Raheem Sterling ambaye msimu huu ana mabao 22 ikiwa ni mara mbili ya mabao ambayo alifunga msimu uliopita ameelezea jinsi ambavyo Guardiola alivyomwambia aachane na tabia ya kumiliki mpira kupitia nje ya mguu wake kwa sababu inapunguza kasi yake.

Msimamo wake ni ule ule tu

Wakati mwingine wachambuzi wamekuwa wakimshambulia Guardiola kwa kushindwa kubadilika wakati mambo yanapokwenda kombo uwanjani. Mwenyewe anaamini katika falsafa zake na kamwe hataki kubadilika. Muda mwingi tabia hii huwa inamsaidia.

Novemba mwaka jana katika pambano dhidi ya Huddersfield walikuwa wanaelekea kupata kichapo chao cha kwanza, lakini wakati wa mapumziko Guardiola aliwaambia wachezaji wake waendelee na mbinu hizo hata kama inamaanisha watapoteza mechi.

Ni kweli waliendelea na mbinu hizo hizo na wakashinda mechi.

Kwa karibu miaka 23, City walifanikiwa kubadili matokeo mara nyingi katika kipindi cha pili na kushinda mechi.

Kumbuka katika mechi dhidi ya timu kama Huddersfield, Southampton na West Ham walifunga mabao katika dakika za mwisho.