Simulizi ya Yanga inafurahisha, Kerr inasisimua

Muktasari:

  • Ni kama vile simulizi ya kijana wa kimasikini kupendwa na Binti mrembo wa kitajiri. Huwa inatokea mara chache sana. Tangu Zali la Mentali la Professor Jay mpaka leo haijatokea tena.

YANGA yenye umasikini uliopitiliza. Yanga yenye majeruhi kama hospitali ya Temeke ama Mwananyamala. Yanga iliyokimbiwa na kocha. Yanga yenye kila aina ya matatizo imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kweli Mungu yupo aisee.

Ni kama vile simulizi ya kijana wa kimasikini kupendwa na Binti mrembo wa kitajiri. Huwa inatokea mara chache sana. Tangu Zali la Mentali la Professor Jay mpaka leo haijatokea tena.

Ilihitaji roho ngumu sana kuamini kama Yanga inaweza kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo. Mechi ya kwanza hapa Dar es Salaam timu hiyo iliwakosa mastaa wake watano wa kikosi cha kwanza.

Kelvin Yondani ambaye ndiye roho wa safu yao ya ulinzi hakucheza. Papy Tshishimbi na Obrey Chirwa ambao ndio mastaa wakubwa zaidi kwenye timu hiyo kwa sasa hawakucheza. Amissi Tambwe na Donald Ngoma walishasahaulika kabisa.

Hata hivyo, Yanga ilishinda mabao 2-0 hapa nyumbani. Haikuwa kazi rahisi. Kuna watu walitoa jasho na damu. Kuna watu wamepambana kufanikisha hilo. Simulizi hii ya Yanga inafurahisha sana.

Imefuzu hatua ya makundi ya michuano ambayo imeishinda Simba yenye kila kitu. Simba yenye fedha za kutosha. Simba yenye makocha wa maana. Simba yenye mastaa wa maana ilishindwa lakini Yanga masikini imeweza. Inashangaza sana.

Pamoja na yote, nasubiri sasa maajabu ya mechi za hatua ya makundi. Nasubiri kuona uamuzi wa Yanga juu ya nafasi iliyoachwa wazi na George Lwandamina aliyewakimbia.

Ipo haja ya nafasi hiyo kuzibwa tena mapema tu kabla ya mechi za makundi zitakazoanza mapema mwezi ujao. Nasubiri kuona kama Yanga itaendelea kuwaamini Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila. Masikini hachagui sana.

Upande wa pili wa simulizi yangu, kuna kocha mmoja Mwingereza anaitwa Dylan Kerr. Huyu anaifundisha Gor Mahia ya Kenya. Wakati Yanga ikiitoa Welaytta Dicha ya Ethiopia, Kerr na Gor Mahia yake waliiondosha Supersport ya Afrika Kusini.

Ni furaha iliyoje. Gor Mahia imeiondosha Supersport ambayo mwaka jana ilifika hatua ya fainali ya michuano hiyo. Ilifungwa mechi ya mwisho na TP Mazembe iliyoibuka mabingwa. Ni timu ngumu kweli kweli.

Hata hivyo, Gor Mahia ilipambana kiume. Ni ile ile Gor Mahia iliyokuja hapa nchini mwaka jana kucheza Michuano ya SportPesa na kutwaa ubingwa. Ndiyo ile ile iliyocheza na Everton pale Taifa.

Kama ulikuwa hufahamu, Kerr huyu aliyeifikisha hatua ya makundi ndiyo yule aliyekuwa akiifundisha Simba miaka miwili tu iliyopita. Alifukuzwa pale Simba Januari 2016. Alifukuzwa baada ya kufungwa kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar. Aliondoshwa kimizengwe.

Miaka miwili mbele, Kerr ameifikisha Gor Mahia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Simba ilifanya nini baada ya hapo? Hakuna cha maana sana.

Mwaka jana Simba ilishinda taji la FA wakati Kerr aliipa Gor Mahia ubingwa wa Ligi Kuu Kenya. Mwaka huu Simba imechemka kwenye michuano hiyo ya kombe la Shirikisho ambayo Kerr na Gor Mahia yake wamefika hatua ya makundi.

Baada ya Simba kumtimua Kerr imefundishwa na kocha watatu mpaka sasa. Alibaki Jackson Mayanja, akaja Joseph Omog na sasa Pierre Lechantre. Simba imetumia gharama kubwa kuajiri makocha wapya bila sababu ya msingi.

Kerr ni miongoni mwa makocha wachache kutoka Ulaya waliokuwa wakilipwa fedha kidogo hapa nchini. Mshahara wake wakati akiwa Simba haufiki hata nusu ya anayolipwa Lechantre kwa sasa. Kerr alikuwa akilipwa kiduchu.

Tatizo kubwa la Kerr ni moja tu. Anaamini zaidi katika soka la kisasa ambalo Tanzania halipo. Hataki kocha apangiwe kitu. Anataka kocha asimamie kila kitu cha kiufundi. Anapenda wachezaji wake wawe huru. Hapa ndipo aliposhindwana na viongozi wa Simba. Kuna wakati walitaka ampange mchezaji fulani lakini akagoma. Kuna wakati alitaka wachezaji wepewe mapumziko lakini viongozi walitaka wawe kambini.

Mazoezi yake yalikuwa ya kucheza na mpira zaidi. Hakuwa na mazoezi mengi ya kutumia nguvu. Viongozi wa Simba walipenda mazoezi ya nguvu zaidi. Mwisho wa siku wakashindwana na kumtimua. Wakaachana na kocha ambaye sasa amekuwa lulu Afrika Mashariki. Wakati mwingine inabidi kujifunza kuishi na makocha wazuri. Tunafahamu soka lakini mambo ya ufundi tuwaachie makocha wenyewe. Tusipende kuwapangia waliosomea kazi yao, tuwape uhuru.