Sikia ukweli huu unaoshangaza

Monday October 9 2017

 

BARCELONA HISPANIA. SOKA ni mchezo unaopendwa sana duniani una mambo mengi yaliyosimama nyuma ya pazia ambayo mashabiki wengi wa soka wamekuwa hawayafahamu. Haya ni baadhi ya mambo yaliyosimama nyuma ya pazia kwa mastaa wengi wa soka.

XAVI HERNANDEZ

Zipo nyakati ambazo wanasoka wanafanya mambo kinyume na matakwa yao kwa ajili ya kuwaridhisha wazazi wao. Akiwa na umri wa miaka 19, kiungo mahiri wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez nusura amwage wino kuitumikia AC Milan ya Italia. Baba yake alikubali dili hilo lakini mama yake alikataa huku akimwambia baba yake Xavi angemtaliki kama mwanaye angeondoka Barcelona na kuhamia AC Milan. Mama yake Xavi ni shabiki mkubwa wa Barcelona.

CRISTIANO RONALDO

Kwa sasa ni mmoja kati ya wanasoka matajiri zaidi duniani. Ronaldo ndiye mwanasoka analiyelipwa zaidi duniani kwa sasa kutokana na kuwa na mshahara mkubwa katika klabu yake ya Real Madrid, huku akiwa pia na matangazo mengi ya biashara. Hata hivyo, zamani hakuwa hivyo. Akiwa na umri wa miaka 14 Ronaldo alifukuzwa shule baada ya kumrushia kiti mwalimu wake mmoja ambaye alikuwa anakebehi hali ya kifedha ya familia yao.

 ZLATAN IBRAHIMOVIC

Mmoja kati ya washambuliaji mahiri wa kati wa zama hizi. Zlatan ametamba na klabu za Malmo, Ajax, Juventus, Inter Milan, AC Milan, Barcelona, PSG na Manchester United. Hata hivyo, ubabe wake wa soka haukuanza sasa. Alikuwa mtambo wa mabao tangu akiwa mdogo.

 Inadaiwa kuna siku timu yake ya utotoni ilichapwa mabao 4-0 huku Zlatan akiwa benchi. Baadaye aliingia uwanjani na kufunga mabao manane peke yake.

JUAN MATA

Klabu za Ligi Kuu England zimeanzishwa miaka mingi iliyopita. Wachezaji wengi wamehama kutoka katika klabu moja kwenda nyingine.

Inashangaza unaposikia ukweli huu, Juan Mata ndiye mchezaji wa kwanza katika historia kuhama kutoka Chelsea kwenda Manchester United katika dili la Januari 2014 wakati wa utawala wa Kocha David Moyes.

ALEX SONG

Wachezaji wa Afrika wanakulia katika mazingira tofauti na wale wa Ulaya. Haishangazi kuona wachezaji wa Afrika wanageuka kuwa tegemeo kubwa kwa familia zao kuliko wachezaji wa Ulaya. Staa wa kimataifa wa Cameroon, Alex Song ambaye alitamba England na klabu ya Arsenal anatoka katika familia kubwa sana kwao Cameroon. Baba yake alikuwa na wake wengi. Song ana ndugu zake 27. Ana dada 17 na kaka 10.

RYAN GIGGS

Staa wa zamani wa Manchester United, Ryan Giggs ni mmoja kati ya wakali waliofunga mabao 100 na zaidi Ligi Kuu England akiungana na Alan Shearer, Sergio Aguero, Wayne Rooney, Frank Lampard, Michael Owen na wengineo. Hata hivyo, Giggs ana rekodi ya kushangaza kidogo. Katika mabao yote aliyofunga Ligi Kuu England hakuwahi kupiga hat trick. Mabao yake mengi ndani ya mechi moja yalikuwa mawili tu.

STEVEN GERRARD

Wachezaji wengine ni wapinzani haswa. Wachezaji wengine wanajali sana upinzani wao wa jadi dhidi ya timu pinzani. Wote tunajua jinsi kuna upinzani mkubwa kati ya Manchester United na Liverpool. Kiungo wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard anaonekana kuwa mpinzani halisi wa Manchester United. Katika maisha yake ya soka, nahodha huyu wa zamani wa Anfield alibadilishana jezi na mastaa wengi wa timu mbalimbali lakini kamwe hakuwahi kubadilishana jezi na mchezaji yeyote wa Manchester United.

RONALDINHO

Mmoja kati ya mastaa walioacha kumbukumbu katika soka ni nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho Gaucho. Kumbe maajabu yake hayakuanzia akiwa na umri mkubwa. Alianza maajabu tangu akiwa mtoto mdogo kwao Brazil. Inadaiwa kwa mara ya kwanza vyombo vya habari kutambua uwezo wa Ronaldinho ni pale timu yake ya utotoni iliposhinda mabao 23-0. Kikubwa zaidi ni Ronaldinho alivyofunga mabao yote.

MESSI NA RONALDO

Hawa ndio wanasoka wanaosumbua zaidi katika zama hizi. Wamekuwa wakifanana kwa mafanikio mengi ndani na nje ya uwanja. Lakini kuna kitu kimoja huwa wanashangaza zaidi. Tofauti kati ya umri wa Ronaldo na Messi ni siku 869. Ronaldo ni mkubwa kwa umri. Lakini kinachoshangaza zaidi ni tofauti kati ya umri wa mtoto wa kwanza wa Messi, Thiago na umri wa mtoto wa kwanza wa Cristiano, Cristiano Junior ni siku hizo hizo 869.

KOMBE LA DHAHABU

Ligi Kuu England haijawahi kuwa na Kombe la Dhahabu. Ni mara moja tu imewahi kuwa na Kombe la Dhahabu. Ni pale FA ilipoamua kuipa Arsenal kombe hilo la dhahabu baada ya kucheza msimu wote wa 2003/2004 bila ya kufungwa mechi yoyote.

NICOLAS ANELKA

Pesa inaongea zaidi leo katika soka la Ulaya kuliko wakati mwingine wowote ule. Hata hivyo, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alishaionyesha dunia kuhusu ubora wake mkubwa katika kutengeneza pesa miaka mingi iliyopita. Fahamu tu Wenger alitumia Pauni 42 milioni kuwanunua mastaa wake wa zamani, Nicolas Anelka, Marc Overmars, Manu Petit, Thierry Henry, Patrick Vieira, Cesc Fabregas, Robin Van Persie, Emmanuel Adebayor na Samir Nasri. Hata hivyo, kwa maajabu ya Wenger, mastaa hawa wote baadaye aliwauza kwa dau la Pauni 42 milioni.