Sikia hii ya Cheka na Antony Joshua

Muktasari:

  • Nyota ya Joshua maarufu kama AJ ilianza kung’ara baada ya kumpiga mkongwe, Wladimir Klitschko mwaka jana, lakini hiyo sio ishu kabisa.

SIO uchawi, Anthony Joshua acheni aendelee kutesa kwenye masumbwi kwani kila zama na wakati wake. Jamaa yuko vizuri sio masihara ana kila sababu ya kuwa bingwa wa dunia wa uzani wa juu.

Nyota ya Joshua maarufu kama AJ ilianza kung’ara baada ya kumpiga mkongwe, Wladimir Klitschko mwaka jana, lakini hiyo sio ishu kabisa.

Unaambiwa mazoezi yake ni balaa hata wakiungana Francis Cheka, Mada Maugo, Francis Miyeyusho, Ibrahimu Class na mabondia wengine unaowafahamu hapa Bongo hawampati AJ mmoja tu.

MAZOEZI YA

AJ NI HIVI

Si unafahamu kama jamaa juzi kati ameuchukua mkanda wa WBO wa Joseph Parker kule Wales tena kwa ushindi mnono wa pointi 3-0 huku majaji wote wakitoa ushindi katika raundi 11 kwa AJ na raundi moja tu ndiyo aliyoshinda Parker, sasa huo sio uchawi? Iko hivi. AJ buana maisha yake ya ndondi ana wataalamu 23, kila mmoja ana jukumu lake katika kuhakikisha anaongeza mataji ya dunia, hadi sasa anashikilia mataji ya WBA, IBF, WBO na anafukuzia lile la WBC.

AJ ana jopo la wataalamu ambao ni Rob Madden (Kocha wa Timu ya AJ), Will Harvey, Henry Baldwin na David Ghansa (Utawala), Ben Ileyemi (Mlinzi), Sina Ghami (Kocha wa Viungo) na Jamie Reynolds (Kocha Mkuu).

Wengine ni Joe Mitchinson (Kitengo cha Video), Eddie Hearn (Promota), Iwan Llewelyn (Meneja wa Mitandao ya Kijamii), Max McCracken na Tony Sims (Wakufunzi), Rowan Wilkinson na Anthony Leaver (Afisa Habari), Andy Bell (Msimamizi wa Matangazo) na Mark Ellison (Mtaalamu wa Lishe).

Bado kuna kina Freddie Cunningham (Meneja), Mark Seltzer (Sparing Partner) na Jonathan Constant, Kevin Ayodele, James Mulley, Michael Jarman na Leon Skinner ambao ni marafiki zake na mara nyingine wanamsaidia katika ‘sparing’.

WASIKIE WABONGO

“Sina meneja na sitaki kuwa naye maana mameneja wa Bongo wanazingua,” anasema Francis Miyeyusho ambaye ni miongoni mwa mabondia wenye heshima kubwa nchini.

Yeye hana mpango kabisa anakwambia hata kwenye mazoezi yake anasimamiwa na Cosmas Cheka, Muddy Brack na Doi Miyeyesho na ndiyo haohao anafanya nao ‘sparing’, akienda kuzichapa nje ya nchi anaambatana na Anthony Rutha au Emmanuel Mlundwa kazi imekwisha.

Ibrahimu Class kidogo japo hajafikia anga za kina AJ lakini anaye meneja (Victoria Joseph), Joe Enea (Mtaalamu wa mazoezi ya nguvu), Habibu Kinyongoli (Kocha Mkuu), Kelvin Majengo, Kondo Nassoro na Super D (Makocha Wasaidizi), Iddi Mkwela, Dull Mbabe na Cosmas Cheka (Sparing Partners).

Kwa upande wa Mada Maugo anakwambia meneja wake ni Janeth Maugo, ana kocha mmoja tu, Mbaruku Heri na ndiye anayemfanyisha ‘sparing’.

Mkali mwingine wa ndondi hapa Bongo, Bruno Tarimo pamoja na kutwaa ubingwa wa Mabara wa WBA, naye haoni ndani kwenye jopo la AJ. Tarimo maarufu kama vifua viwili yeye kocha wake ni Sharifu Mukhsin na ndiye meneja wake.

Mabondia wanaompa sparing ni Iddi Pialali na Ally Maono, lakini pia amekuwa akinolewa na Anthony Rutha na ndiye aliambatana naye Australia alipotwaa ubingwa wa Mabara wa WBA. Francis Cheka kocha wake mkuu ni Abdallah Salehe ‘Comando’ ndiye kocha wake kwa zaidi ya miaka 10, Sparing Partner wake ni Shaban Kaoneka japo huwa anafanya pia na mabondia wa timu ya taifa na anaye meneja.

MSIKIE KINYOGOLI

“Huo utaratibu wa meneja bondia kuwa na menejimenti yake ni mzuri, ila kwa Watanzania udhaifu wetu hatuna uelewa na utawala, mtu anapokuwa kocha wa bondia basi anataka ammiliki yeye tu,” anasema Habibu Kinyogoli na kuendelea.

“ Ulaya wana uwezo wa kuwalipa, lakini huku kwetu ukitaka mambo hayo utajikuta hupati fedha.”

Kinyogoli anasema ili kubana matumizi mabondia wengi huwafanya wake zao kuwa mameneja, lakini unatakiwa kuwa na mbunifu wa kumuelekeza avae bukta na joho gani, anyoe vipi, apande vipi ulingoni ni vitu kama hivyo, mtaalamu wa lishe lakini tatizo ni fedha.

“Wenzetu Ulaya kama AJ, pambano lake moja tu anailipa ‘crew’ yote hiyo na chenji inabaki ya kutosha tu, sisi bado tuko nyuma kwenye hilo, ndiyo sababu utakuta mabondia wetu wengi hata kuwa na kocha ni shida,” alisema Kingogoli.

Alisema enzi zake alipokuwa akimnoa Bingwa wa Dunia wa WBU, Rashid Matumla alijaribu kutumia mbinu ya AJ kwa kuwakaribisha baadhi ya makocha tofauti ili wamsaidie akafanikiwa.