Sanchez na hukumu ya jezi ya George Best

Muktasari:

  • Kwa nini alazimike kusubiri nje akiwa na jezi namba 12, akisubiri kupata nafasi wakati alikuwa shetani kuliko mashetani wote Old Trafford?

GEORGE Best, aliichezea Manchester United mechi 470. Katika mechi zote hizo zote hakuna aliyoanzia benchi.

Kwa nini alazimike kusubiri nje akiwa na jezi namba 12, akisubiri kupata nafasi wakati alikuwa shetani kuliko mashetani wote Old Trafford?

Moja kati ya mechi hizo 470, ilikuwa ni dhidi ya Sheffield Wednesday.

Mechi hii ilipigwa machi 1969 na alivaa jezi No. 9. Alitumia jezi No. 10, katika michezo 39 na jezi namba 8, katika michezo 43.

Katika michezo 141, alivaa jezi No. 7, ukiwemo ushindi wa kihistoria dhidi ya Benfica, kwenye fainali ya kombe la Bara Ulaya (ligi ya mabingwa), mwaka 1968. Hii ndio sababu mpaka Jezi hii inafahamika kama jezi ya George Best!

Kuanzia hapo, utamaduni wa mastaa kugombania jezi ya George Best ukaanza. Kila staa anayetua ‘Theatre of Dreams’ amekuwa na kiu ya kupewa jezi hii. Kila mtu anataka kuonja joto la Jezi No.7.

Baada ya George Best kufanya yake, wakafuata mastaa kibao waliopewa jezi hii. Bryan Robson, Eric Cantona, David Beckham, Cristiano Ronaldo, Memphis Depay na sasa shetani mpya amepatikana, Alexis Sanchez!

Licha ya jezi hiyo kujulikana kama jezi ya George Best, ieleweke katika mechi zote 470 alizocheza mchawi huyo, aliyetumbukia kwenye ulevi wa pombe hadi umauti unamkuta, alicheza mechi 246 akiwa na Jezi namba 11.

Turudi kwenye hili la jezi aliyokabidhiwa Alexis Sanchez. Steve Coppel anatajwa kama mtu aliyevaa viatu vya Best vikamwenea viruzi, alijiunga na Man United mwaka 1975, akapewa No. 7, akaivaa ikamkaa.

Alichokifanya uwanjani mpaka sasa kinakumbukwa. Akaja Bryan Robson.

Huyu alijiunga na United, akitokea West Bromwich Albion, akapewa jezi namba 11 avae. Hata hivyo katika mchezo wake wa kwanza kukatokea mabadiliko kidogo.

Coppell akiwa ameumia, Robson aliingia kuziba pengo la Coppell, ikabidi avae Jezi yake! Kuanzia hapo jezi hii ikahamia kwa Robson rasmi. Akawa mrithi wa Best.

“Nilipotua pale Old Trafford, nilikabidhiwa jezi namba 11, lakini kutokana na mapenzi yangu na jezi namba saba, niliomba nipewe jezi hiyo.

“Aliyekuwa anaivaa ni Steve Coppell, katika mchezo dhidi ya City, nikatakiwa kujaza pengo lake, nilipomwomba kuvaa jezi, alikubali,” alisema Robson.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 na 90, huku Robson akiwa anaandamwa na majeraha ya kila mara, ilibidi wanaume wengine wakabidhiwe majukumu yake.

Peter Davenport, Russell Beardsmore, Clayton Blackmore, Neil Webb na Andrei Kanchelskis wakapata fursa ya kuonja joto la jezi hii.

Hata hivyo, aliporejea alirudishiwa jezi. Hali hiyo ikaendelea hadi Novemba 1992, pale United ilipopata saini ya Eric Cantona. Kila kitu kikabadilika. Mechi ya kwanza ya Cantona, ilikuwa ni mchezo wa kirafiki dhidi ya Benfica.

Alivaa jezi namba 10. Mechi ya kwanza ya ligi, ilikuwa ni Desemba mwaka huo, alipoingia akitoea benchi dhidi ya Man City. Alipopata nafasi ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza, akimpumzisha Robson.

Msimu wa 1993-94 utaratibu wa kutumia namba kwa ajili ya kupanga kikosi ukaanzishwa.

Ikabidi Cantona akabidhiwe jezi namba saba rasmi huku Robson akichukua namba 12. Cantona akavaa jezi hiyo hadi pale alipostaafu mwishoni mwa msimu wa 1996-97.

Wakati huo wote, David Beckham yeye alikuwa anajivunia kuvaa namba 10.

Hata hivyo, Teddy Sheringham, alipotua Old Trafford akitokea Tottenham Hotspur, alitoa masharti ya kupewa jezi namba 10 aliyoizoea, ikabidi Beckham akubali kuachia jezi yake, shingo upande!

Sio kwamba Beckham hakupenda namba saba, hakujua atakabidhiwa jezi hii baada ya kuvuliwa namba 10.

Ferguson alimpigia simu akiwa mapumziko na kumtaarifu amevuliwa jezi namba 10, lakini hakuambiwa ni kitu gani kinaandaliwa kwa ajili yake.

“Nilifadhaika sana, kila nikifikiria ni kipi nilichofanya kibaya hadi kupokonywa jezi, sikupata jibu, kisha mwezi mmoja baadae, tukiwa mazoezini siku chache kabla ya ligi kuanza, Kocha alikuja akiwa na jezi mpya kwa ajili yangu, ilikuwa ni namba 7, ilikuwa ni Jezi ya George Best na Eric Cantona, sikuamini,” alisema Beckham katika moja ya mahojiano yake na wanahabari.

Mwaka 2003, Beckham aliondoka Old Trafford na kutimkia Real Madrid. Ni mwaka huo huo ndipo, Alex Ferguson alipomsajili kinda wa Sporting

Lisbon, Cristiano Ronaldo. Bila kupepesa akamkabidhi mikoba ya Best, Cantona na Beckham. Jezi namba 7, ikaenda kwa mreno huyo.

Licha ya Cristiano Ronaldo awali kutoridhika na jezi hiyo, historia inamtaja kama mmoja wa wanaume waliovaa viatu vya George Best pale Old Trafford ikamkaa vizuri. Kama kuna kitu kinachohusudiwa na Ronaldo ni ‘No.7’ na hili linathibitishwa na nembo yake ya CR7.

Mbali na Ronaldo, Cantona na Beckham kabla ya Sanchez, kina Michael Owen, Antonio Valencia na Memphis Depay nao walipata fursa ya kuonja

joto la jezi hii inayoheshimika sana pale Old Trafford, lakini kwa bahati mbaya sana wakachemka.

Sasa ni zamu ya Alexis Sanchez. Ni zamu yake kuamua kunyoa au kusuka.

Ni zamu yake kuendeleza heshima ya jezi No 7 pale Old Trafford. Usiku wa Januari 26, Sanchez alikuwa mmoja wa wapiganaji 11 wa Jose Mourinho, katika uwanja wa vumbi wa Huish Park. Ulikuwa ni mchezo wa raundi ya nne, Kombe la FA, dhidi ya vibond Yeovil Town. Akishuhudiwa na mashabiki takribani 9,195 akafanya awezalo kuisaidia Man United kuinyanyasa Yeovil. Haukuwa mwanzo mbaya!

Hii ikawa ni mara ya kwanza jezi hii kutumika tangu ilipovaliwa kwa mara ya mwisho na Memphis Depay. Hata hivyo, tofauti na alivyotarajia hakupata mapokeo mazuri sana kutoka kwa wachezaji wa Yeovil.

Nathan Smith alichakua jukumu la kumkaribisha kwa staili ya mechi za mavumbini. Akamkwatua vibaya sana. Lakini Sanchez hakutaka kuonekana mzembe, aliamka akajikung’uta na kuendelea na mechi.

Kutokana na faulu hiyo, mwamuzi akaizawadi Man United mpira wa adhabu, Sanchez akawa ndio mpigaji lakini shuti lake lililopaa mbali kabisa na lango la Artur Krysiak, lilifanya uwanja mzima ulipuke na zomeazomea wote wakiimba, “What a waste of money.”

Alichokifanya baada ya hapo, hakisimuliki kwa maneno machache.

Alikokota mabeki atakavyo, akipiga vyenga huku akiwakimbiza hadi uwanja mzima ukalipuka na shangwe.

Beki wa Yeovil, Tom James aliomba mechi imalizike kwa jinsi alivyokuwa anakimbizwa.

Akicheza katika winga ya kushoto, sambamba na Juan Mata na Marcus Rashford kuunda utatu mtakatifu, Sanchez alikuwa na kazi ya kuwalisha mipira Mata na Rashford.

Dakika 75 alizokuwa uwanjani zilitosha kuonyesha thamani na kuwafanya mashabiki wa Arsenal kuanza kuzimiss huduma zake. Asisti mbili alizotoa kwa Rashford na Herrera, zilitosha kabisa kuisaidia Man United kuibuka na ushindi wa 4-0 na kusonga mbele.

Kiasi cha Paundi milioni zilizotumika kumng’oa Emirates ni zaidi ya kikosi kizima cha Yeovil, hivyo basi ni mapema kusema Man United wamelamba dume lakini kutokana mwanzo huo, ni dhahiri kuwa Jezi ya George Best imepata mrithi.