Saa 2 matata hotelini na Victor Wanyama

Tuesday June 12 2018

 

By CHARLES ABEL DAR ES SALAAM

ASIKUAMBIE mtu, maisha anayoishia Mkenya, Victor Wanyama nje ya uwanja yanaweza kuwa ya kushangaza pengine tofauti na jinsi watu wanavyomtazama kutokana na umaarufu alionao.

Ndani ya uwanja akiwa na jezi ya klabu yake ya Tottenham Hotspurs inayoshiriki Ligi Kuu ya England sambamba na timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Wanyama anakuwa ni binadamu ambaye hutofurahia kukutana naye kwa shughuli yake pevu.

Lakini sasa, hali ya kushangaza ni kwamba, licha ya kucheza soka la shoka anapokuwa uwanjani, nahodha huyo wa Kenya, amekuwa na mtindo wa tofauti wa maisha binafsi.

Takriban muda wa saa mbili nilipata fursa ya kukaa naye karibu alipokuwepo nchini kwa mapumziko wiki iliyopita. Muda huo ulitosha kupata picha halisi ya upande wa pili wa Wanyama tofauti na anapokuwa uwanjani.

Kwangu nilijiona mtu mwenye bahati kupata nafasi ya kuzungumza na nyota mkubwa kama huyo. Hao wazungu tunawaona kila siku wakigombea kupiga naye picha huko Ulaya pindi anapokuwa uwanjani ndiye itakuwa miye buana!

Ndani ya baa iliyopo levo ya nane ambayo ni ya juu zaidi kwenye Hoteli ya Kifahari ya Hyatt Regency jijini ambayo Wanyama alifikia, huku tukipulizwa na ubaridi ambao kikawaida sio hali ya hewa iliyozoeleka hapa Dar es Salaam, nilifanikiwa kuvuna mawili matatu kutoka kwa kiungo huyo anayehusishwa kuhitajika na Manchester United.

Ndani ya baa hiyo ndipo tulipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Wanyama akiwa sambamba na ndugu zake watatu ambao amekuja nao nchini, huku mimi nikiwa pamoja na wanahabari na wachambuzi wa soka waandamizi, Edo Kumwembe na Shaffih Dauda, ni eneo ambalo linaweza kukusaidia utazame vyema majengo pacha ya

Benki Kuu ya Tanzania ambayo yako jirani na hoteli hiyo upande wa Kaskazini Mashariki huku upande wa Kusini Mashariki kuna Bandari ya Dar es Salaam.

Ukiwa hapo unapata nafasi pia ya kuona Kivuko cha Kigamboni pamoja na Soko la Samaki la Kimataifa la Feri jijini.

Tulilazimika kutangulia kwenye baa hiyo na kupata vinywaji, laini kabla ya Wanyama na nduguze kuja baadaye kwani majira hayo ya saa 3 usiku alikuwa nyumbani kwa mmoja wa rafiki zake wakubwa nchini, Yusuf Bakhresa aliyemualika kwa ajili ya futari.

Ilinishangaza kuona idadi kubwa ya wateja waliokuwa wakipata vinywaji na kula chakula katika baa hiyo wakiwa ni raia wa kigeni, huku ngozi nyeusi tukiwa wachache, pengine ni kutokana na gharama za juu zinazotozwa kwa huduma kwenye hoteli hiyo.

Nakumbuka glasi moja ya juisi niliyoagiza bei yake ni Sh.12,000 ya Kitanzania, wakati kiuhalisia mtaani glasi hiyo unaweza kununua hata kwa Sh 500.

Saa 3.30 usiku, Wanyama aliwasili hotelini hapo akiwa kwenye gari ya kifahari aina ya Brabus na tulilazimika kushuka na lifti kumfuata hadi katika eneo la kupumzikia ambalo liko jirani na mlango wa kuingia ambako alikuwa ameketi pamoja na nduguze.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale ilitupasa kurudi kule baa kutokana na utulivu uliokuwepo na kumpa nafasi Wanyama kuona mandhari ya jiji la Dar es Salaam usiku.

Tukiwa kule baa, baadhi ya raia wa kigeni walishtuka na kumsogelea kwa ukaribu Wanyama huku wakionekana kutoamini macho yao kwa kumuona nyota huyo wa Spurs

na wengine walidiriki hata kuuliza ili kupata uhakika kama ndiye ama siye na walipojiridhisha, wengi wao waliomba kupiga naye picha huku wakimhoji maswali ya hapa na pale.

UCHANGAMFU KINOMA

Imezoeleka hapa nchini kwa mastaa wengi wa aina yake kutopenda usumbufu wa mashabiki au watu kwa kutaka kupiga nao picha, lakini hali ilikuwa tofauti kwa staa huyo wa Afrika, aliyeonyesha kumchangamkia kila mmoja aliyeomba kupiga naye picha pasipo kuonyesha hali yoyote ya kuchukia.

Maongezi mengi ya kiungo huyo na ndugu zake yalihusu ziara yao nchini Tanzania na hakupenda sana kuzungumzia masuala ya ndani ya uwanja.

“Napapenda sana Tanzania hasa Zanzibar kwa sababu kuna utulivu uliopitiliza, lakini pia watu wake ni wakarimu na mazingira yanavutia.

Kesho nitaenda Kenya, lakini nadhani nitarudi wakati wa mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup),” alisema Wanyama.

HANA MAJIVUNO

Kama kuna watu wanafaidi mafanikio ya Wanyama ni ndugu zake ambao amekuwa akiambatana nao kila anapokuja nchini kwa ajili ya mapumziko.

Pamoja na kiungo huyo kulipia gharama za huduma zote pindi wawapo mapumzikoni, anaonyesha anaishi nao kwa upendo kwani kwa muda wote tuliokuwa hapo, sikuona

akimkaripia wala kumtuma yeyote kati yao na alionekana kufurahia zaidi kuwa karibu nao muda wote.

Wanyama alionekana kutupa heshima kubwa wote tuliokuwa kwenye meza ile, kwani katika muda wote ambao tuliketi pale hakufanya mazungumzo yoyote kwa simu hata

alipopigiwa alikuwa akikata na alionyesha ushirikiano wa kuchangia maongezi mbalimbali japo alionekana kutokuwa mzungumzaji sana.

NIDHAMU YA MSOSI

Maisha ya soka la kulipwa sio ya lelemama na pengine ndio maana kundi kubwa la wachezaji wa Kitanzania limeonekana kuogopa kwenda nje ya nchi na hilo nilijifunza kupitia kwa Wanyama.

Moja ya mambo ya msingi ambayo nyota wa kulipwa wamekuwa makini nalo sana ni suala la mlo ambapo mara kwa mara huwa wanaepuka kula au kutumia vyakula vinavyoweza kuathiri afya yake.

Nilijifunza kitu kutoka kwa Wanyama pale tulipolazimika kuagiza chai ili kupasha joto miili kutokana na hali ya baridi ambayo ilizidi kuongezeka kadri saa zilivyozidi kuyoyoma usiku huo.

Wakati sisi wengine tukiagiza ama chai ya kawaida au maziwa, Wanyama yeye aliagiza chai inayotengenezwa na majani ya kijani (Green Tea), lakini aliamua kutumia asali badala ya sukari.

Kitaalamu sukari inatajwa kuchangia ongezeko la uzito kitu ambacho wanasoka wengi wa kulipwa huwa wanakikwepa, kwani husababisha viwango vyao kutetereka.

MAANDALIZI YA MSIMU YAMPASUA KICHWA

Katika idadi kubwa ya mechi za mwishoni, Wanyama hakuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha Spurs na hii ni kutokana na majeraha aliyoyapata na hata alipopona alijikuta akipoteza namba kikosini.

Kiungo huyo mkabaji huyo anakiri kuwa sio kazi nyepesi kwa mchezaji aliyetokea majeruhi ndani ya kikosi cha Spurs kurudisha namba, japo bahati nzuri kwake ni kuwa alipoteza nafasi katika mechi za mwisho za msimu hivyo anaweza kutumia kipindi cha maandalizi ya msimu mpya kurudisha namba yake.

Pia anatufichulia kuwa hilo pia halitokuwa jambo jepesi kutokana na ugumu wa programu ambazo wachezaji hufanyishwa wakati wa maandalizi.

“Hakuna kipindi tunachokuwa tunafanya mazoezi magumu na yanayotesa kama muda wa maandalizi ya msimu. Kiukweli nawazia sana programu hizo kwa sababu ndizo

tunalazimika kutumia nguvu kubwa, lakini baada ya hapo tutakuwa tukifanya programu za kawaida wakati igi itakapokuwa inaendelea,” anasema Wanyama.

BUSH, 50 CENT WAMSHTUA

Miongoni mwa mambo yaliyomsisimua Wanyama ni pale alipoambiwa hotelini hapo ndipo panapopendelewa na watu maarufu duniani pindi wanapokuja nchini.

Miongoni mwa watu waliowahi kufikia kwenye hoteli ya Hyatt Regency ni aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush pamoja na mwanamuziki 50 Cent.

“Sikufahamu kuhusu hilo bwana. Hata hivyo hapa ni pazuri sana kufikia kwa sababu huduma zao ni nzuri,” alisema kiungo huyo.

MASIMULIZI YA BOTI

Moja ya mazungumzo yaliyoonekana kumfurahisha zaidi Wanyama ni yale yaliyokuwa yakihusu usafiri wa majini hasa kutoka Visiwani Zanzibar kuja Dar es Salaam.

Ikumbukwe jana yake asubuhi tu, alitumia usafiri wa boti kutoka Zanzibar kuja Dar lakini hakusita kuelezea hofu yake juu ya usafiri huo.

“Kuna nyakati boti tuliyopanda ilinipa hofu kwa jinsi ilivyokuwa inayumba kutokana na mawimbi. Muda wote nilikuwa nahisi boti itazama.

Hata hivyo nashangaa hivi mnavyoniambia kuwa muda ule ndio mawimbi hayakuwa makubwa. Sasa kama vile tu nilikuwa napata wasiwasi ingekuwa ningesafiri mchana au jioni ambapo mnasema mawimbi huwa makubwa zaidi si ingekuwa hatari,” alihoji huku akicheka kuonyesha alivyosisimka na habari hizo.

Pamoja na yote, Wanyama alionyesha umakini wa hali ya juu katika uzungumzaji na hakuruhusu yeye kuteka mazungumzo.

Alionekana kuwa na nidhamu kubwa ya maisha na haukupenda kujionyesha yeye ni mtu tofauti katika kundi hilo ambalo tulikuwa naye.

Ilipofika saa 6 kasoro usiku tuliagana naye pamoja na ndugu zake kabla ya kuelekea katika vyumba walivyofikia kwenye hoteli hiyo ya kifahari tayari kujiandaa na safari ya kurudi Kenya.