Rekodi ngumu kuzivunja katika soka hizi hapa

Muktasari:

  • Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamefanya mambo ndani ya miaka 10 iliyopita. Hata hivyo, pindi watakapotazama rekodi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Australia, Archie Thompson watagundua rekodi zao bado ni cha mtoto kwa staa huyu.

SOKA ni mchezo wa rekodi. Kuna rekodi nyingi za soka zinawekwa kila siku na kuna rekodi nyingi za soka zinafutwa kila siku. Zifuatazo ni rekodi ambazo itakuwa vigumu kuvunjwa katika zama hizi.

Afunga mabao 13 mechi moja

Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamefanya mambo ndani ya miaka 10 iliyopita. Hata hivyo, pindi watakapotazama rekodi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Australia, Archie Thompson watagundua rekodi zao bado ni cha mtoto kwa staa huyu.

Katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2002 kati ya Australia dhidi ya Visiwa vya Samoa, Archie alifunga mabao 13 peke yake katika ushindi wa mabao 31-0 wa Australia dhidi ya Samoa. Anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya mechi moja mpaka sasa.

Real Madrid

Pengine ndio maana inafahamika kuwa klabu kubwa zaidi Ulaya na duniani kwa jumla. Madrid inashikilia rekodi ya kuchukua mara nyingi zaidi taji la ubingwa wa Ulaya. Mara 11. Kipindi chake bora zaidi katika michuano hiyo kilianzia mwaka 1955 mpaka 1960 ambapo ilitwaa taji hilo mara tano mfululizo.

Wakati huo Madrid ilikuwa na wakali kama kina Alfredo Di Stefano, Francesco Gento, Ferenc Puskas na wengineo. Kwa sasa haitazamiwi kama kuna klabu moja inaweza ikachukua ubingwa wa Ulaya mara tano mfululizo. Klabu nyingine zitakuwa wapi wakati inafanya hayo?

Kadi nyekundu ya haraka

Umewahi kuona au kusikia kadi nyingi nyekundu za mapema lakini hii ilikuwa kiboko yao. Katika pambano kati ya timu ya Cross Farm Park Celtic dhidi ya Taunton East Reach Wanderers beki wa Cross Farm Park Celtic, Lee Todd alipewa kadi nyekundu katika sekunde ya pili tu ya pambano hilo. Todd alikuwa amekerwa na filimbi ya mwamuzi ya kuanzisha mpira akiamini mwamuzi wa pambano hilo alikuwa amepuliza filimbi hiyo kwa nguvu zaidi bila ya sababu za msingi. Alimtukana mwamuzi na hapohapo akapewa kadi nyekundu.

Ilikuwa sekunde ya pili tu tangu mwamuzi aanzishe pambano hilo. Haionekani kama rekodi ya Todd inaweza kuvunjwa katika siku za karibuni.

Hat trick ya haraka zaidi

Sijui alifungaje lakini mchezaji mmoja wa Ligi za Jumapili England anashikilia rekodi ya kufunga hat trick ya haraka zaidi. Alitumia sekunde 70 tu kupiga hat trick hiyo ya mapema.

Katika Ligi Kuu ya England mchezaji anayeshikilia rekodi ya kufunga hat trick ya haraka zaidi ni nyota wa Liverpool, Sadio Mane ambaye akiwa na Southampton alipiga hat trick ya haraka zaidi katika pambano dhidi ya Aston Villa ambapo alitumia dakika 2 na sekunde 56 kufunga. Jaribu kujiuliza staa huyo alitumia kasi gani kufunga hat trick hiyo.

Rogério Ceni

Umeona wapi kipa akawa anashindana na washambuliaji katika kufunga mabao? Huyu hapa Rogerio Ceni kipa wa zamani wa kimataifa wa Brazil amestaafu soka hivi karibuni akiwa na rekodi ya kipekee sana. kipa huyu wa zamani wa timu ya Sao Paulo ya Brazil amefunga mabao 131 katika maisha yake ya soka. Awali mashabiki walimfahamu zaidi kipa wa zamani wa Paraguay, Jose Luis Chilavert kwa kufunga mabao mengi lakini rekodi zinaonyesha Chilavert amezidiwa mabao 64 na Ceni.

Katika kipindi cha miaka 25 alichoichezea Sao Paulo, Ceni alikuwa mtaalamu wa kupiga faulo pamoja na penalti na hivyo kufunga mabao mengi kiasi hicho. Alistaafu soka akiwa ametwaa mataji 20 makubwa na Sao Paulo ikiwemo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Brazil na mawili ya ubingwa wa Amerika Kusini maarufu kama Copa Libertadores.

Brazil

Rekodi hii ni kali na inashikiliwa na Timu ya Taifa ya Brazil. Haijulikani katika siku za usoni lakini mpaka sasa Brazil inashikilia rekodi ya kushiriki katika fainali zote za Kombe la Dunia.

Imeshiriki mara 20 huku ikifukuziwa kwa karibu na Ujerumani na Italia ambazo zimeshiriki mara 18. Bahati mbaya kwa Italia ni mwaka huu pia itakosekana katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia. Brazil pia inashikilia rekodi ya kuchukua taji la Kombe la Dunia mara nyingi zaidi. Imechukua mara tano ingawa inafukuzwa kwa karibu na Ujerumani iliyochukua mara nne. Hata hivyo, Ujerumani inaweza kuifikia Brazil mwaka huu huko Russia.