MAKALA: Okwi anatumika kama hirizi

Muktasari:

NIONAVYO: Kwao Okwi ni zaidi ya ubingwa wa VPL. Hawa ndio mashabiki wa Simba na viongozi wao, hata hili la tuhuma la kutakatisha fedha nalo litapita sababu ya Okwi.

UKITAKA kuwafurahisha mashabiki wa Simba huna haja ya kutumia nguvu kubwa, wewe mtaje Emmanuel Okwi na msifie tu inatosha. Mashabiki wa Simba kwao Emmanuel Okwi ni zaidi ya ubingwa wa VPL.

Hii ndiyo sababu kubwa ya kina Aveva na Kaburu kuendelea kuiongoza Simba hadi sasa bila mabango yanayowataka waondoke pale msimbazi.

Si rahisi kuzuia Presha ya mashabiki wa Simba na Yanga kwa kukosa ubingwa mara tatu tena ukienda kwa mpinzani wako. Yanga inachukua na kuweka ndoo ya VPL mara tatu mfululizo mbele ya Simba na bado kina Aveva wapo tu pale Simba.

Kinachowaweka pale ni Emmanuel Okwi. Kila Msimu unapofikia mwisho na viongozi wa Simba kugundua kuwa hawatachukua ubingwa basi wanawawekea mashabiki wao picha ya Emmanuel Okwi basi na wao wanatulia.

Kwao Okwi ni zaidi ya ubingwa wa VPL. Hawa ndio mashabiki wa Simba na viongozi wao, hata hili la tuhuma la kutakatisha fedha nalo litapita sababu ya Okwi.

Usajili wa Okwi ndani ya Simba si wa kitaalamu sana, Okwi analetwa kuja kutuliza hasira za wanasimba kwa kutokuchukua ubingwa.

Viongozi wa simba wangelifanya nini zaidi kuwazuia mashabiki wao wasianze maneno?

Okwi hakuwahi kuwa mfungaji bora popote pale si hapa nchini wala nchini kwao Uganda. Sifa kuu ya Okwi kwa mashabiki wa Simba ni historia ya kuifunga Yanga.

Okwi huu ni mkataba wake wa tatu kusaini Simba, wa kwanza alisaini 2010 akitokea Sports Club Villa ya nchini kwao Uganda, mwaka 2013 wakamuuza Tunisia kwa timu ya Etoile Du Sahel na alifanikiwa kucheza mechi moja tu ya ushindani.

Etoile baada ya kushindwana naye alirudi nchini kwao na akaombewa kucheza Villa hadi msimu wa 2013/2014 alipojiunga Yanga.

 Mara ya Pili Okwi kurudishwa Simba kuja kutibu majeraha ya mashabiki wa Simba kwa kutokuchukua Ubingwa ilikuwa ni msimu wa 2014/2015.

Baada ya kufanikiwa kuwatuliza mashabiki viongozi wa Simba walimuuza SønderjyskE ya Denmark kwa mkataba wa miaka mitano.

Huku alicheza dakika 317 tu ambapo alifanikiwa kucheza michezo Sita.

Baada ya SønderjyskE kuona hana msaada kwa timu yao waliamua kuvunja naye mkataba. Okwi kama kawaida akarudi Villa kuja kutega kina Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Evance Aveva wana soo gani bahati nzuri wakapata balaa la kutokuchukua VPL.

 Okwi akajua lazima wampigie Simu ili akawatulize mashabiki wa Simba pale Msimbazi.

Kweli Idd Mosi akaonekana Dewji akiwaambia wanasimba kuwa amewaletea Zawaidi ya Idd huku pembeni Okwi akiwa anacheka na Kiduku chake.

 Baada ya ile video kusambaa swala la Niyonzima kusajiliwa Simba likaisha, magazeti yote na mashabiki wa Simba wakashangilia Okwi kurudi.

Hapa kaja kutibu tena majeraha ya kutokuchukua Ubingwa. Simba hawajawahi hata Siku moja kujiuliza kwa nini wenzetu huwa wanavunja naye mkataba... hili kwao si kitu ilimradi aliwahi kuifunga Yanga inatosha.

Mwacheni aje kupiga Stori na Mayanja kuhusu Villa na Uganda Cranes si wote wamechezea timu hizi?

Wana mengi ya kuongea nje ya uwanja kuliko ndani ya Uwanja. Hapa ndipo unapoweza kupima kiwango cha akili cha mashabiki wa Simba.

Wanashindwa kuelewa wanataka nini haswa Ubingwa au Okwi mwenye bahati ya kuifunga Yanga?
  Kwa upande wa pili viongozi wa Simba hawajui nini wanafanya hata kama walikuwa wanataka kumsajili Niyonzima kweli walikosa fedha za kumbakisha Ajib?

Hivi ni kweli hawajui Ajibu ana uwezo wa kupiga mipira iliyokufa zaidi ya Niyonzima? Hapa tofauti inajitokeza kuwa Simba wamesajili chenga za Niyonzima wakaacha kusajili magoli ya Ajibu kwa hili wamekosea watakuja kugundua kwenye ligi.

 Simba wangepaswa kufanya fitna zote wapate mtu kama Msuva au Mbaraka Yusuph kuliko Okwi. Sioni Simba ikichukua Ubingwa mbele ya Ngoma, Ajib, Tambwe, Kamusoko, Chirwa na Msuva.

Sioni Boko, Mavugo, Kichuya, Niyonzima na Okwi kama watafikisha idadi ya magoli ya Yanga msimu ujao. Yote kwa Yote mashabiki wanauziwa jezi ya Okwi kwa sasa pale Kariakoo wanataka nini zaidi? Hii ndio Hirizi yao ‘this is Simba Buana’.

Niamini mimi kama Simba ingefanikiwa kuchukua Ubingwa wa 2016/2017 wasingemsajili Okwi kabisa. Wasingemsajili kwa kuwa hana kiwango na hakidhi matakwa ya kitaalamu ya timu inayotaka kwenda kucheza michezo ya kimataifa, amekuja tu kama hirizi ya kuwafunga mashabiki midomo.

0712 702 602