Okwi aingia anga za mastaa VPL,Bocco Kashtuka

Sunday April 15 2018

 

SHOO za kibabe za Emmanuel Okwi sasa zimemuweka karibu na wababe wenzake ndani ya Ligi Kuu Bara (VPL) inayodhaminiwa na Vodacom. Watoto wote tupa kule, yaani ubabe mwanzo mwisho.

Okwi sasa unaambiwa ameingia kwenye orodha ya mastaa wa Ligi Kuu Bara ambao wameweza kufunga mabao 18 ama zaidi. Alitimiza idadi hiyo ya mabao Alhamisi iliyopita alipoifunga Simba bao moja kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Mbeya City.

Kwenye orodha hiyo huwezi kukuta ‘watoto’ wadogo kama kina Ibrahim Ajib, Mbraka Yusuf ama Juma Liuzio. Mchezaji ambaye anacheza vizuri mechi moja na kuharibu kwenye mechi tatu zinazofuata. Mchezaji ambaye anacheza vizuri pale anapojisikia.

Asikwambie mtu, kufunga mabao 18 Ligi Kuu siyo jambo la mchezo mchezo ati. Okwi mpaka sasa amefunga idadi hiyo ya mabao na ana mechi sita za Ligi mbele yake. Kwanini asiivuke idadi hiyo wakati hapo mbele kuna timu kama Majimaji bado hawajacheza nazo?

Hata hivyo imemchukua Okwi zaidi ya miaka minane Ligi Kuu kufikisha idadi hiyo ya mabao. Mara nyingi alikuwa akiishia mabao 10 ama 12 tu. Kufunga mabao 18 siyo mchezo kabisa.

Hebu fikiria wachezaji hatari kama Mrisho Ngassa, Saimon Msuva, Jerry Tegete na wengineo hawakuweza kufikisha idadi hiyo. Yaani hata yule Kipre Tchetche ambaye ambaye alitamba pale Azam na kula fedha nyingi tu za Bakhresa hakuwahi kufikisha idadi hiyo.

Hakuna ubishi kwamba kwa mabao 18 aliyofunga mpaka sasa na kuongoza kwenye chati ya wafungaji wa VPL, Okwi ameingia katika orodha ya wababe wa Ligi Kuu. Hata akiondoka nchini tena hatakuwa na deni.

Unawafahamu mastaa wengine waliowahi kufunga mabao 18 ama zaidi Ligi Kuu kwa miaka ya karibuni? Mwanaspoti inaangazia wachezaji walioweza kufikisha idadi hiyo katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Mohammed Hussein- Mabao 26

Huyu ndiye mwenye Ligi Kuu yake. Jina lake maarufu zaidi ni Mmachinga na aliupiga mpira wa maana pale Yanga miaka hiyo wakati Rais wa Tanzania akiwa Ally Hassan Mwinyi na kisha Benjamin Mkapa.

Sasa pata picha enzi hizo, Mmachinga alicheza sambamba na Edibily Lunyamila na Sekilojo Chambua. Walikuwa ni hatari hawa jamaa. Akikukosa mmoja lazima mwingine akumalize. Inadaiwa kuwa utatu wao ndio uliowahi kufunga mabao zaidi Ligi Kuu.

Sasa mwaka 1998 Mmachinga aliweka rekodi ya maana ya kufunga mabao 26 Ligi Kuu, idadi ambayo mpaka leo imemfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa ligi. Miaka 20 sasa rekodi hiyo imedumu na huenda ikadumu zaidi na zaidi. Nani ataivunja?

Abdallah Juma- Mabao 25

Mshambuliaji wa maana zaidi kuwahi kuichezea Mtibwa Sugar ni Abdallah Juma. Yapo maneno mengi mabaya yanasemwa juu yake lakini ukweli ni kwamba jamaa ana rekodi yake ya kufunga mabao 25 Ligi Kuu.

Rekodi hii aliiweka 2006. Unaambiwa kila Mtibwa Sugar iliposhinda kule kwao Manungu-Turiani, Morogoro, taarifa zilieleza kuwa mabao yalifungwa na Juma. Yaani kila Mtibwa ikishinda ilikuwa ni kazi ya staa huyo.

Bahati mbaya ni kwamba hakuweza kufunga tena hata mabao 15 Ligi Kuu baada ya hapo. Inastaajabisha sana.

Amissi Tambwe-Mabao 21

Straika mziviaji ziadi kuwahi kucheza Ligi Kuu, Amissi Tambwe naye akirejea kwao Burundi hatakuwa na deni kwani mpaka sasa ameacha rekodi nyingi tu za maana hapa Bongo. Ana rekodi ya kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja ‘Hat Trick’ za kutosha. Amekuwa mfungaji bora wa Ligi mara mbili.

Rekodi ya kibabe zaidi ya Tambwe ilikuwa kufunga mabao 21 msimu wa 2015/16. Mabao yake hayo yaliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu tena kwa kishindo.

Bahati mbaya kwa Tambwe ni majeraha sugu aliyopata msimu huu ambayo bila shaka yatahitimisha maisha yake pale Yanga. uwezekano wa Yanga kuendelea naye kwa msimu ujao ni mdogo kama vile Majimaji kutwaa ubingwa wa Ligi kuu.

Hamis Kiiza-Mabao 19

Baada ya kucheza Yanga kwa miaka miwili, Kiiza alirejea kwao Uganda na kisha kujiunga na Simba mwaka 2015. Alipokuwa Yanga hakuwa tishio sana, lakini alipokwenda Simba mambo yakawa tofauti.

Kiiza alikuwa akifunga karibu kila wikiendi. Alikimbizana na Tambwe kwenye chati ya wafungaji kila siku. Hakuwa mtu wa mchezo mchezo. Hadi msimu unamalizika alikuwa amefunga mabao 19, akizidiwa mawili tu na Tambwe aliyeibuka mfungaji bora.

Tena huenda angemaliza na mabao zaidi msimu huo lakini baadaye alifanya mgomo baridi kushinikiza malipo ya mishahara yake jambo ambalo lilimfanya akose mechi kadhaa za mwisho wa msimu.

John Bocco-Mabao 19

Staa wa Simba, John Bocco naye pamoja na kucheza Ligi Kuu kwa miaka 10 sasa, amewahi kuvuka idadi ya mabao 18 mara moja tu. Ndiyo maana unaambiwa kufunga idadi hiyo ya mabao siyo jambo jepesi hata kidogo. Ni lazima uwe mbabe.

Bocco ambaye alidumu Azam kwa miaka tisa kabla ya kujiunga na Simba mwaka jana, aliweka rekodi hiyo msimu wa 2011/12. Msimu huo Bocco aliifungia Azam mabao 19 na kuibuka mfungaji bora.

Mbali na mabao hayo, takwimu zinaonyesha kuwa Bocco ndio straika hatari zaidi kuwahi kutokea Ligi Kuu ambapo mpaka sasa amefunga mabao 97. Amefunga pia mabao karibu 50 kwenye mashindano mengine aliyoshiriki.

Amissi Tambwe-Mabao 19

Straika huyu Mrundi hakuja nchini kuuza sura. Anastahili kabisa kuwa shemeji wa Tanzania baada ya kuoa mtoto mmoja matata wa Kibongo. Kazi aliyofanya kwenye soka hapa nchini siyo ya kitoto.

Msimu wake wa kwanza tu alikuwa pale Simba na akafunga mabao 19. Inafurahisha sana. Pamoja na ugeni wa Ligi. Pamoja na kiwango kibovu cha Simba iliyomaliza kwenye nafasi ya nne msimu huo, Tambwe alifunga mabao 19. Achene utani, kama ni kufunga jamaa anajua.

Baadaye Simba ilimzingua akaamua kujiunga na Yanga ambayo tayari imempa mataji matatu ya Ligi Kuu, moja la FA, moja la Ngao ya Hisani na pia amepata fursa ya kucheza hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

Boniface Ambani- Mabao 19

Hapa nchini kuna mastraika wawili kutoka Kenya waliowahi kutikisa. Kuna Boniface Ambani na Ben Mwalala. Achana kwanza na Mwalala ambaye alikuwa na nyota ya kupendwa pale Jangwani.

Ambani alikuwa hatari zaidi kwenye kufunga. Msimu wa 2008/09 alifanya kazi ya maana ya kupeleka taji pale Yanga akifunga mabao 19 yaliyomfanya pia kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu.

Yanga ya msimu huo ilikuwa hatari ambapo Ambani alicheza sambamba na Mwalala na Mrisho Ngassa. Tegete alikuwa akipewa dakika chache chache kumalizia kazi iliyofanywa na wababe hao.

Mussa Mgosi-Mabao 18

Mgosi naye amestaafu soka na rekodi ya maana. Alifunga mabao 18 msimu wa 2009/10 ambao timu yake ya Simba ilitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Msimu huo Mgosi alikuwa moto wa kuotea mbali. Alikuwa na kasi, uwezo wa kupiga chenga, mashuti na kufunga. Mabeki wa timu pinzani walipata wakati mgumu sana kumzuia asifunge. Yanga wenyewe wanamkumbuka kwani aliwafunga mabao matatu msimu huo.

Tangu kuondoka kwa Mgosi, ni Tambwe ndiye aliyeweza kufunga idadi kubwa zaidi yake pale Simba. Wengine wote walichemka. Okwi anamaliza shughuli kwa sasa kwani anaweza kuvunja rekodi zote za watangulizi wake hao.