Ngassa asema uchawi hauna maana yoyote kwenye soka

Muktasari:

Anasema kipindi anajiunga kwa Wekundu hao mwaka 1991 hata hivyo, mambo yake hayakwenda vizuri kwani hakuweza kupata namba ya kudumu.

Mkali huyo wa Soka, nyota yake ilizidi kung’ara kwani baada ya Ligi ya Muungano kumalizika hakukaa muda mrefu Pamba na badala yake alitimkia Simba.

Anasema kipindi anajiunga kwa Wekundu hao mwaka 1991 hata hivyo, mambo yake hayakwenda vizuri kwani hakuweza kupata namba ya kudumu.

“Kiwango changu kilishuka mno, nikawa sipati namba au muda mwingine nikiingia natolewa mapema, kwahiyo sikupata raha kabisa kwenye ile timu na tatizo ilikuwa ni ugeni,”anasema.

Anaeleza licha ya kujitahidi kuzoea maisha mapya kwenye Klabu ya Simba, lakini bado benchi la ufundi halikumuamini zaidi kumpanga kikosini.

“Wakati naendelea pale Simba, lakini Pamba walizidi kunifuata ili nirudi, kwahiyo nikaangalia maisha yangu ya Msimbazi na majukumu ya kifamilia nikaamua nirudi Pamba ili niwe karibu na familia yangu,”anasema Ngassa.

Anasema hata alirudi Pamba hakuweza kukaa zaidi na kuamua kustaafu kutokana na majukumu ya kifamilia na aliona mpira unaweza kumsahaulisha watoto wake.

Mafanikio

Anasema mafanikio yake kwenye soka ni kuitumikia timu ya taifa kwa muda mrefu kuanzia 1984-89 mfululizo na kujulikana kwa wadau nchini.

Anasema a alianza kuona mafanikio kipindi akiwa Coop United na miaka hiyo wananchi ndio walikuwa wakipendekeza majina ya wachezaji wanaostahili kucheza timu ya taifa.

“Nilijiona mwenye bahati nilipokuta majina yangu kwenye Gazeti la Mfanyakazi kuwa miongoni mwa wachezaji wa Timu ya Taifa Taifa Stars mwaka 1982-83 nikiwa Coop United.

“Kipindi hicho wananchi ndio walikuwa wanapendekeza majina ya wachezaji, nikiwa nimetulia sehemu napitia Gazeti la Mfanyakazi nikakuta jina langu na hapo ndio tulikuwa kwenye Mashindano ya Taifa Cup nikiwa Coop United, nilifurahi sana,” anasema mkongwe huyo.

Ngassa anaongeza licha ya kipindi chote hicho kukipiga kwenye timu hiyo, lakini maslahi yalikuwa kidogo ukilinganisha na hali ya sasa kwa wachezaji wanavyovuta mpunga wa maana.

Ushirikina kwenye soka

Baba huyu mzazi wa Straika wa Ndanda, Mrisho Ngassa anasema ushirikina kwenye soka ni mkubwa na anathibitisha wazi kuhusishwa katika kamati za ufundi. Anasimulia kwanza alianza kupewa madawa akiwa timu moja (haitaji jina) wakati wa mashindano ya klabu bingwa alipopewa ‘mzigo’ ili autupe kwenye mfereji wa maji yanayotiririka kisha anawe miguu na macho na aongee maneno fulani ili kukamilisha masharti ili washinde.

“Siku hiyo tulikuwa tunatarajia kucheza na Mukula FC ya Rwanda mwaka 1988, nikapewa dawa, huku nikiambiwa kuwa nyota yangu ndio imeng’aa, hivyo niende kufanya mambo.”

Anaeleza kwamba alipomaliza kutekeleza alivyoelekezwa,siku ya mechi alicheza ovyo, hadi mashabiki wakamchukia na kulitaka benchi la ufundi limtoe uwanjani na hapo kocha alikuwa, Muksin Amir akisaidiwa na James Bukumbi.

“Katika mchezo huo wa awali tukiwa nyumbani tulitoka suluhu ya bila kufungana, lakini tulipoenda kwao Burundi tukashinda mabao 2-0, mabao yakifungwa na Nteze John na Kitwana Seleman,”anasema.

Anasema siku hiyo anapewa madawa ili timu ilishinde alijikuta akipoteza uaminifu na kuahidi kutorudia tena kushiriki mambo ya kishirikina.

Anaeleza pia hadi sasa wapo wachezaji ambao hutumiwa na klabu zao kishirikina, licha ya kwamba wao wanakuwa hawataki, lakini kutokana kupenda namba wanaamua kutumika hivyo.

Azimia Uwanjani

Mkali huyu wa zamani, anasema katika maisha yake hawezi kusahau tukio lililompata mwaka 1985-6 akiwa na timu ya Pamba alipogongwa kichwa na mchezaji wa Majimaji, Mwafongo na kuzimia kwa dakika kadhaa.

Anasema enzi hizo alikuwa msumbufu sana kwa mabeki wa timu pinzani, hivyo wakati akijaribu kupokea pasi kwa kichwa ili amponyoke beki huyo, alikutana na kichwa ambacho kilimtoa uwanjani kwa muda.

“Yule jamaa namkumbuka hadi leo, alinipiga kichwa nikazimia kwa muda wakati wa mchezo wetu, ilikuwa nipokee pasi kwa kichwa ili nimpite, lakini mshikaji alinigonga vibaya mno nikazimia kwa muda,” anasema nyota huyo.

Anasema katika matukio mengi ya kustaajabisha ambayo hawezi kuyasahau ni kukosa ubingwa katika hali ya kutatanisha, ikiwamo mechi yao ya Pamba na Pan African mwaka 1984.

Katika mchezo huo dhidi ya Pan ambayo ilikuwa hatarini kushuka daraja. Pamba ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0 hadi mapumziko na kujihakikishia ubingwa lakini kipindi cha pili mambo yakabadilika na kuukosa ubingwa huo.

Anakumbuka kuwa wakati wa michuano ya Kombe la Muungano wakiwa na Malindi na tayari wameshajihakikishia ubingwa, ghafla mchezaji Abdul Malaika aliwafunga na kuwakatisha ndoto za taji hilo.

“Hapo tulikuwa na ahadi kibao kwamba tukishinda tunapewa fungu nono na baadhi ya wadau wa soka, lakini dakika za mwisho tukautema ubingwa kwa kuruhusu bao 1-0,” anasema.

Awakumbuka nyota wakali

Anasema a licha ya zamani kuwapo kwa mastaa wakali, lakini kwake Mtemi Ramadhan, Daud Salum, Fred Felix Minziro na Ramadhani Lenny (Simba) na Octavian Mrope, Salim Omary wa Coastal Union walikuwa hatari. Wengine ni Yusuph Banda (Yanga), Adolph Kondo na Charles Mgodo (CDA) na Frank Kasanga Bwalya wa Red Star ambao walikuwa wakimbamba nyota huyo.

Neno kwa wachezaji na TFF

Ngassa anaanza kwa kusema kuwa hadi sasa bado hajavutiwa na kiwango cha wachezaji kwa msimu huu, kwani wote wamekuwa hawana mwendelezo mzuri kwenye ligi.

Mchezaji huyo ambaye aliwahi kuinoa Toto Africans anashauri kuwa wachezaji wa sasa lazima wajitambue na kuthamini kazi yao hiyo, huku wakitumia vyema kipato wanachokipata.

Anasema wanapaswa kujituma na kutobweteka na sifa na kutamani mafanikio ya haraka, badala yake wapambane kuhakikisha wanafika mbali kama wale wa mataifa mengine.

“Lazima wajitambue na kuheshimu kipato wanachokipata katika matumizi sahihi, wasipende mafanikio ya haraka wala kulewa sifa, wapambane kufika mbali,”anasema Ngassa.

Anashauri pia Shirikisho la Soka (TFF), kutoa adhabu kali kwa klabu ambazo zitaonekana kuendekeza aina yoyote ya ushirikina kwenye michezo.

Anaeleza ushirikina hauna faida yoyote kwenye uhai wa soka hasa hili la kisasa na badala yake mazoezi na maandalizi mazuri ndio silaha ya kuliendeleza soka kwa maendeleo.