Ndiwa na Sawe waipatia Kenya medali mbili za dhahabu

Nairobi, Kenya. Bendera ya taifa la Kenya imeendelea kupeperushwa katika uwanja wa Stephen Keshi, huko Assaba Nigeria, yanakofanyika mashindano ya Afrika, baada ya Mwanariadha, Stacy Ndiwa (mita 10,000) na bingwa wa Afrika kuruka juu (high jump), Mathew Sawe, kuongeza medali mbili za dhahabu katika kapu la dhahabu la Kenya.

Wawili hao waliifanya Kenya kufikisha medali ya tano ya dhahabu hapo jana, ambapo Ndiwa alimuongoza mwanariadha mwenzake Alice Aprot kushinda nafasi mbili za mwanzo, mbio za mita 10,000. Ndiwa alitumia muda wa dakika 31: 31.17 kuvuka utepe huku Aprot yeye akitumia dakika 31:36.12 kumaliza mbele ya Muethiopia, Gete Alemayehu ( 32:10.68), aliyemaliza wa tatu.

Wakizungumzia ushindi wao huo, Ndiwa aliyechukua fedha miaka miwili iliyopita na Aprot ambaye alishinda wakati huo walisema: "Tuliamua kushirikiana, tukikimbia kama timu bila kujali nani atashinda lengo letu kubwa likiwa ni kuipa Kenya dhahabu ya tano, hatukuwa wabinafsi, maana tulijua adui yetu ni Ethiopia hivyo tuliamua kummaliza kwanza."

Awali, katika siku ya tatu ya makala haya, bingwa wa Afrika, Mathew Sawe, alithibitisha kuwa ndiye mfalme wa kuruka juu (high jump), barani Afrika baada ya kuipatia Kenya dhahabu ya Nne, katika makala haya 21 ya mashindano ya ubingwa wa Afrika, yanayoingia siku ya mwisho leo huko Assaba Nigeria.

 

Mkenya huyo, anayenolewa na Mfaransa Moussa Fall, aliruka urefu wa mita 2.30, sawa na rekodi take ya taifa na kuipa Kenya sababu ya kuendelea kucheka huko Nigeria na kupata nafasi ya kuwakilisha taifa katika mashindano ya Birmingham Diamond League na Zurich Diamond League, yatakayofanyika Agosti 18 na 30 mtawalia.

Sawe, 30, ambaye aliwapiku Waafrika kusini, Chris Moleya (mita 2.26) na Mpho Linksm (mita 2:15), alipohojiwa na wanahabari baada ya ushindi wake alisema: “Nimefurahishwa sana na ushindi. Hii inanipa motisha ya kufanya vizuri huko Birmingham na Zurich, Waafrika kusini walikuwa moto wa kuota lakini mwisho, dhahabu yetu iko salama."