Nakwambia watatoana jasho kusaka tuzo Russia 2018

MOSCOW, RUSSIA. ARJEN Robben na Alexis Sanchez na Arturo Vidal hawatakuwapo. Lakini kwa mashabiki wa Kombe la Dunia 2018 nchini Russia mwakani ni kicheko tu, kwa sababu hawajapoteza nafasi kubwa ya kuwashuhudia mastaa wanaowakubali kwenye soka.

Si unajua upinzani wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo au ule wa Neymar na Eden Hazard, basi wakali wote hao watakuwepo Russia.

Mastaa hawa watanogesha fainali hizo wakiwania tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo.

Lionel Messi – Argentina

Wengi walikuwa na mashaka makubwa Argentina isingetoboa kupata nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2018. Hata hivyo, supastaa wao, Lionel Messi alionyesha dhahiri kwa nini alistahili kuvikwa kitambaa cha unahodha wa timu hiyo baada ya kufunga mara tatu pekee yake dhidi ya Ecuador kwenye ushindi wa 3-1, hivyo Argentina kufuzu na kumfanya Messi kuwamo kwenye orodha hiyo.

Neymar – Brazil

Neymar alikuwa mtu muhimu katika kikosi cha Tite kilichofuzu kucheza fainali hizo mapema kabisa.

Ndiye aliyekuwa kinara wa mabao katika mechi za kufuzu baada ya kufunga mara sita katika mechi 13, hivyo Brazil inakwenda Russia ikiwa na matarajio makubwa kutoka kwake.

Eden Hazard – Ubelgiji

Amekuwa akilinganishwa kiwango na mastaa kama Messi na Ronaldo, hivyo fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakuwa nafasi pekee kwa staa huyo wa Chelsea kuuthibitishia ulimwengu hata yeye ni moto unaotisha na mbele ya wababe wenzake kuonyesha ndiye staa mwingine mpya anayekuja kufunika zama za wakali waliozoeleka.

Cristiano Ronaldo – Ureno

Alikuwamo katika mchezo Ureno ilipotoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uswisi Jumanne iliyopita na kufuzu kwa fainali hizo za Russia.

Hivyo, Ronaldo atakuwepo katika fainali hizo kuonyesha ubabe wake na mpinzani wake Messi kuwania tuzo ya mchezaji botra wa michuano hiyo.

Robert Lewandowski – Poland

Amecheza mechi 10 za kufuzu Kombe la Dunia na kufunga mabao 16 na kuweka rekodi ya aina yake.

Alifunga mabao 30 kwenye Bundesliga msimu uliopita akiwa na kikosi cha Bayern Munich na msimu huu ameshafunga mara nane katika mechi saba. Ubora wake umemfanya kuwa mtu muhimu kwa Poland na mashabiki wake wanamsubiri kwa hamu Russia hapo mwakani.

Paul Pogba – Ufaransa

Majeraha yamemweka nje katika kikosi cha Manchester United lakini hakuna mashaka kiungo ghali duniani, Paul Pogba atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia.

Ufaransa haikuwa na mushkeli sana katika harakati zake za kufuzu kwa michuano hiyo, hivyo mashabiki wa timu hiyo hasa wale wa supastaa Pogba watamsubiri kwa hamu kuona kitu gani atakakifanya kwenye michuano hiyo mikubwa duniani.

Harry Kane – England

Straika huyo wa Tottenham Hotspur, Harry Kane alifunga bao matata kabisa lililowafanya England kujihakikishia tiketi yao ya kufuzu kwenye fainali hizo za mwakani.

Kitu kizuri, wakati anafanya hivyo, amekuwa na mchango mkubwa sana katika kuhakikisha England inafuzu na alifunga mabao matano katika mechi sita alizoanzishwa.

Mashabiki wa England wanakwenda Russia wakiwa na imani na straika wao kufanya mambo makubwa kwenye michuano hiyo.

Nemanja Matic – Serbia

Kiungo huyu alionekana akitokwa machozi wakati taifa lake la Serbia lilipopata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Georgio Jumatatu iliyopita.

Ushindi huo uliwafanya waongoze Kundi D na hivyo kufuzu kucheza fainali hizo.

Akiwa kwenye ubora mkubwa kabisa kwa sasa, mashabiki wa Serbia wanaamini atakwenda kuwa silaha yao muhimu katika michuano hiyo na hakika hakitakuwa kitu cha kushangaza kuona kama ataonyesha kiwango bora kabisa kwenye fainali hizo.

Alvaro Morata – Hispania

Hakika ndiye silaha ya Hispania kwa sasa na wanaamini kabisa kama watakwenda kutamba kwenye fainali hizo huko Russia, basi staa huyo atakuwa amehusika kwa mchango mkubwa kweli kweli.

Morata alifunga mabao matano katika mechi alizochezea Hispania kuwania kufuzu kwenye fainali hizo za mwakani.

Yapo yale mawili aliyofunga kwenye ushindi wa La Roja wa mabao 8-0 dhidi ya Liechtenstein mwezi uliopita. Anatazamiwa kwenda kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Antoine Griezmann – Ufaransa

Kwenye Euro 2016, alicheza soka la kiwango bora kabisa kuisaidia Ufaransa kufika fainali ambapo ilifungwa na Ureno.

Wakati ikielekea kwenye fainaliza Kombe la Dunia 2018, aliendelea kuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Ufaransa akifunga mabao manne na kuasisti mengine manne katika mechi 10 alizochezea kikosi hicho cha Les Bleus na hivyo matarajio ni makubwa kwa staa huyo kwenda kung’ara kwenye ardhi ya Russia na anatajwa anaweza kuwa mmoja wa wakali watakaokwenda kuwania tuzo ya ubora ya fainali hizo za dunia.

Romelu Lukaku – Ubelgiji

Straika huyu wa Manchester United, amethibitisha yeye ni hatari zaidi anapokuwa mbele ya goli na hilo ndilo linalompa nafasi ya kwenda kutamba Kombe la Dunia 2018 huko Russia.

Ameonyesha umahiri wake wa kufunga mabao kwa misimu yote mitano aliyokuwa Ligi Kuu England na sasa amefunga mabao saba katika mechi saba alizoichezea Man United msimu huu, huku akitazamiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Ubelgiji katika fainali za huko Russia, ambapo katika mechi nane za kufuzu fainali hizo, alifunga mabao 11.