NJE YA BOKSI: Nani kasema soka dakika 90?

Tuesday September 12 2017Peter Kisaranga

Peter Kisaranga 

By Peter Kisaranga

UMEWAHI kupitiwa na usingizi na hatimaye kukosa pambano la soka kati ya timu unazoshabikia?

Au mara nyingine unaweza kuwa safarini ama mahali usipoweza kufuatilia pambano kabisa, njia ambayo imezoeleka siku za karibuni ni pamoja na kufuatilia mechi kwenye intaneti ama programu-tumizi kama livescore n.k.

Kuna wakati kutokana na sababu mbalimbali mchuano unaweza kuahirishwa na hivyo basi ukalazimika kungoja kwa kipindi cha siku kadhaa kabla ya mechi hiyo kuchezwa tena.

Mastori bwana yanaeleza pambano la Ligi Kuu Denmark msimu wa mwaka 1995/96 kati Ab Aalborg na Brondby FC lililochezwa Septemba Mosi 1995.

Ikiwa mchezo umefika dakika 73 na sekunde 53 Brondby ikiongoza mabao 2-0 mashabiki wa timu hiyo ya Brondby waliwasha miale ya moto na kuitupa uwanjani, hivyo kusababisha refa wa mchezo huo aliyefahamika kwa jina la Knudfisker kusimamisha pambano.

Miale ya moto kwa miaka hiyo haikuwa kitu kinachokatazwa kwa mashabiki, hivyo refa alikosa sababu ya kuwanyima ushindi Brondby na pia Aalborg walikuwa wakidai muda wao pia.

Pambano hilo lilikosa tarehe ya kurudiwa, ila kwa bahati nzuri timu hizo zilikutana kwenye michezo ya ndani ya Danish Cup Aprili 1996. Iliamuliwa baada ya mechi hiyo, timu hizo zimalizie dakika 16 na sekunde 7 za mchezo wa wa ligi uliovunjwa.

Brondby ilishinda kwa jumla ya mabao 3-0 (ukijumlisha na matokeo ya awali). Kuanzia kipyenga cha kuanza mchezo Septemba Mosi 1995 mpaka kipyenga cha kutamatisha mchezo Aprili 6, 1996 (tena kwa refa tofauti).

Pambano hilo linahesabika kutumia miezi 6 na siku 5, sasa hapo utasemaje kuwa soka dakika 90 bwana!

Tukirudi hapa nyumbani Simba ikishiriki Kombe la Washindi mwaka 2001 dhidi ya Ismailia ilijikuta ikilala doro baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao mawili.

Ulikuwa ni mchezo wa marudiano baada ya ule wa Misri ambapo Simba ililala mabao 2-0. Hivyo timu hiyo ya Tanzania ilitaka ushindi wa mabao 2-0 ili kufuzu kwa hatua inayofuata.

Basi mchezo ulianza katika Uwanja wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa) na ndani ya dakika 20 mchezaji wa Simba, Joseph Kaniki alishawarudisha Waarabu katikati ya uwanja mara mbili.

Ndipo mvua kubwa iliponyesha na mchezo kuarishwa hadi kesho yake, ambapo Simba alishinda bao 1-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.

pkisiraga@gmail.com

twitter: @PixiDeHaya