Nafasi nyingiii bao chache

Muktasari:

Data hizi hapa zinaweka mambo yote bayana juu ya timu zilizotengeneza nafasi juu za kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kwa kuzingatia vigogo waliopo kwenye Top Six.

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER City ndiyo timu inayoonekana kufunga mabao kwa kadri inavyojisikia kwenye Ligi Kuu England, kutokana na kufunga mara nyingi kuliko timu yoyote ile, lakini je ni wao waliotengeneza nafasi nyingi?

Data hizi hapa zinaweka mambo yote bayana juu ya timu zilizotengeneza nafasi juu za kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kwa kuzingatia vigogo waliopo kwenye Top Six.

Liverpool – nafasi 155, mabao 21

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Liverpool inashika nafasi ya tano kwa sasa kutokana na kukusanya pointi 19 katika mechi 11 ilizocheza. Liverpool imeshinda mechi tano, sare nne na kupoteza nne, lakini ikiwa timu namba moja kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga katika ligi hiyo kwa msimu huu. Liverpool imetengeneza nafasi 155, lakini imefunga mabao 21 tu.

Man City – nafasi 145, mabao 38

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, vinara Manchester City ndio wanaonekana kuwa na fowadi inayoweza kutumia nafasi nyingi zaidi ilizozipata katika mechi hizo 11 ilizocheza. Man City haijapoteza mechi hadi sasa, ikikusanya pointi 31 katika mechi 11 ilizocheza kwa maana imeshinda mara 10 na kutoka sare mara moja tu. Wakati ikielezwa kwamba imefunga mara nyingi kuliko wengine, lakini Man City imeshindwa kuzitumia vyema nafasi ilizotengeneza kutokana na kufunga mara 38 tu katika nafasi 145 ilizotengeneza katika Ligi Kuu England msimu huu.

Arsenal – nafasi 142, mabao 20

Kikosi cha kocha Arsene Wenger kimezidiwa bao moja tu la kufunga na Liverpool na hilo ndilo linalowafanya kushika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo kwa sababu timu hizo zote mbili zimelingana pointi, zina pointi 19. Kwenye tofauti ya mabao wapo sawa pia, Liverpool ikifunga 21 na kufungwa 17 (+4) na Arsenal imefunga 20 na kufungwa 16 (+4). Kwa msimu huu katika Ligi Kuu England, Arsenal imeonekana kwamba haijatumia vizuri nafasi ilizotengeneza kutokana na kufunga mara chache, 20 tu huku ikiwa imetengeneza nafasi za kufunga 142.

Tottenham – nafasi 137, mabao 20

Tottenham na mahasimu wao Arsenal hawajatofautiana kwa kufunga msimu huu, timu hizo mbili mahasimu wakubwa wa huko London, ambao leo watamenyana, wote wamefunga mabao 20 katika mechi 11 walizocheza kwenye Ligi Kuu England.

Lakini, kwenye msimamo, Spurs inashika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 23 katika mechi hizo 11 baada ya kushinda saba, sare mbili na kupoteza mbili. Spurs wao wamefungwa mabao matano tu. Lakini, umakini unaonekana kuwa tatizo baada ya kufunga mabao hayo 20 tu katika nafasi 137 za mabao ilizotengeneza kwa msimu huu.

Chelsea – nafasi 121, mabao 19

Mabingwa watetezi kwenye Ligi Kuu England msimu huu wanatia aibu, wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi baada ya kukusanya pointi 22 katika mechi 11 ilizocheza, wameshinda saba, sare moja na kuchapwa tatu. Chelsea wameruhusu mabao 10 kwenye wavu wao, hivyo wanakuwa na chanya 9 tu katika tofauti yao ya mabao ya kufunga na kufungwa. Lakini, kwa msimu huu, Chelsea imeonekana kuwa na tatizo kwenye kufunga, kutokana na kuwa na uwiano usio mzuri sana kwa kufunga mara 19 tu katika nafasi 121 za kufunga ilizotengeneza kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Man United – nafasi 108, mabao 23

Kwenye Top Six, Manchester United ndiyo timu iliyotengeneza nafasi chache zaidi za kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Jambo hilo pengine ndilo lililomfanya straika wao Romelu Lukaku kushindwa kufunga mabao kwa siku za karibuni, akitoka kapa katika mechi saba za michuano yote iliyoshiriki Man United hivi karibuni.

Kwenye Ligi Kuu England, Man United inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo kwa kukusanya pointi 23, wao wametengeneza nafasi za kufunga 108, lakini wamefanikiwa kufunga mabao 23 tu.

Lakini, Man United ndiyo timu iliyofungwa mabao machache zaidi kwenye ligi hiyo msimu huu, imeruhusu wavu wake kuguswa mara tano tu.