Mwisho wa enzi za Wenger

Muktasari:

  • Wenger alizaliwa Oktoba 22, 1949 huko Strasbourg, Alsace. Kwa mujibu wa baba yake, Wenger alianza kuonyesha mapenzi ya mpira wa miguu alipokuwa na umri wa miaka sita tu. Kwa sasa umri wake ni miaka 68.

ILE muvi ya Arsene Wenger na Arsenal yake imefikia mwisho. Mfaransa huyo sasa ataachana na kikosi hicho chenye maskani yake Emirates mwishoni mwa msimu huu huku akiwa amekitumikia kwa karibu miaka 22.

Ndiyo, miaka 22. Hakika ni muda mrefu sana, Tanzania hapo ingekuwa imefanya uchaguzi wa kuchagua marais wake mara tatu tofauti. Kwa sasa kocha huyo anafikiria tu kibarua kipya, huku ikidaiwa kwamba anaweza kurudi zake kwao Ufaransa, akiripotiwa kuanzisha mazungumzo ya kujiunga na ama Paris Saint-Germain au AS Monaco, aliyeiwahi kuinoa miaka ya huko nyuma kabla ya kwenda Japan na baadaye kuhamia Arsenal mwaka 1996. Kwa mapenzi yake ya soka, Wenger anaweza kwenda kuinoa moja ya timu hiyo.

Wenger alizaliwa Oktoba 22, 1949 huko Strasbourg, Alsace. Kwa mujibu wa baba yake, Wenger alianza kuonyesha mapenzi ya mpira wa miguu alipokuwa na umri wa miaka sita tu. Kwa sasa umri wake ni miaka 68.

Alivyotua Arsenal

Wenger alitua Arsenal akitokea Nagoya Grampus Eight ya Japan. Lakini, kabla ya hapo alikuwa Monaco, ambayo aliinoa kati ya 1987 na 1994. Kwa maana hiyo, Nagoya alikaa kwa kipindi kifupi sana kabla ya kutua Arsenal, ambapo alichaguliwa kuinoa timu hiyo Oktoba 1996. kwa maana hiyo, Wenger anakaribia kukamilisha miaka 22 kwenye kikosi hicho na kuwa kocha aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwa waliopo kwa sasa. Katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi cha Arsenal, Wenger amebeba mataji matatu ya Ligi Kuu England, saba ya Kombe la FA na saba ya Ngao ya Jamii. Taji lake la mwisho la ligi kubeba ilikuwa 2004. Wenger ameifanya Arsenal kumaliza ya pili kwenye ligi mara sita tofauti, amecheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja. Wenger ameshinda mara tatu tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka kwenye Ligi Kuu England, huku akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi mara 15 tofauti katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi hicho cha Arsenal ambacho amekiongoza katika viwanja viwili tofauti kutoka Highbury hadi Emirates. Kitu kizuri kutoka kwa Wenger ni kwamba Arsenal ilimteua kuwa kocha wao Oktoba, mwezi ambao alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa. Kabla ya kuwa kocha, Wenger alikuwa mchezaji na kuwahi kuzichezea Mutzig, Mulhouse, ASPV Strasbourg na Strasbourg. Kwenye ukocha aliinoa pia Nancy ya Ufaransa.

Kipato chake Arsenal

Unaambiwa hivi, kipato cha Wenger kinatajwa kuwa ni Pauni 26 milioni. Ukiweka kando pesa anazopiga kwa kulipwa mishahara kwa huduma yake anayotoa huko Arsenal, kocha huyo amekuwa akitengeneza pesa pia kutokana na kuchapisha vitabu vyake kadhaa, ikiwamo kile kitabu kinachofahamika kwa jina la “Arsene Wenger: The Inside Story of Arsenal Under Wenger.”

Alikuwa mchambuzi wa soka pia kwenye michuano ya Euro 2016. Mshahara wake wa sasa huko Arsenal, Wenger analipwa Pauni 8 milioni kwa mwaka. Mkataba wake wa miaka miwili aliosaini kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana, unaonyesha kwamba kocha huyo analipwa Pauni 15 kwa kila dakika. Wakati alipotua Arsenal mwaka 1996, mshahara wake ulikuwa Pauni 500,000 kwa mwaka. Hiyo ina maana kwamba hadi wakati anaondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu atakuwa amevuna Pauni 100,000,000 kwa kipindi chote alichokuwa kwenye kikosi hicho.

Familia yake

Wenger ameachana na mkewe, Annie Brosterhous. Huyo ndiye aliyekuwa mkewe, ambaye alidumu naye kwenye ndoa kwa miaka 15. Annie alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu, ambaye aliwahi kuichezea Ufaransa katika michezo ya Olimpiki. Uhusiano wao wa kimapenzi ulianza katikati ya miaka ya tisini. Wawili hao walifunga pingu za maisha mwaka 2010, lakini wakaja kuachana mwaka 2015. Walikuwa wakiishi pamoja kwenye jumba lao huko Totteridge, London na walifanikiwa kupata mtoto wao wa kipekee, binti Lea mwaka 1997. Sababu kubwa ya Wenger kuachana na mkewe, Annie ilidaiwa kwamba kocha huyo aliangukia kwenye penzi la dogodogo flani hivi. Lakini, kabla ya Annie kuolewa na Wenger, alikuwa na mume mwingine, mcheza kikapu wa Ufaransa, George Brosterhous, ambaye aliza naye watoto wawili. Binti yake Wenger, kwa sasa ni mhitimu wa elimu ya Chuo Kikuu, ambapo alisoma Chuo Kikuu cha Cambridge University na kuhitimu mwaka 2017. Mtoto huyo aliwaliza kabla ya wazazi wake kufunga ndoa, ilikuwa kwenye kipindi chao cha uchumba na ndiye anayedaiwa kwamba aliukuwa chanzo cha wazazi hao kuoana.

Kumbe kafukuzwa

Kwa maelezo ya Wenger ni kama vile ameamua kuachia ngazi mwenyewe, lakini kumbe kinachoripotiwa ni kwamba kocha huyo amelazimishwa kuachia ngazi, kwa kifupi amefukuzwa. Mmiliki wa Arsenal, Stan Kroenke, ndiye aliyekuwa akimsapoti kocha huyo kwa muda wote licha ya kuwapo na kelele kutoka kwa mashabiki na mabosi wengine kwenye bodi kutaka aondoke, lakini sasa bosi huyo amedaiwa kuondoa shilingi yake kwa kocha huyo na hakuwa na namna nyingine zaidi ya Wenger kufunguliwa lango la kutokea. Hadi kufikia mwisho wa msimu huu, Wenger angekuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, lakini kwa sababu amelazimishwa kuondoka kabla ya mkataba wake kumalizika, basi atalipwa Pauni 11 milioni za fidia na mishahara yake kwa mwaka uliokuwa umebaki. Kitendo cha Kroenke kupoteza imani na Wenger kilifanya kazi kuwa rahisi sana ya Mfaransa huyo kung’atuka kuachia kitu alichokuwa akiking’ang’ania kwa muda wote licha ya kelele za mashabiki wengi.

Wachezaji wamwaga chozi

Wakati Wenger ameamua kufichua siri akiwaambia wachezaji wake kwamba mwisho wa msimu huu hataendelea kuwa kocha kwenye timu hiyo, kitendo hicho kiliacha huzuni kubwa kwa wachezaji na kusabababisha wengi wao kumwaga machozi. Wenger amedumu Arsenal kwa karibu miaka 22, kuna wachezaji wengine wanaocheza kwenye timu yake kwa sasa walikuwa bado hawajazaliwa, hivyo waliona kama wamempoteza baba yao vile. Kiungo Jack Wilshere, ambaye alisema anamchukulia Wenger kama baba yake vile kwa sababu ndiye aliyempa nafasi ya kucheza akiwa na miaka 16 na tangu wakati huo amekuwa akimwaamini hata pale mashabiki walipombeza uwanjani. Wilshere alisema wachezaji wa timu hiyo walipokea kwa mshtuko sana kauli ya kocha wao kwamba anaondoka na mmoja aliondoka akiwa anamwaga machozi baada ya Wenger kukamilisha hotuba yake ya kuaga. Baadaye, Wilshere alituma meseji yake kwenye Twitter na kumshukuru Wenger kwa kila kitu, jambo ambalo liliwavutia wachezaji wengi wa Arsenal na kubonyesha kitufe cha ‘like’ posti hiyo.

Amenoa mastaa 221

Ukitaka kufahamu kwamba miaka 22 si mchezo kwa kocha kudumu kwenye timu moja, cheki orodha ya wachezaji wote ambao Wenger aliwasajili akiwa kocha wa Arsenal. Kocha huyo amewanoa wachezaji 221 katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi hicho, kuanzia kipa David Seaman hadi straika Pierre-Emerick Aubameyang. Orodha hiyo ya wachezaji 221 ni hii hapa;

David Seaman, Lee Dixon, Tony Adams, Steve Bould, Nigel Winterburn, Martin Keown, Patrick Vieira, Paul Merson, David Platt, John Hartson, Ian Wright, Ray Parlour, Dennis Bergkamp, Remi Garde, Steve Morrow, John Lukic, Andy Linighan, Paul Shaw, Gavin McGowan, Scott Marshall, Stephen Hughes, Matthew Rose, Lee Harper, Ian Selley, Nicolas Anelka, Giles Grimandi, Marc Overmars, Emmanuel Petit, Luis Boa Morte, Christopher Wreh, Jason Crowe, Paolo Vernazza, Alex Manninger, Alberto Mendez, Jehad Muntasser, Matthew Upson, Isaiah Rankin, Kaba Diawara, Nelson Vivas, Freddie Ljungberg, Omer Riza, David Grondin, Fabian Caballero, Michael Black na Nwankwo Kanu.

Wengine ni Oleg Luzhny, Silvinho, Thierry Henry, Davor Suker, Stefan Malz, Ashley Cole, Tommy Black, Rhys Weston, Jermaine Pennant, Graham Barrett, Julian Gray, Brian McGovern, Lauren, Robert Pires, Sylvain Wiltord, Lee Canoville, Stuart Taylor, Moritz Volz, Igors Stepanovs, Tomas Danilevicius, Edu, Sol Campbell, Giovanni van Bronckhorst, Francis Jeffers, Junichi Inamoto, Richard Wright, John Halls, Carlin Itonga, Rohan Ricketts, Stathis Tavlaridis, Jeremie Aliadiere, Sebastian Svard, Juan, Gilberto Silva, Kolo Toure, Pascal Cygan, Ryan Garry, Rami Shaaban, David Bentley, Justin Hoyte, Jens Lehmann, Graham Stack, John Spicer, Jerome Thomas, Quincy Owusu-Adeyie, Gael Clichy, Cesc Fabregas, Ryan Smith, Frankie Simek, Olafur-Ingi Skulason, Michal Papadopulos, Jose Antonio Reyes, Robin van Persie, Mathieu Flamini, Sebastian Larsson, Danny Karbassiyoon, Johan Djourou, Manuel Almunia, Arturo Lupoli, Philippe Senderos, Patrick Cregg, Emmanuel Eboue, Alexander Hleb, Alex Song, Fabrice Muamba, Anthony Stokes, Nicklas Bendtner, Kerrea Gilbert, Abou Diaby, Emmanuel Adebayor, Tomas Rosicky, Theo Walcott, Julio Baptista, William Gallas, Matthew Connolly, Denilson, Mark Randall, Armand Traore, Mart Poom, Bacary Sagna, Eduardo da Silva, Lassana Diarra, Lukasz Fabianski, Fran Merida, Nacer Barazite, Kieran Gibbs, Henri Lansbury, Aaron Ramsey, Samir Nasri, Carlos Vela, Jack Wilshere, Francis Coquelin, Gavin Hoyte, Jay Simpson, Mikael Silvestre, Amaury Bischoff, Rui Fonte, Paul Rodgers, Andrei Arshavin, Vito Mannone, Thomas Vermaelen, Gilles Sunu, Wojciech Szczesny, Sanchez Watt, Craig Eastmond, Kyle Bartley, Thomas Cruise, Marouane Chamakh, Laurent Koscielny, Sebastien Squillaci, Jay Emmanuel-Thomas, Ignasi Miquel, Conor Henderson, Emmanuel Frimpong, Gervinho, Carl Jenkinson, Alex Oxlade-Chamberlain, Mikel Arteta, Yossi Benayoun, Per Mertesacker, Andre Santos, Chuks Aneke, Ryo Miyaichi, Oguzhan Ozyakup, Park Chu-Young, Daniel Boateng, Nico Yennaris, Santi Cazorla, Olivier Giroud, Lukas Podolski, Martin Angha, Serge Gnabry, Damien Martinez, Thomas Eisfeld, Jernade Meade, Nacho Monreal, Yaya Sanogo, Mesut Ozil, Chuba Akpom, Kristoffer Olsson, Hector Bellerin, Isaac Hayden, Gedion Zelalem, Kim Kallstrom, Joel Campbell, Calum Chambers, Mathieu Debuchy, Alexis Sanchez, Danny Welbeck, David Opsina, Ainsley Maitland-Niles, Stefan O’Connor, Gabriel, Petr Cech, Alex Iwobi, Glen Kamara, Ismael Bennacer, Krystian Bielik, Jeff Reine-Adelaide, Mohamed Elneny, Rob Holding, Granit Xhaka, Shkodran Mustafi, Lucas Perez, Chris Willock, Alexandre Lacazette, Sead Kolasinac, Reiss Nelson, Josh Dasilva, Joe Willock, Eddie Nketiah, Marcus McGuane, Ben Sheaf, Matt Macey, Henrikh Mkhitaryan na Pierre-Emerick Aubameyang.

Mourinho amuaga kwa kijembe

Baada ya kutangaza tu ataachia ngazi mwisho wa msimu huu, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye ni mpinzani mkubwa sana wa Wenger, amesema kocha huyo ataagwa kwa staili anayostahili wakati atakapokwenda na timu yake huko Old Trafford.

Si unajua, Man United na Arsenal zitacheza Aprili 29 na Mourinho atamuaga Wenger kama anavyostahili kuagwa. Makocha hao wawili wamekuwa na upinzani mkali sana tangu walipokutana kwenye Ligi Kuu England, Mourinho akianzia Chelsea kabla ya sasa kuwa kocha wa Man United.