Msimbazi, Jangwani mzuka umepanda

Muktasari:

Klabu hizo kongwe zinatarajiwa kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika pambano lao la 100 la Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965, huku kila timu ikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya mechi zao zilizopita za ligi hiyo wikiendi iliyopita.

Mwanza. WAKATI mshale wa saa kuelekea pambano la watani wa jadi wa soka nchini ukizidi kukimbilia kwa kasi, nyota wa zamani wa timu hizo na baadhi ya mashabiki wa mitaa ya Jangwani na Msimbazi wameshindwa kujizuia na kutoa yaliyopo mioyoni mwao.

Klabu hizo kongwe zinatarajiwa kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika pambano lao la 100 la Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965, huku kila timu ikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya mechi zao zilizopita za ligi hiyo wikiendi iliyopita.

Simba iliambulia sare mjini Iringa dhidi ya wenyeji wa Lipuli, kabla ya Yanga kupata pia sare dhidi ya Mbeya City siku moja baadaye. Hata hivyo utamu ni kwamba Simba itaikaribisha Yanga katika mchezo huo wa marudiano katika msimu huu ikiwa ndio vinara wa Ligi hiyo kwa pointi 59 ikiwazidi wapinzani wao alama 11, licha ya Yang kuwa na mechi mbili mkononi.

Kuelekea mpambano huo mkali, ambao utatoa picha ya timu inayoweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Nyota wa zamani na mashabiki wa klabu hizo jijini Mwanza wametoa dukuduku lao kuelekea mchezo huo na mitazamo yao.

KHALFAN NGASSA

Winga huyo wa zamani wa Pamba, Simba na Taifa Stars, anasema licha ya kuwa mchezo huo kuwa mgumu, Simba ina nafasi kubwa ya kuondoka na pointi tatu.

Anasema kuwa kutokana na morali ya wachezaji na rekodi waliyoiweka mpaka sasa ya kutopoteza mchezo wowote vinaweza kuibeba kwenye mpambano huo.

“Mchezo huo ni mgumu kwa pande zote, lakini Simba nawapa asilimia kubwa ya kushinda kutokana na ubora wao na rekodi waliyoiweka msimu huu kwa kucheza mechi zote bila kupoteza,” anasema Ngassa ambaye ni baba mzazi wa nyota wa zamani wa timu hizo, Mrisho Ngassa anayekipiga Ndanda FC kwa sasa.

Ngassa anasema mara nyingi mechi ya Watani hao inapofika presha kuanzia uongozi hadi kwa Mashabiki hupanda kwa kiasi kikubwa, hivyo mwenye bahati na maandalizi mazuri ndiye atatoka kifua mbele pale Taifa.

Anasema kuwa vikao mara kadhaa huwa vingi, huku kamati mbalimbali zikitengwa kwa ajili ya mpambano huo, hivyo ni ngumu kutabiri atakayeshinda haraka.

JUMA AMIR MAFTAH

Straika huyu wa Pamba, Simba na Taifa Stars, anasema mchezo huo hautabiriki kwa wepesi kutokana na presha ya timu zote mbili na kwamba atakayefanya maandalizi mazuri ndiye ataondoka na ushindi.

Anasema kuwa licha ya wengi kuibeza Yanga kutokana na hali yao kwa sasa ilivyo, inaweza kuwashangaza wengi na kumlaza wanayeamini anaweza kushinda.

Anaongeza kuwa kwa tathimini yake kutokana na ubora wa timu zote, anaipa Simba nafasi ya kuchomoza na ushindi kwenye mtanange huo na kwamba kasi ya wachezaji wa kikosi hicho ni hatari.

“Kwa ujumla mchezo utakuwa mgumu, Yanga inabezwa ila inaweza kushangaza wengi, lakini kwa tathmini yangu fupi nawapa Simba nafasi ya kuweza kushinda,” anasema Nyota huyo.

AUGUSTINO MALIMA

Kipa huyu wa zamani wa TP Lindanda, (Pamba) anasema anaipa nafasi kubwa Yanga kushinda kwani safu yao ya ushambuliaji ipo vizuri huku beki ya Simba ikiwa na makosa ya mara kwa mara.

Anasema iwapo Yanga watatulia na kuwasoma wapinzani wao, wanaweza kuwatandika Simba mabao mengi.

“Yanga wanaweza kushinda mchezo huo kutokana na umakini watakaoutumia washambuliaji wake. Simba ni wazuri sehemu nyingi lakini eneo la ulinzi huwa si la kuaminika sana,” anasema Malindi.

MNENGE SULUJA

Winga huyu wa zamani wa Pamba na Simba, anasema mchezo huo ni mgumu kutokana na timu zote kuhitaji ushindi, lakini akawapa ushauri Simba kuwa ili iweze kupata alama tatu mabeki wawe makini kuwazuia Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib, kuhakikisha hawaleti usumbufu langoni mwao.

Anasema kuwa lazima Simba ijaze viongo wengi ili kuwamaliza mapema Yanga kwa kuhakikisha wanawabana mwanzo mwisho na hatimaye kuondoka na ushindi.

“Mabeki wa Simba wawe makini kuwazuia Chirwa na Ajib wasikatize miguuni mwao, wajaze viungo wengi ili kuwabana wapinzani wao kama kweli wamedhamiria kushinda,” anasema Suluja.

WASIKIE MASHABIKI

Shabiki lialia wa Yanga, Emmanuel Majura ‘Ema Yanga’ anasema Simba isitarajie mteremko katika pambano hilo kwani anawaamini wachezaji wao watafanya kweli.

Anasema kwa kawaida Yanga inapokutana na Simba huwa inabadilika sana hata kama ina mapungufu kadhaa, hivyo mchezo wa Jumapili wanaamini kwamba watatoka uwanjani kwa kicheko.

“Tunawaombea sana wachezaji wetu siku hiyo wawe fiti, wafuate melekezo wasitetereke, hata hivyo Yanga ikikutana na Simba huwa kuna mabadiliko makubwa, hivyo matarajio yetu ni ushindi,” anasema Majura.

Anasisitiza kwamba wao kama sehemu ya mashabiki wamejipanga kuisapoti timu hiyo kwa hali na mali kuhakikisha wanatetea ubingwa wao kwa mara ya tatu mfululizo. Naye Khamis Maluli, anasema kuwa liwake jua lazima Chama lao lifanye kweli na kutibua rekodi kwa wapinzani wao ambao hawajapoteza.

“Tunaenda kumchinja huyo anayejiita Mnyama, tunamchuna vizuri, pale hachomoki, tuna uwezo vijana wetu tunawaamini sana kinachohitajika ni uzima kila mmoja kujitokeza kushuhudia mchezo huo,” anatamba Maluli ambaye ni Katibu wa Mashabiki Jijini Mwanza. Naye Hassan Kaheshi, Shabiki wa kugalagala wa Msimbazi anasema kuwa mechi hiyo ndio ya kutangazia ubingwa o kwa msimu huu na kwamba moto wa Wekundu hauzimiki kirahisi na hakuna anayeweza kuzuia mafuriko kwa mikono.

Anasema ubora na uwezo wa kikosi cha Simba kwa msimu huu ni moto wa kuotea mbali, hivyo Mashabiki wa Simba popote nchini wajitokeze kwa wingi kusherehekea ushindi kwenye mchezo huo wa Jumapili.

“Sisi mashabiki Mwanza tayari tumejipanga kusafiri kuisapoti timu yetu na hii ni kutokana na kuamini kwamba tunashinda na kutangazia ubingwa,” anasema Kaheshi.