Mo Salah na ishu ya Ronaldo, Messi

Muktasari:

  • Misri walicheza na Uruguay kwenye Kundi A, lakini supastaa huyo Mo Salah aliishia tu kukaa benchi. Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa msimu uliopita, jambo hilo lilimfanya winga huyo kuanza kulinganishwa na mastaa wa dunia kama Lionel Messi wa Argentina na Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Ureno.

SIKU ambayo alitimiza umri wa miaka 26, supastaa wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah, aliwekwa benchi wakati akishuhudia timu yake ikichapwa bao 1-0 na Uruguay kwenye mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia kule Russia. Ilikuwa Ijumaa iliyopita.

Misri walicheza na Uruguay kwenye Kundi A, lakini supastaa huyo Mo Salah aliishia tu kukaa benchi. Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa msimu uliopita, jambo hilo lilimfanya winga huyo kuanza kulinganishwa na mastaa wa dunia kama Lionel Messi wa Argentina na Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Ureno.

Katika kusherehekea miaka hiyo 26 ya kuzaliwa ya Mo Salah, Mwanaspoti linajaribu kukuletea kile walichofanya mastaa anaolinganishwa nao staa huyo wa Anfield, yaani Messi na Ronaldo wakati na wao walipotimiza umri wa miaka 26.

Ukweli ni kwamba hakuna uwiano hata kidogo, Mo Salah kuwafikia Ronaldo na Messi kwa walichofanya wakati wanatimiza umri wa miaka 26, ni mbingu na ardhi.

Lionel Messi, alitimiza miaka 26, Juni 24, 2013

Wakati anasherehekea kutimiza umri wa miaka 26 ulikuwa ni mwisho wa msimu wa 2012/13. Kipindi hicho, Lionel Messi alikuwa kwenye fomu yake kweli.

Muargentina huyo aliweka rekodi ya dunia kwenye kufunga baada ya kutupia wavuni mabao 91 ndani ya mwaka mmoja (2012) na akabeba tuzo ya Ballon d’Or, iliyokuwa ya nne mfululizo. Messi akawa amefikia kwenye kiwango bora kabisa duniani, alipofikisha umri wa miaka 26 tayari alikuwa ameshashinda mataji sita ya La Liga, matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mengine mawili ya makombe ya ndani.

Cristiano Ronaldo, alitimiza miaka 26, Februari 5, 2011

Supastaa, Ronaldo, alitimiza umri wa miaka 26 katika nyakati alizoanza kupelekeshwa na Messi licha ya kuwa na kiwango bora cha mpira.

CR7, kama anavyofahamika kwa mashabiki, alikuwa bado hajaanza kubeba mataji ya maana huko Madrid, alikojiunga kwa ada ya Pauni 80 milioni mwaka 2009.

Lakini, alibeba Copa Del Rey miezi michache baada ya siku yake ya kuzaliwa. Hata hivyo, licha ya kwamba alikuwa bado hajatamba sana kwenye La Liga wakati huyo, Ronaldo alitokea Man United, ambako alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England, taji moja la FA, mawili ya Kombe la Ligi na Ballon d’Or mara moja.

Mo Salah, ametimiza miaka 26, Juni 15, 2018

Huu ni ukweli kuhusu Mo Salah na kile alichovuna kwenye soka wakati anatimiza umri wa miaka 26. Kitu bora zaidi kwake kama mchezaji ni kufunga mabao 44 ndani ya msimu mmoja, huku akifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kikosi chake cha Liverpool. Alifika fainali pia ya Mataifa ya Afrika akiwa na kikosi cha Misri.

Mafanikio yake makubwa ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Uswisi, wakati alipokuwa na kikosi cha FC Basel mara moja katika msimu wa 2012/13.