Mo Salah anavunja tu rekodi huko Liverpool

Muktasari:

  • Staa huyo peke yake alipiga Bao Nne, Liverpool ikiichapa Watford 5-0 na kuzidi matarajio yote waliyokuwa nao wababe hao wa Anfield wakati walipomsajili staa huyo kutoka AS Roma.

ACHA Liverpool waingiwe wazimu kwa soka maridadi linalochezwa na Mohamed Salah.

Staa huyo peke yake alipiga Bao Nne, Liverpool ikiichapa Watford 5-0 na kuzidi matarajio yote waliyokuwa nao wababe hao wa Anfield wakati walipomsajili staa huyo kutoka AS Roma.

Katika mechi hiyo, Salah alipiga asisti pia ya bao jingine lililofungwa na Roberto Firmino kwenye mechi hiyo na kumfanya awe amehusika kwenye mabao yote iliyovuna Liverpool juzi Jumamosi huko Anfield kwenye mechi ya Ligi Kuu England.

Lakini, mabao hayo yanamfanya Salah kuendelea kuzivunja tu rekodi kwenye kikosi hicho cha Liverpool. Sasa ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya msimu kumalizika, kuna uwezekano mkubwa wa Salah akaendelea kuzipukutisha na kuweka rekodi nyingine katika kikosi hicho cha Kocha Jurgen Klopp.

Rekodi ambazo Mo Salah a.k.a Messi wa Misri, ameshazivunja hadi sasa huko Liverpool ni hizi hapa.

Mabao mengi msimu wa kwanza

Kwenye historia ya Liverpool, Salah ndiye mchezaji wa kwanza aliyefunga mabao mengi katika msimu wake wa kwanza katika kikosi hicho chenye maskani yake Anfield. Kabla ya hapo hakukuwa na mchezaji aliyefunga mara nyingi kama alivyofanya Salah msimu huu.

Staa huyo hadi sasa ameshatupia wavuni mabao 36, mabao 28 Ligi Kuu, moja Kombe la Ligi na saba Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amecheza mechi 40 tu na hivyo anavunja rekodi iliyokuwa imewekwa na Fernando Torres, aliyekuwa amefunga mabao 33 katika msimu wake wa kwanza Liverpool, 2007/08.

Mfungaji wa mabao mengi wa Liverpool

Tangu kuanza kwa Ligi Kuu England, Liverpool iliwahi kuwa na mchezaji mmoja tu aliyefunga mabao mengi zaidi kwa msimu mmoja. Kutokana na Salah kufunga mabao 36 katika mechi 40 alizocheza hadi sasa, amefikia rekodi ya Robbie Fowler, ambaye alifunga idadi kama hiyo ya mabao katika mechi 53 alizocheza katika msimu wa 1995/96. Hakuna mchezaji mwingine aliyewahi kufunga idadi kubwa ya mabao hivyo kwenye kikosi cha Liverpool ndani ya msimu mmoja tangu kuanza kwa Ligi Kuu England.

Mabao mengi mguu wa kushoto

Supastaa Mo Salah ni mchezaji anayefahamu vyema kuutumia mguu wake wa kushoto. Katika mabao yake 36 aliyofunga msimu huu, mabao 23 ameyasukumia wavuni kwa mguu wa kushoto na hivyo kuvunja rekodi ya Fowler, aliyekuwa akiongoza kwa kufunga mara nyingi kwa mguu wa kushoto katika msimu wa 1994/95 alipofunga mabao 19.

Salah bado ana nafasi kubwa ya kuongeza mabao yake ya mguu wa kushoto kwa msimu huu kwa sababu Ligi Kuu haijamalizika na Liverpool bado ipo Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kinara wa mabao ligi za Ulaya

Ukihesabu zile Ligi Kuu tano bora za Ulaya, yani England, Hispania, Ufaransa, Italia na Ujerumani, kote huko Mo Salah ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi kuliko wachezaji wengine wote wanaocheza kwenye ligi za nchi hizo ikiwamo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Hata Robert Lewandowski na Edinson Cavani wamefunikwa na Salaha kwa mabao. Staa huyo wa Misri amefunga mabao 28 kwenye Ligi Kuu England na kuwazidi mastaa kama Harry Kane, Cavani na Messi, ambao wamefunga mabao 24 kila mmoja.

Mpasia nyavu maridhawa

Kama mchezaji ameweza kuonyesha usahihi wa kupasia nyavu kwa kila nafasi anayopata basi Mo Salah amethibitisha hilo.

Winga huyo wa Kiafrika alifunga mara nne katika mashuti yake manne aliyopiga dhidi ya Watford.

Mchezaji mwingine kuwahi kufanya hivyo Ligi Kuu England ni Andrey Arshavin, wakati alipofunga mara nne uwanjani Anfield, Liverpool ilipomenyana na Arsenal mwaka 2009. Kwa maana hiyo, Mo Salah amevunja rekodi hiyo ya staa wa Russia, Arshavin.

Mabao mengi kwenye mechi moja ya ligi

Tangu Liverpool ianze kucheza Ligi Kuu England hakuna mchezaji wao aliyewahi kufunga zaidi ya mabao manne katika mechi moja ya ligi hiyo. Lakini, kwa kitendo cha Salah kufunga mara nne dhidi ya Watford juzi Jumamosi, jambo hilo linamfanya aingie kwenye anga za magwiji waliowahi kutupia wavuni mara nne katika mechi za Ligi Kuu England. Mastaa hao ni Fowler (1995 na 1996), Michael Owen (1998 na 2003) na Luis Suarez (mwaka 2013).

Rekodi ambazo Salah bado hajazivunja

Salah anafukuzia rekodi ya kuwa mfungaji wa mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu England ndani ya msimu mmoja. Kuna wachezaji wanne wanaoshikilia rekodi huo ambao walifunga zaidi ya mabao 30, ambao ni Andy Cole, Alan Shearer, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez.

Mfungaji bora Mwafrika Ligi Kuu England, ambayo kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na Didier Drogba, aliyefunga mabao 29 katika msimu wa 2009/10 na nyingine kibao ikiwamo ya mfungaji bora wa Liverpool kwa msimu mmoja, Ian Rush, aliyefunga mabao 47 katika mechi 65 alizocheza kwenye msimu wa 1983/84. Rekodi ya mabao mengi ndani ya msimu mmoja Ligi Kuu England kwa Liverpool inashikiliwa na Suarez, aliyefunga mara 31.