Mkapa: Aliipiga Simba kijanja tu

Muktasari:

  • Nidhamu yake na kujitoa kwa ajili ya timu ilimfanya awe mmoja ya nyota waliolitetemesha soka la Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

KWA mashabiki wa soka jina la Kenneth Pius Mkapa sio geni. Unajua kwa nini? Jamaa alikuwa anajua soka bwana, asikuambie mtu. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, alikuwa hana utani uwanjani. Haikujalisha yupo mazoezi ama katika mechi, beki huyo wa kushoto alikuwa mtu wa kazi.

Nidhamu yake na kujitoa kwa ajili ya timu ilimfanya awe mmoja ya nyota waliolitetemesha soka la Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mkapa alisifika kwa uwezo wake wa kukaba washambuliaji wasumbufu na uwezo wa kupandisha mashambulizi ya timu yake, mbali na umahiri wa kufumua mashuti makali na kufunga mabao muhimu.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na beki huyo mkimya na kufichua ishu yake ya kutafuna fedha za Simba waliomsajili, kisha kuamua kusalia Jangwani mpaka alipostaafu soka la ushindani. Ilikuwaje? Ungana naye upate uhondo kamili.

YULE YULE

Asikuambie mtu, Mkapa enzi akicheza alikuwa mtu mkimya mno, alikuwa anapenda sana kufanya mambo kwa vitendo kuliko kuongea sana. Licha ya kuwahi kuwa nahodha wa Yanga, lakini ilikuwa nadra kumsikia akichonga kama baadhi ya nyota wa sasa, kitu ambacho hata sasa akiwa amestaafu soka, hajabadilika.

Hapendi kuzungumza mara kwa mara, ndiyo maana ni nadra kumsikia akichambua chochote, sio kama hayupo ndani ya familia ya soka. Hapana ni tabia yake ya kuzaliwa na pengine malezi aliyolelewa, lakini ni mtu makini na mwenye upeo mkubwa na ndio maana amecheza kwa muda mrefu akiwa na nidhamu na ubora uleule hadi anastaafu rasmi.

Kwa sasa mkali huyo anaishi maeneo ya Buguruni Rozana, akiendelea na maisha yake huku akifuatilia kwa ukaribu kila kinachoendelea katika soka la Tanzania na sarakasi zake.

AKIPIGA VIWANDANI

Mkali huyo anasema soka lake lilianzia utotoni, lakini kwa muda mrefu alicheza katika viwanda na ndio alikuwa anafanya kazi, huku soka hilo likiwa na ushindani baada ya kuvikutanisha viwanda mbalimbali katika mashindano ambayo walikuwa wakishiriki.

“Nilichezea timu ya Kiwanda cha Uchapishaji Tanzania (KIUTA) mwaka 1983 nakumbuka tulikuwa tunacheza, nikiwa mfanyakazi kiwandani kabla ya kupitishwa ridandasi na kujikuta nikiachana na timu hiyo na kuingia mitaani,” anasema Mkapa.

Licha ya kucheza timu za mchangani za Costa Rica na Risasi za Mbagala pia amekipiga Tiger ya Mtoni Mtongani kabla ya mwaka 1985 alipojitosa Tambaza ya Magomeni na kushiriki nao Ligi Daraja la Nne.

Anasema akiwa na timu hiyo ndipo uwezo wake ulipoonekana na kuonwa na klabu kubwa ikiwamo Pan Africans iliyomsajili mwaka uliofuata wa 1986 kabla ya kudakwa na Yanga na kujipatia umaarufu mkubwa wa soka lake la jihadi.

MISHAHARA KWA MBINDE

Mkapa anasimulia, enzi zao wakicheza, walikuwa wanatakiwa wacheze na kupata ushindi ili waweze kupata posho pamoja na mishahara lakini kama ikitokea wamepoteza, wanakuwa wanajipunguzia kiwango cha kupata pesa.

“Mapato yetu yalikuwa yanapatikana vizuri tukiwa tumepata ushindi. Watu walikuwa wanakuja uwanjani kwa wingi mpaka waone tumepata ushindi, kuja kwao kwa wingi tulikuwa tunapata mapato mengi ya mlangoni ndio na sisi tulipwe, lakini kama tukipoteza mashabiki hawaji hivyo na sisi pesa tunapata ndogo, ilikuwa tunalazimika kupata ushindi ili kuwavutia mashabiki,” anasimulia.

Aliongeza ukongwe wa klabu ambao ulikuwa nao, pia uliwahitaji kupata matokeo mazuri ili kulinda heshima ya klabu na sio kupoteza katika michezo yao ili kulinda heshima ya klabu kwa kufanya vizuri.

NDOTO ZA UPADRI

Katika maisha kila mtu huwa na ndoto zake na kwa bahati mbaya wachezaji wengi ukizungumza nao kuhusu ndoto walizokuwa nazo utoto hudai walitamani wawe wafanyabiashara wakubwa ama wasomi, ila kwa Mkapa hali ni tofauti.

“Nikiwa mdogo nilikuwa napenda siku moja nije kuwa padri kutokana na mazingira niliyolelewa na kukulia, lakini kadri siku zilivyokuwa zinaenda mbele soka lilinimeza na kubadilisha upepo wa ndoto hizo.”

Anasema hata licha ya kuumia kushindwa kutimiza ndoto zake, lakini anashukuru soka limemsaidia kwa mambo mengi, akiamini kila kitu wakati mwingine ni mipango ya Mungu Mwenyezi.

AHAMISHIWA MBELE

Kawaida ya mchezaji kiraka huwa anacheza sehemu ambazo zinalingana, kama ni beki basi ataweza kucheza nafasi zote za ulinzi bila tatizo, lakini Mkapa ni tofauti kwani licha ya kumudu beki, alijikuta akihamishiwa nafasi ya ushambuliaji.

Anakiri licha ya kutokuizoea nafasi hiyo, lakini kwa namna hali ilivyokuwa ya uhaba wa washambuliaji, ililazimika kucheza na kwa bahati alimudu.

“Ilinichukua muda kuzoea nafasi ile kwa vile sikuwa na mazoea nayo, ila kujitoa na kuwa na uthubutu ulinifanya niwe na mafanikio, nakumbuka katika msimu huu, nusu yake nilicheza beki na duru la pili nilicheza mbele.”

ALIYEMNYIMA RAHA

Mkapa anakiri katika kipindi chake, alikutana na wakati mgumu, pindi Yanga inacheza na RTC ya Shinyanga, kwani walikuwa na winga Ahmed Abbas aliyekuwa akimpa tabu.

“Huyu jamaa ilikuwa hatari sana nikikutana naye, kwani alikuwa mjanja mjanja sana katika uchezaji wake, alikuwa sio mtu wa kutulia sehemu moja unaweza ukasema umemkaba kumbe kashahama na anafunga,” anasema.

Anaongeza mchezaji huyo alikuwa akitumia akili nyingi akiwa na mpira, hivyo hata katika kumkaba alikuwa anatumia akili nyingi kuliko nguvu kwani angekuwa anafanya kutumia nguvu basi angekuwa anasumbuliwa na mchezaji huyo.

Mkapa anakiri enzi akicheza kuna mambo kadhaa ya kishirikina aliyokutana nayo na hasa inapokaribia mechi kubwa, pia anafichua vimbwanga vya mechi za watani havikuanza leo, sambamba na kuanika jinsi alivyoiliza Simba fedha zao. Ki vipi?

Itaendelea Jumatatu ijayo