Mechi za kibabe Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Man United ilishinda 2-1 na hivyo kujiweka pazuri katika kuondokana na presha ya kuhusu nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

MANCHESTER United na Liverpool wameshamalizana juzi Jumamosi. Mabao mawili ya Marcus Rashford yalitosha kwa Jose Mourinho kumtambia mpinzani wake, Jurgen Klopp, ambaye kabla ya mechi hiyo huko Old Trafford alichonga sana domo akiponda mfumo wa mpinzani wake kuwa yeye hachezi kwa kupaki basi.

Man United ilishinda 2-1 na hivyo kujiweka pazuri katika kuondokana na presha ya kuhusu nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Kitu cha kushangaza kuhusu mechi hiyo, kulikuwa na kadi tatu tu za njano ndizo zilizoonyeshwa, ikiwa ni tofauti kabisa na ilivyotarajiwa Man United na Liverpool zinapocheza, kadi ni jambo la kawaida.

Hizi ndizo mechi za kibabe zaidi zilizoshuhudia kadi nyingi kwenye historia ya Ligi Kuu England.

Chelsea v Man United,

kadi 242

Zinapocheza Chelsea na Man United ni ubabe tu. Kwenye historia ya Ligi Kuu England, mechi hiyo ndiyo iliyoshuhudia kadi nyingi zaidi zikionyeshwa.

Kadi za njano zilizoonyeshwa katika mechi za wababe hao ni 232 na kadi nyekundu 10 na hivyo kufanya jumla ya kadi 242.

Everton v Liverpool,

kadi 225

Mahasimu wakubwa hawa. Mechi yao inaitwa Merseyside Derby. Mechi za Liverpool na Everton ndizo zilizoshuhudia kadi nyingi zaidi nyekundu baada ya kuonyeshwa 21 kwenye Ligi Kuu England.

Mechi hizo pia za kibabe imeshuhudia kadi 204 za njano zikionyeshwa na kufanya jumla ya kadi 225.

Arsenal v Man United,

kadi 223

Kwa miaka ya karibuni, Man United na Arsenal mechi zake zimekuwa na upinzani mkali sana. Hakuna timu inayopenda kupoteza kizembe kwenye mechi za aina hiyo na ndiyo maana zimekuwa na ushabiki mkubwa.

Man United na Arsenal mechi zake zimeshuhudia kadi 223, ikiwa kadi za njano 214 na kadi nyekundu tisa.

Arsenal v Chelsea,

kadi 223

Wababe wote hao ni wa kutoka Jiji la London. Kutokana na hilo ndicho kinachofanya mechi hizo kuwa na upinzani mkali kwa sababu ya ukweli hakuna timu inayotaka kuonekana kibonde ndani ya jiji hilo.

Upinzani huo umefanya mechi yao kuwa ya kibabe na kushuhudia kadi nyingi, na zimeonyesha kadi 223, njano 210 na nyekundu 13.

Arsenal v Tottenham,

kadi 219

London Derby. Arsenal na Tottenham ni mahasimu wakubwa kweli kweli kwenye soka la Ligi Kuu England. Timu hizo mbili zinapokutana, huwa panachimbika.

Kutokana na hilo, ndicho kitu kinachofanya mechi yao kuwa na kadi nyingi kwa kuwa ni ya kipinzani sana. Kwenye mechi zao, kadi 219 zimeonyeshwa, njano 208 na nyekundu ni 11.

Chelsea v Tottenham,

kadi 207

Mechi nyingine ya kibabe Ligi Kuu England kwa timu za London. Chelsea na Tottenham wanapokutana upinzani umekuwa mkali kweli kweli kwa siku za karibuni na hilo linafanya mechi yao kuwa na mvuto mkubwa. Kutokana na hilo, mechi zao zimefanya kushuhudia kadi nyingi, 207 jumla, za njano ni 198 na nyekundu ni tisa.

Chelsea v Liverpool,

kadi 197

Kwenye Big Six, mara nyingi timu zake zote zinapokutana shughuli huwa ni pevu. Jambo hilo linafanya hata mechi baina ya Chelsea na Liverpool kuwa ya upinzani zaidi kwa sababu hakuna timu inayopenda kupoteza kirahisi.

Upinzani huo umefanya mechi hiyo kuchezwa kibabe na ndiyo maana kadi zimekuwa nyingi pia na jumla ya kadi 197 zimeonyesha, njano 189 na nyekundu nane.

Liverpool v Man United,

kadi 196

Mahasimu wa jadi. Mechi za Liverpool na Man United huwa na mvuto wa kipekee. Wababe hao ni wapinzani wasiokwisha uhasama wao Ligi Kuu England na ndiyo maana mechi yao imekuwa miongoni mwa mapambano yaliyoshuhudia kadi nyingi zikionyeshwa kwa wachezaji.

Man United na Liverpool imeshuhudia kadi 196, njano zikiwa 180 na nyekundu ni 16. Ukiacha Everton na Liverpool, Man United na Liverpool ndiyo mechi iliyoshuhudia kadi nyingi nyekundu kwenye Ligi Kuu England.