Mechi ya Chamazi ilikuwa bab’kubwa

Muktasari:

  • Unajua kwa nini? Yanga kwa msimu huu imekuwa timu dhaifu na inayosuasua katika mechi zake kutokana na mambo mengi inayoisonga kwa sasa, lakini kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa ndani ya dakika 90, Azam iliduwaza Azam Complex.

MOJA kati ya mechi tamu za Ligi Kuu Bara katika msimu huu ilikuwa juzi Jumamosi kati ya Azam dhidi ya Mabingwa Watetezi, Yanga. Pambano hilo lilimalizika kwa matokeo yaliyowashtua wengi kwani hakuna aliyetarajia kama Azam ingekufa nyumbani.

Unajua kwa nini? Yanga kwa msimu huu imekuwa timu dhaifu na inayosuasua katika mechi zake kutokana na mambo mengi inayoisonga kwa sasa, lakini kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa ndani ya dakika 90, Azam iliduwaza Azam Complex.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 yapo mambo ambayo yalitokea na kuleta burudani kwa namna moja ama nyingine na kuacha yakiwa kama alama katika mchezo huo, Mwanaspoti linakumegua hapa.

Azam haikuiheshimu Yanga

Azam ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza tena likifungwa dakika ya nne tu na mchezo na straika chipukizi Shaaban Idd Chilunda. Dogo huyo alifunga kwa mguu wa kulia akimalizia mpira ulioguswa na kiungo wa Yanga Papy Kabamba Tshishimbi katika harakati zake za kuokoa krosi safi ya beki wa kushoto wa Azam, Bruce Kangwa na Chilunda hakuwa na kingine ila kuukwamisha mpira wavuni.

Baada ya bao hilo ilikuwa ni kama kilichotarajiwa na wengi walioamini Azam itashinda mchezo huo, hivyo wenyeji walijiaminisha kazi imeisha na kuidharau zaidi Yanga ambao ilitulia na kuifanya izinduke na kusawazisha dakika 30.

Bao hilo likifungwa na mchezaji yuleyule aliyewaliza Azam katika mechi yao ya marudiano ya msimu uliopita, Mzambia Obrey Chirwa.

Kitendo cha Yanga kutoka nyuma na kusawazisha bao kisha kupata la ushindi kinaonyesha Azam ilitawaliwa na akili kuwa Yanga haiko imara na ingeshinda kirahisi katika mechi ngumu hasa baada ya bao la kuongoza.

Nkongo aliwapa bao Azam

Mwamuzi Israel Mujuni Nkongo, alifanya kosa kubwa tena akiwa karibu na tukio akiacha Kangwa akifanya kosa la kuvuta beki wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy na Mzimbabwe huyo kutengeneza bao la kuongoza kwa wenyeji.

Nkongo alionyesha wazi aliathirika kisaikolojia kwa malumbano ya kutotakiwa kuchezesha mchezo huo yaliyokuwa yakiendelea siku moja kabla ya mechi. Hata baadhi ya maamuzi yake katika mchezo huo kuna wakati yalionekana kama hayakuwa sawa, kwa faulo zilizokuwa zikifanywa na wachezaji wakati mwingine zilipaswa kuwatolewa kadi hata nyekundu.

Yakubu bonge la beki

Azam ina ukuta mgumu, lakini uimara wa ngome hiyo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na beki Mghana, Yakubu Mohamed kwani ndiye nguzo ngumu muhimu kwao.

Haishangazi kama ataendelea na ubora huu na kutwaa tuzo ya beki bora mwishoni mwa msimu alikuwa ametulia na kufanya mambo kwa akili kubwa.

Inawezekana mtu akakataa hili kwa kigezo kwamba Yanga imefunga mabao mawili mbele yake, lakini ukaingalia mabao hayo yametokana na akili kubwa ya mipango ya Yanga kwa kugundua ukuta wa Azam ni mgumu na kufunga au kutengeneza mabao yao mbali na kuwasogelea mabeki wa kati na kuwanyima akili.

Utamlaumu Yakubu kwa lipi wakati mabao yote yalitokana na makosa ya kizembe ya kipa Razack Abalora aliyekosa umakini katika mchezo huo tofauti na alivyo.

Cioaba naye mtata

Kituko kikubwa katika mchezo huo ni Kocha wa Azam, Aristica Cioaba kuzozana na mashabiki kila mara na kufikia hata kutoa kauli chafu.

Mromania huyo alishindwa kuvumilia kejeli na maneno makali waliyotolewa na mashabiki na kuamua kuwajibu kwa kuwaonyesha kidole cha kati tukio ambalo Mwanaspoti lilimshuhudia mwamuzi wa akiba Herry Sasii akiliona na kuliandika katika katarasi yake, haitashangaza kama atafungiwa.

Sure Boy aliinunua kadi

Kadi nyekundu pekee katika mchezo huo aliyopewa kiungo wa Azam Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ kwa kosa la kumsukuma Hassan Kessy kama ilinunuliwa kwa lazima, kwani alifanya kitendo hicho wakati mwamuzi tayari alishaizawadia timu yake mpira wa adhabu kwa kosa alilofanya Kessy.

Hakuna maneno mazuri zaidi ya kusema kiungo huyo alinunua kadi hiyo kwa bei nafuu, kwani alitoka mbali na eneo la tukio na kumsukuma Kessy mbele ya mwamuzi, huku akijua tayari ana kadi ya njano aliyopewa mapema.

Mzozo ageuka mlinzi

Unamjua yule Herry Mzozo wa Friends Rangers ambaye ndiye bosi wa timu hiyo inayopambana kupanda Ligi Kuu? Jamaa ni mtata sana aliingia katika jukwaa la VIP na kukuta limejaa na kuzuiwa.

Jamaa hakukubali aliangusha mzozo hapo kusema hata kama kumejaa hadhi yake ni kukaa jukwaa hilo hata kama atasimama. Alipoona mambo magumu akaenda mbali zaidi akimtoa getini na kusema geti hilo atalilinda yeye na kufanikiwa kukaa hapo huku akiwaacha vigogo wengi wakiumia kwa vicheko.

Yanga iliiteka Chamazi

Azam ilikuwa nyumbani juzi, lakini ghafla ilijikuta kama ikiwa ugenini baada ya mashabiki wa Yanga kufurika kwa wingi na kufanya ubabe wa kuchagua sehemu ya kukaa.

Ingawa uwanja haukujaa lakini yale maeneo muhimu yote yalifurika mashabiki wa Yanga huku Azam ikiwa na mashabiki wachache kuliko wageni wao.

Utabiri mapema

Kabla ya Azam kuvaana na Yanga jioni, mapema kulipigwa mechi ya utangulizi ya vikosi B vya timu hizo na matokeo ni Yanga B kuinyuka wenyeji mabao 2-1 na kuwa kama utabiri wa matokeo ya mchezo wa timu kubwa. Na kweli bwana mechi ya wakubwa ikaisha baada ya dakika 90 kwa Yanga kutakata tena Chamazi.

Ushindi wa kwanza

Azam imepoteza mechi ya nne nyumbani, lakini mechi hiyo ina maumivu mara mbili dhidi ya Yanga kwa kuvunjiwa rekodi yao nzuri, pia wapinzani wao wakizindua uwanja huo kwa mara ya kwanza kwao. Kabla ya mechi hiyo, Yanga haikuwahi kushinda katika uwanja huo na matokeo mazuri kwao ni sare.Azam nayo kama ilivyokuwa kwa kipa wake namba moja Abalora kabla ya mechi hiyo haikuwa imefungwa mchezo wowote msimu huu. Rekodi hizo zimesitishwa rasmi na kuifanya Yanga kuungana na JKT Ruvu, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar kuwa timu pekee zilizofanikiwa kuondoka na matokeo mazuri katika uwanja huo.

Simba wabebwa kimtindo

Simba haikucheza juzi, katika mchezo huo iliwakilishwa na bosi wake Kaimu Makamu wa Rais Idd Kajuna na wekundu hao walikuwa na matokeo ya aina mbili waliyotaka yatokee. Kwanza ilitaka sare yoyote ile ili ijitanue zaidi kileleni, lakini kipigo cha Azam ni furaha kwa Simba, kwani kiliwaacha salama kileleni na jana ilijiongezea pointi katika Uwanja wa Taifa kwa kufunga majimaji mabao 4-0.