JICHO LA MWEWE: Mbona tuna akina Poulsen wengi tu hapa Tanzania!

TUNAHITAJI kuishi katika dunia yao na kujiamini. Wakati mwingine huwa nahoji jinsi ambavyo mashabiki wa soka nchini wanavyoamini kwamba, usafiri wa ndege ni wa kifahari kupitiliza. Unaweza kukutana na mashabiki ambao wanashangilia timu yao kupanda ndege.

Kwa mfano, katika soka letu, Simba ikipanda ndege kwenda Mbeya ni habari kubwa. Hapo habari inakuwa tamu zaidi. Yanga ikipanda ndege kwenda Mwanza ni habari. Kama ikitumia usafiri wa basi haiandikwi usafiri uliotumia.

Mambo mengi tunapaswa kuyaona ni ya kawaida tu ili tuyashinde kiurahisi, tukianza kuona mambo mengi ni ajabu, basi hatutafika katika safari yetu kwa sababu hatutaamini kama yanawezekana kwa urahisi sana.

Kwa mfano, mshambuliaji wa Denmark, Yussuf Poulsen juzi Jumamosi aliifungia Denmark katika pambano la Kombe la Dunia dhidi ya Peru. Ilikuwa ni habari iliyotikisa nchi. Kisa? Baba yake Yussuf ni baharia mmoja wa Tanga aliyezamia Ulaya na kuzaa na mwanamke wa Kizungu katika nchi ya Denmark.

Kwa sasa imekuwa habari ya mjini. Jiulize Nigeria ina akina Yussuf wangapi? Hata Dele Alli wa England ni Yussuf wao. Wana akina Yussuf zaidi ya 1,000 wanaochezea au waliowahi kuchezea mataifa mbalimbali. Hawajali sana.

Ghana hivyo hivyo. Ukipekua wachezaji wa Ghana waliowahi kuchezea mataifa mbalimbali tena ya nchi kubwa unajikuta unashangaa. Ndio, Walianza kusafiri zamani. Wanaiishi dunia. Wanaitawala dunia. Tulipaswa kuwa hivi.

Wakati Marcel Dessaily alipotwaa ubingwa wa dunia na Ufaransa mwaka 1998, Waghana hawakujali sana kama inavyotutokea sisi kwa Yussuf. Maelfu ya mastaa wa Ghana walishatamba Ulaya muda mrefu kabla ya Dessaily, ambaye aliamua kuitosa nchi yao.

Kwanini tunajali sana? Kwa sababu tumekosa uwezo wa kujiamini katika uwezo wetu. Hatusafiri sana wala hatujiamini sana. Ndio maana imeonekana ni ajabu kwa mtoto wa Mtanzania kuwa mchezaji mkubwa Denmark.

Tuache kuona vitu vya kawaida kuwa vitu vya ajabu. Tutafanikiwa. Kuna wachezaji wetu wengi ambao wana uwezo wa kucheza nje wakatamba kama Yussuf, lakini hawajiamini. Kama wachezaji hao wangeondoka na kutamba nje, leo habari ya Yussuf ingekuwa ndogo tu mitandaoni.

Kwa mfano, Nigeria haina muda wa kushupalia habari ya mtoto yeyote wa Mnigeria, ambaye anaichezea timu ya taifa jingine, kama vile Dele Alli, kwa sababu hata wao wenyewe wapo katika michuano hiyo na wachezaji wao wanacheza katika kiwango sawa na Dele. Hii ndio namna ya kufuta ushamba.

Tunahijika turudi nyuma na kuusimamisha mchezo wetu. Tujitegemee. Tusiwe na muda sana wa kujadili vitu ambavyo havitusaidii sana. Kama Taifa Stars ingekuwa katika fainali za Kombe la Dunia, basi leo tusingezungumza habari za Yussuf kwa ukubwa huu.

Tungemuona mchezaji wa kawaida kwa sababu tuna majukumu yetu.

Wakati mwingine, pia inakera kuona Watanzania tumerudi nyuma kimawazo na kutaka tuanze kuwapa uraia wachezaji wa kigeni wanaotamba nchini ili waichezee timu ya taifa. Bado taifa halijafika huko. Huu ni uvivu wa kutengeneza mpira wetu.

Taifa ambalo lilikuwa na Sunday Manara, Hamis Gaga, Sekilojo Chambua, Athuman China, Athuman Mambosasa, Mohamed Kajole na wengineo, leo haiwezekani ghafla lisiwe na vipaji. Kuna tatizo sehemu. Wachezaji wa kariba hii kama wangekuwepo leo hata hawa wa kigeni kina Thaban Kamusoko tusingewanunua.

Kuna wakati huwa tuna fikra tuanze kukusanya watoto wa Kitanzania waliozaliwa nje ambao, wanacheza soka. Ukifuatilia kwa karibu wapo wengi lakini viwango vyao wala havifikii vya baadhi ya wachezaji wetu mahiri wa ndani. Yule mchezaji wa Tanzania anayecheza pale England anafikia kiwango cha John Bocco? Sidhani.

Tuanze kuamini katika mambo makubwa zaidi. Naamini Yussuf angekuwa Tanzania asingefika alikofika. Amewekwa katika mfumo na amefika alikofika. Kwetu angeharibika. Kuna Watanzania wengi wana vipaji kuliko Yussuf, lakini tumewapoteza au wamejipoteza wenyewe.

Watanzania milioni 50 kuiona habari ya Yussuf kama kubwa ni ishara kwamba, kuna tatizo mahala. Kuna sehemu tumekosa kujiweka katika dunia ya watu walioitawala dunia. Wenzetu wasingeiweka kama habari kubwa sana.

Wenzetu wana watoto wa nchi zao waliozaliwa Ulaya ambao kwa sasa ni wachezaji mastaa, madaktari, Maprofesa, waandishi wa habari, wanasiasa mashuhuri, waandisi na watu wa nyadhifa mbalimbali.

Ni kitu cha kawaida kwa watu wanaojichanganya. Tujifunze kujiamini na kutawala maisha yetu pamoja na kujua kwamba, tumechelewa sana.