Mbao FC ni pesa juu ya pesa

Muktasari:

Katika Ligi Kuu msimu huu, ziko timu chache zilizofanikiwa kuzishawishi kampuni ili kuzidhamini.

MIONGONI mwa changamoto zinazoukabili mchezo wa soka nchini, ni hali ngumu ya kifedha inayozikabili klabu na taasisi mbalimbali za kisoka kila siku.

Klabu hizo zimekuwa zikihaha usiku na mchana kusaka kampuni zitakazosaidia kuwapa udhamini ili kupunguza gharama za kuhudumia timu zao.

Katika Ligi Kuu msimu huu, ziko timu chache zilizofanikiwa kuzishawishi kampuni ili kuzidhamini. Miongoni mwao ni Mbao FC ambayo baada ya kushiriki Ligi Kuu kwa msimu mmoja tu, tayari imevutia kampuni mbili kuipa udhamini.

COWBELL PESA

Baada ya Mbao FC kuzitikisa Simba, Yanga na Azam katika mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Mbao iliivutia Kampuni ya Hawaii Product Supplies ambayo iliingia mkataba wa kuidhamini timu hiyo ya jijini Mwanza.

Kampuni hiyo ya wazalishaji wa maziwa ya unga ya Cowbell, iliingia mkataba wa miezi sita (6) wa kuidhamini Mbao uliokuwa na thamani ya Shilingi 25 milioni pamoja na kuipatia vifaa vya mazoezi.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuwekeza kwenye mchezo wa soka lakini baadaye ilisaini pia mkataba na Ruvu Shooting.

Msimu huu imepanga tena kuendelea kuidhamini pamoja na kuongeza fungu la udhamini.

“Uendeshaji wa timu kwenye ligi ni wa gharama kubwa, sisi viongozi tusingeweza lakini kwa udhamini wa ndugu zetu wa Cowbell, tumefanikiwa kupunguza mzigo wa gharama na bila shaka ni miongoni mwa sababu zinazofanya tufanye vizuri,” anasema Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi.

MATAJIRI WENGINE

Wakati baadhi ya timu zikiishangaa Mbao ilivyoweza kuvutia kampuni hii na kupata mkwanja, hivi karibuni imewashangaza tena baada ya kusaini mkataba mnono wa Sh140 milioni kutoka Kampuni ya Uuzaji magari ya GF Trucks & Equipments.

Katika udhamini huo, Sh70 milioni zitatumika kuinunulia timu hiyo basi la kisasa huku  Sh.70 milioni zilizosalia  zitatumika katika shughuli za uendeshaji wa klabu. Mkataba huo ni wa mwaka mmoja huku kukiwekwa kipengele cha kuboreshwa zaidi mara baada ya Ligi Kuu kumalizika.

Kampuni hii pia ni mara ya kwanza katika udhamini wa mchezo wa soka kama inavyothibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa GF Trucks & Equipments, Imran Karmali.

“GF Trucks & Equipment Ltd haijawahi kushiriki katika udhamini wa soka la kiwango cha Ligi Kuu. Huu utakuwa ni udhamini pekee katika kampuni hii. Madhumuni ni kukuza vipaji vya mpira wa miguu na tunatarajia kusaidia Mbao FC kufikia malengo yake msimu huu.

“Tuliifuatilia timu hii kwa ukaribu tangu msimu uliopita ilipofika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA). Tuna matumaini kupitia udhamini wetu itaendelea kufanya kufanya vizuri,” alisema Karmali.

WAJIPANGA ZAIDI

Mratibu wa Mbao FC, Zephania Njashi alifichua mikakati ya kuwatangaza zaidi wadhamini wao pamoja na kuvutia wadhamini wengine zaidi kuwekeza kwenye timu yao.

“Klabu yetu ipo katika hatua za mwisho kuzindua tovuti yake ambayo itaenda sanjali na uzinduzi wa kurasa za mitandao ya kijamii, ili tupate nafasi ya kutosha kuitangaza timu pamoja na wadhamini wetu.

“Pamoja na hilo tutahakikisha tuna uongozi imara lakini pia tutaimarisha uhusiano wetu na vyombo vya habari ambavyo vimekuwa wadau wetu wakubwa,” anasema Zephania.

Mbao ilipanda Ligi Kuu msimu uliopita kwa bahati ya mtende kutokana na kutumia fursa ya kushushwa daraja kwa timu tatu zilizoongoza Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2015/2016 zilizotuhumiwa kujihusisha na upangaji wa matokeo ambazo ni Geita Gold, JKT Oljoro na Polisi Tabora huku Mbao iliyoshika nafasi ya nne, ikiangukiwa na bahati hiyo ya kupanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.