Mazoezi kwa wazee huongeza kumbukumbu

Friday August 11 2017

 

By DK. SHITA SAMWEL

FAIDA kubwa kufanya mazoezi ni kuiwezesha miili yetu kuwa na afya njema hivyo kutuepusha na maradhi kama vile ya kisukari, moyo, kiharusi na hata unene uliokithiri.

Mazoezi hayo yanaweza hata kuwa yake mepesi ambayo mhusika huyafanya huku akiendelea kupata hewa safi ya Oksijeni pasipo kusitisha upumuaji.

Mazoezi haya yana mchango mkubwa kiafya kwani, yanamsaidia mhusika kuwa na mzunguko mzuri wa damu, upumuaji mzuri, kudhibiti uzito wa mwili na kumfanya ajisikie vizuri kihisia.

Mazoezi hayo ni pamoja na kutembea, kukimbia kidogo kidogo, kuruka kamba, kucheza muziki, kuogelea na hata kufanya shughuli ndogo zinazohusisha viungo vya mwili kufanya kazi.

Zipo tafiti zinazozungumzwa mara kwa mara katika majarida na mitandao ya elimu ya sayansi ya tiba kuhusu mazoezi mepesi yanavyosaidia kuongeza siku za kuishi. Kikubwa hapa ni namna yanavyosaidia kutuepusha na maradhi.

Tafiti hizo pia zimegundua kwamba, mazoezi mepesi yanarudisha uwezo wa kukumbuka kwa wazee. Ikumbukwe, wazee wengi kuanzia umri wa miaka 60, uwezo wao wa kutunza kumbukumbu huanza kupungua.

Ugonjwa maarufu wa kupoteza kumbukumbuku ujulikano ni ‘Alzheimer disease’, ingawa si wote wanaopoteza kumbukumbu wana ugonjwa huu.

Ripoti iliyochapishwa katika Jarida la Health Physiology na kuchapwa katika tovuti ya WebMD, inasema wazee wenye tabia ya kufanya mazoezi ya kuendesha baiskeli au kujinyosha viungo, huongeza uwezo wao wa kukumbuka kuliko wale wasiofanya hivyo.

Matokeo ya Utafiti huo yanaonyesha kuwa pamoja na kwamba, kimuundo ubongo haufanani na misuli, lakini kadiri mtu anavyozeeka ufanyaji mazoezi husaidia kuimarisha uwezo wake wa kukumbuka na hata kufikiria mambo mapya.

Uzuri ni kwamba wazee hawahitaji kufanya mazoezi mazito katika vituo maalumu vya mazoezi, mazoezi ya ni kama kutembea, kunyoosha viungo na hata kucheza muziki.

Utafiti huo ulihusisha watu wazima, waume kwa wake, waliokuwa wakiendesha baiskeli au mazoezi ya kunyoosha viungo kwa muda wa saa mbili kwa wiki katika muda wa miezi sita, ulionesha kuwepo kwa maendeleo makubwa katika uwezo wao wa kukumbuka na hata kufikiria mambo mapya.

Ripoti hii inaweza kutafsiriwa kama changamoto kwa watu walio katika nafasi mbalimbali za kutoa maamuzi ya kiuongozi kuwa na tabia na ufanyaji mazoezi kwani, inaweza kuimarisha uwezo wao wa kukumbuka na kufikiria mambo mapya, na hivyo kuzidi kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku.

Ni vizuri kuibeba kama changamoto hata kwa watu wengine ili kuanzisha utaratibu wa kujifanyia mazoezi mepesi kwa ajili ya kuimarisha afya ya akili na mwili kwa ujumla.

Fanya haya ili kuufanyisha mwili mazoezi mepesi

Yapo mazoezi mepesi yanayoweza kufanyika ukiwa nyumbani au ofisini, ni rahisi kuyafanya ili kuweza kuwa na mwili imara wenye afya njema.

Ukiwa nyumbani au hata sehemu ya kazi, jenga mazoea ya kuushughulisha mwili wako ili misuli ya mwili kwa ujumla ifanye kazi.

Unapoamka asubuhi, cha kwanza unapaswa kukaa angalau dakika tano huku ukivuta pumzi ndefu na kutulia, kisha ukaanza kunyoosha viungo vya mwili wako kwa dakika kadhaa. Unaweza kutumia chumba unacholala kutembea umbali mfupi mara nyingi, kwenda na kurudi. Anza kidogo kidogo ili kujenga mazoea mpaka iwe ni kawaida yako.

Tumia nusu saa kila siku ukiwa ndani kwako kwa kutembea chumbani au nje ya nyumba. Unaweza pia ukachanganya na mazoezi mengine ikiwamo kuruka kamba. Kama uko ofisini unaweza ukajenga mazoea kwa kutembea, unaweza ukaepuka kutuma mtu kama vile kukuchukulia kikombe kwa ajili ya kahawa.

Badala ya kutumia zaidi rimoti kuwasha televisheni au kipooza hewa, tembea na ufanye mwenyewe. Tumia ngazi kupanda ghorofa na achana na kutumia lifti.

Kama unatumia usafiri wa umma, unaweza ukawa unashukia mbali kidogo na kituo chako ili utembee kuushughulisha mwili.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo ukiyafanya yataushughulisha mwili wake na kukupa matokeo chanya bila ya kutumia gharama yoyote.

Inashauriwa kujenga tabia ya kutembea angalau kilomita mbili kwa siku ukitumia kati ya dakika 30 hadi 45. Fanya hivyo mara tano kwa wiki.