Mayanga kama vipi inatosha

Monday October 9 2017

 

By GIFT MACHA

TAIFA Stars imekwenda mbele kisha ikarudi tena nyuma. Imefika mahala sasa tunapaswa kumwambia Kocha Salum Mayanga kuwa inatosha, kwani hasomeki kabisa Stars. Tunaweza kumwambia Mayanga sio kwa nia mbaya, ila ni kwa nia ya kuliokoa Taifa na majanga. Miezi 10 aliyokaa Taifa Stars inatosha kumuongezea wasifu wake.

Achana na matokeo ambayo Taifa Stars inapata, kinachokatisha tamaa ni kiwango kibovu cha timu hiyo chini ya kocha Mayanga.

Stars haichezi vizuri. Inashambuliwa muda mwingi wa mchezo. Timu haiwezi kupiga pasi 15 zikakamilika. Wachezaji wanakosa ubunifu na mbinu za kuvunja ngome za wapinzani. Inasikitisha sana kuona timu ya Taifa iko katika hali kama hiyo.

Mayanga alianza vizuri punde baada ya kuipokea timu mapema mwaka huu, lakini sasa mambo yako tofauti. Kiwango kilichoonyeshwa na Stars kwenye mechi dhidi ya Botswana na Burundi mwezi Machi mwaka huu kimetoweka kabisa.

Katika mechi iliyopita dhidi ya Botswana licha ya Stars kushinda kwa mabao 2-0 bado kiwango kilikuwa kibovu. Timu ilibebwa zaidi na uwezo wa Msuva na baadhi ya wachezaji wengine. Kwenye mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Malawi hali ilikuwa ambaya zaidi.

MFUMO UTATA

Kocha Mayanga ni muoga kufungwa, tena kupita kiasi. Inashangaza kuona katika mechi ya kirafiki anatumia straika mmoja na viungo watatu, tena akiwa nyumbani. Kwanini timu inajilinda nyumbani? Tena dhidi mechi ya kirafiki na timu ya kawaida kama Malawi?

Katika mchezo dhidi ya Malawi timu ilianza na Mbwana Samatta pekee kama straika. Raphael Daud alicheza nyuma ya Samatta na pembeni wakacheza Saimon Msuva na Shiza Kichuya. Inashangaza sana. Unawezaje kumpanga Daudi acheze nyuma ya Samatta wakati benchi kuna Ibrahim Ajibu na Mbaraka Yusuf? Kwanini timu inacheza soka la kujilinda ikiwa nyumbani?

Matokeo yake Stars ikashindwa kutengeneza nafasi. Mipira ilipokwenda mbele ilikosa watu. Samatta akaonekana kama anacheza chini ya kiwango. Kwanini tunampa wakati mgumu staa wa timu yetu?

Mfumo wa kujaza viungo wengi na kuchezesha washambuliaji wachache ni wa kizamani. Ni mfumo unaotumika katika mechi za mtoano hasa ukishapata ushindi kwenye mchezo wa nyumbani.

Ukienda ugenini unajaza viungo ili kuzuia zaidi kuliko kushambulia. Sio mfumo wa kutumia unapocheza nyumbani, tena katika mechi ya kirafiki na timu kama Malawi. Kwanini tunakwenda kinyume?

Timu inapokuwa nyumbani inatakiwa kushambulia zaidi na sio kukaba. Ni akili ya kawaida kwenye soka. Hili nalo ni jambo la kumkumbusha Mayanga? Kama timu inashindwa kushambulia ikiwa nyumbani itaweza kushambulia ugenini?

Angalau kwenye mechi ya juzi kipindi cha pili, Mayanga alipofanya mabadiliko kwa kuwaingiza Mbaraka na Ajibu timu ikaonyesha uhai. Stars ikacheza soka la shoka na kutengeneza nafasi. Angalau pia timu ikapata bao la kusawazisha.

MUUNGANIKO WA TIMU

Tukubali ama tukatae, ila ukweli ni kwamba muda mwingi  Stars inacheza kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, timu haina muunganiko. Kila mchezaji anacheza anavyodhani inafaa. Angalau Msuva na Samatta wanaelewana, hivyo muda mwingine walionekana kuwa wanataka kufanya kitu.

Kichuya yupo kwenye kiwango cha juu, lakini anacheza sana mwenyewe. Viungo hawaelewani. Timu inabebwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Ajibu na Mbaraka pia wanatumia vipaji vyao zaidi kuliko muunganiko wa timu.

Katika hili Mayanga ana kazi ya kufanya. Ukiwatazama Malawi walivyokuwa wakicheza utaelewa namna Taifa Stars iko ovyo. Malawi wanacheza kwa nafasi. Timu imeungana na wanafahamu nini cha kufanya pindi wanapokuwa na mpira. Hii ndio sababu walitupa kazi kubwa juzi Jumamosi.

MECHI ZA MASHINDANO

Licha ya kwamba Mayanga amefanya vizuri katika mechi za kirafiki na zile za Kusini mwa Afrika (COSAFA), bado ameshindwa kufanya kitu katika mechi za mashindano. Stars ilipata sare nyumbani dhidi ya Lesotho katika mchezo muhimu wa kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).  Ilishangaza sana. Kama Stars inapata sare na Lesotho hapa nyumbani, vipi ikienda kucheza kwao? Vipi ikikutana na Uganda na Cape Verde?

Stars ikatolewa pia kwenye kuwania kufuzu kushiriki Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) baada ya kushindwa kupata ushindi wowote dhidi ya Rwanda. Kwa kifupi Mayanga hajapata ushindi wowote katika mechi tatu za mashindano makubwa alizoiongoza Stars. Kama Stars ya Mayanga imeshindwa kuifunga Lesotho hapa nyumbani. Ikashindwa kuifunga Rwanda nyumbani na ugenini. Itaweza kuzifunga Uganda na Cape Verde? Inahitajika miujiza.

NIDHAMU YA TIMU

Haijawahi kutokea katika kipindi cha muda mrefu kuona  Stars ikicheza na wachezaji wake wawili kuonyeshwa kadi nyekundu. Ilitokea kwenye mchezo dhidi ya Malawi ambapo Mzamiru Yassin na Erasto Nyoni walionyeshwa kadi hizo. Nini kimeikumba timu ya Taifa?

Nidhamu imekwenda wapi. Nyoni alifanya kitendo cha kulaaniwa. Mchezaji wa kiwango chake sio wa kumkanyaga mchezaji wa timu pinzani.