Matajiri wenye mapenzi sana na soka la bongo

Mohammed Dewji.

Muktasari:

  • Wapo matajiri kadhaa wanaopigiwa upatu kwa sasa kuweza kuwekeza klabuni hapo

HABARI kubwa mjini kwa sasa ni mchakato wa mabadiliko ndani ya Simba. Wadau wengi wa soka nchini wanasubiri kwa hamu kuona ni bilionea gani anakwenda kuwekeza kwa vigogo hao wa Msimbazi. Kila mtu anasubiri.

Kwa kifupi, Simba iko mbioni kukamilisha mchakato wa mabadiliko kutoka mfumo wa Wanachama kwenda katika mfumo wa Hisa ambao utashuhudia mwekezaji mmoja akiwekeza Sh20 bilioni ama zaidi ili kuweza kumiliki nusu ya klabu hiyo.

Wapo matajiri kadhaa wanaopigiwa upatu kwa sasa kuweza kuwekeza klabuni hapo, lakini mbivu na mbichi zitafahamika baada ya wiki moja tu, mchakato wa kutangaza tenda utakuwa umekamilika.

Wakati wadau wa soka nchini wakisubiri kuona ni nani atafanikiwa kununua asilimia 50 ya hisa za Simba, makala haya yanakuletea orodha ya matajiri ambao wamewahi kulitikisa soka la Tanzania.

YUSUF MANJI

Huyu bado ni wa moto moto kabisa. Bilionea Yusuf Manji atakumbukwa na wadau wengi wa soka nchini kwa kile alichoisaidia Yanga kwa miaka zaidi ya 10. Manji aliingia Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2006 akiwa kama mfadhili lakini miaka sita baadaye aliamua kuchukua nafasi ya uongozi wa juu wa klabu hiyo.

Katika miaka sita ya kwanza akiwa mfadhili, Manji alisaidia katika usajili, ukarabati wa jengo la klabu, kulipa mishahara makocha na wachezaji pamoja na kutoa posho kwa mechi walizoshinda. Kuna wakati alilipia mashabiki viingilio ili waingie kwa wingi uwanjani kuishangilia Yanga.

Mwaka 2012 aligombea nafasi ya mwenyekiti katika klabu hiyo na kushinda kwa kishindo na katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, Yanga ilitwaa mataji manne ya Ligi Kuu, moja la Kagame, moja la FA, pia kufanikiwa kufika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

Manji alijiuzulu nafasi yake ya uongozi ndani ya Yanga mwezi Mei mwaka huu lakini bado wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa wakielezea kiu yao kuona anarejea tena.

SAID SALIM BAKHRESA

Bilionea Said Salim Bakhresa pamoja na familia yake wana mapenzi ya soka usiambiwe na mtu. Bakhresa alikuwa mfadhili wa Simba katika miaka ya zamani na kuisaidia timu hiyo katika nyakati nyingi ngumu kabla ya baadaye kuamua kutoka kivyake.

Bakhresa aliamua kuanzisha timu yake ya soka, Azam FC mwaka 2007 na mwaka mmoja baadaye ilipanda kushiriki Ligi Kuu Bara.

Kwa kuthibitisha ana mapenzi na soka, Bakhresa aliiwezesha timu yake hiyo kumiliki uwanja wa kisasa wenye hosteli, gym, bwawa la kuogelea na vikorokoro vingine vingi vinavyowawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi. Klabu yake ya Azam imekuwa pia na nguvu kubwa katika usajili, kuajiri makocha, viongozi wa maana, pia kuwalipa vizuri wote walioajiriwa klabuni hapo. Katika kipindi cha miaka 10, Azam imetwaa taji moja la Ligi Kuu, moja la Kagame, matatu ya Mapinduzi na moja la Ngao ya Hisani.

AZIM DEWJI

Nani anakumbuka mafanikio ya Simba kufika fainali ya kombe la CAF mwaka 1993? Kama unakumbuka basi utamkumbuka bilionea, Azim Dewji ambaye alikuwa kiongozi wa klabu hiyo.

Azim ni miongoni mwa matajiri waliotikisa soka la Bongo na kuifanya Simba kuwa timu yenye ushindani mkubwa. Bilionea huyu mbali na kuisaidia Simba kutwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu, alihakikisha inaacha historia kimataifa na ilitokea tu bahati mbaya ikapoteza mchezo huo wa fainali kwa Stellah Adbijan ya Ivory Coast.

Azim huwa anakiri mbali na kutumia fedha nyingi kuibeba Simba, pia aliishi na wachezaji vizuri na kuwajengea morali ya kupambana.

MEREY BALHABOU

Bilionea mwingine aliyewahi kutikisha soka la Tanzania ni Merey Balhabou. Bilionea huyu aliyekuwa akifanya biashara ya mafuta ya magari, alifanikiwa kuiweka Moro United katika ramani ya soka la Tanzania.

Moro United ilisimama chini ya ufadhili wa Balhabou mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka 2005 kabla ya kuanza kushuka taratibu. Katika kipindi chote hicho, Moro United ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zikiwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu kwa msimu.

Katika kipindi hicho, nyota wakubwa kama Juma Kaseja, Pitchou Kongo, Abdi Kassim na wengineo walicheza Moro United, huku aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti Yanga, Davies Mosha akiwa mmoja wa wakurugenzi wa klabu hiyo. Moja ya mafanikio makubwa ya Moro United ni kufika fainali ya kombe la Tusker.

ABBAS GULAMALI

Marehemu Abbas Gulamali naye anakumbukwa kwa kutikisa soka la Bongo. Gulamali aliisaidia Yanga kusimama miaka ya 1980 na 1990 na alikuwa akichuana na Azim Dewji aliyekuwa Simba.

Alisaidia kwa kiwango kikubwa katika usajili wa Yanga, kulipa mishahara jambo lililoiwezesha klabu hiyo kufanya vizuri ndani na nje ya nchi. Katika kipindi chake, alisifika kwa kutumia fedha kuwashawishi wachezaji hasa kutoka Simba kujiunga na Yanga, kitendo ambacho kiliwapa shida matajiri wa watani zao hao ambao kila wakati walilia hasara.

MOHAMMED DEWJI

Bilionea huyu amehangaika sana na soka la Tanzania. Kwanza alianza kwa kuidhamini Simba mwaka 1999-2004 kabla ya kushindwana na viongozi wa klabu hiyo na kuamua kujiweka pembeni. Baadaye akaisaidia Singida United lakini ikachemsha.

Akatoka akainunua African Lyon iliyokuwa na mastaa kama Mbwana Samatta lakini baadaye ikamshinda na kuamua kuachana nayo. Kwa sasa Dewji amejikita tena Simba na ametangaza nia ya kununua hisa za klabu hiyo. Ni wazi bilionea huyu ana mapenzi makubwa na soka na anautazama mchezo huo kama fursa kubwa kibiashara.