Masogange Awakutanisha Kiba na Diamond

Muktasari:

Masogange alifariki dunia Ijumaa jioni katika Hospitali ya Mama Ngoma alikokuwa amelazwa kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili kuhifadhiwa mwili wake kabla ya jana kuagwa Leaders Club.

MAMIA ya waombolezaji wamejitokeza kwenye Viwanja vya Leaders Club kumuaga aliyekuwa mpambaji video za Bongo Flava, Agnes Gerald ‘Masogange’.

Masogange alifariki dunia Ijumaa jioni katika Hospitali ya Mama Ngoma alikokuwa amelazwa kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Muhimbili kuhifadhiwa mwili wake kabla ya jana kuagwa Leaders Club.

Katika msiba huo, mbali na kuaga, kulikuwa na matukio mbalimbali yakiendelea na Mwanaspoti halikuwa nyuma katika kufuatilia kwa kina na hapa linakuwekea kila kitu.

KIBA, Diamond uso kwa uso

Kwa muda mrefu sasa, wasanii wasanii Ali Kiba na Naseeb Abdul ‘Diamond’ hawajakutana. Hiyo ni kutokana na ubize wa kazi zao na mashabiki wao wamekuwa wakitamani sana siku moja wakutane.

Wengi walikuwa wakijiuliza iwapo wasanii hao watatokea kujumuika na wenzao kumuaga mwanadada huyo na wakati ratiba ya uombolezaji ikiendelea, ghafla alifika Kiba na gari yake aina ya BMW X5 saa sita na kwenda kukaa moja kwa moja katika meza kuu iliyokuwa imeandaliwa.

Mwenyekiti wa kamati ya msiba, Steve Nyerere alimpa nafasi ya Kiba kuzungumza na alitumia wasaa huo kuwakumbusha watu waliokuwa uwanjani hapo kukumbuka ibada.

“Alikuwa rafiki yangu na niliwahi kufanya nae kazi, ni mcheshi sana, kazi ya Mungu haina makosa kikubwa ndugu zangu tukumbuke ibada, vyote tunavyofanya inabidi tupate nafasi ya kusali, nimetoka katika harusi lakini nimepitiliza hapa kwa sababu hii nayo ni moja ya ibada katika dini yetu,” alisema.

Baada ya Kiba kumaliza kuongea, Steve Nyerere alisema anatambua uwepo wa WCB na ndipo aliingia Diamond na Harmonize na moja kwa moja walienda kuketi katika meza kuu.

Hata hivyo, shauku kubwa ilikuwa ni iwapo wasanii hao watasalimiana na bila hiyana walisalimiana kwa Diamond kumpa mkono Kiba ambaye alikuwa ameketi na dakika tatu baadaye Kiba alinyanyuka na kuondoka.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilifukunyua sababu za kuondoka kwake na kubaini msanii huyo alifika uwanjani hapo akiwa ametoka katika Ndoa ya mdogo wake (Abdu Kiba) ambayo ilifungwa (Jumapili) asubuhi.

WATU WAZIMIA, VIONGOZI WA SERIKALI NDANI

Muda wa kuaga mwili wa marehemu ulipofika, jeneza lilifunguliwa lakini aliyekuwa mpenzi wa marehemu siku za nyuma Rammy Gails, alianguka ghafla na kupoteza fahamu

Sio yeye tu, hata waombolezaji wengine pia walikuwa wakianguka na kupoteza fahamu na kupelekwa katika gari la wagonjwa.

Katika viwanja hivyo, walikuwepo viongozi wa Serikali akiwepo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi.