Mara paap! Bocco amemaliza mchezo

Muktasari:

  • Okwi ana mabao 14 mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini wakati mashabiki wakimpenda zaidi yeye kuna mfalme mmoja ndani ya timu hiyo anapambana na vita ya kimya kimya, ni John Bocco.

SIMBA hawafurahii ushindi bila kuona straika wao Mganda, Emmanuel Okwi, ametupia wavuni, ikitokea hivyo ni kama mambo hayajakamilika kwao.

Okwi ana mabao 14 mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini wakati mashabiki wakimpenda zaidi yeye kuna mfalme mmoja ndani ya timu hiyo anapambana na vita ya kimya kimya, ni John Bocco.

Bocco anapita katika sayari ya peke yake ndani ya Simba na njia hiyo hakuanza nayo kikosini hapo bali alikuwa na akili hiyo tangu alipokuwa Azam FC aliyoitumikia kwa karibu miaka 10 kabla ya kuondoka na kutua Msimbazi msimu huu.

Kafunika kinoma

Azam ilimuacha Bocco kwa maelezo zama zake zimeisha klabuni hapo huku ikisingizia umri wake umeenda, jambo lililowashangaza wengi. Huenda hilo lilimuumiza mno Bocco na ndio maana ametulia alipotua Simba na kufanya yake.

Alipotua Simba alikuwa na akili yake kichwani kwamba ana kazi ya kuthibitisha ubora wake kwa kufanya kazi ya kuifungia Simba na sasa ana mabao 10 tayari wakati anayeongoza kwa mabao Azam ni Mbaraka Yusuf aliyefunga mara tatu tu akifuatiwa na kinda Yahya Zayd, mawili.

Hakutarajiwa kung’ara

Wakati Simba ikifanya usajili wa nguvu mwisho wa msimu uliopita, wapo wachezaji waliopigiwa hesabu za kuwa tishio zaidi ambao ni kiungo Haruna Niyonzima aliye nje ya uwanja akiwa majeruhi na hajasababisha wala kufunga bao. Pia kuna Okwi kipenzi cha mashabiki aliyefunga mabao 14, lakini Bocco hakupigiwa hesabu kwani alionekana wa kawaida, lakini kwa kazi aliyoifanya lazima umvulie kofia na kumsifu hata kama kimya kimya.

Kokote anafunga

Kabla ya Simba haijacheza na Mwadui juzi Alhamisi, Bocco alikuwa na tofauti kubwa kati yake na Okwi, licha ya Okwi kuwa na mabao 14 lakini bao lake la kwanza ugenini nje ya jiji la Dar es Salaam amelifunga katika mchezo huo tena kwa penalti. Hiyo ni tofauti na Bocco. Jamaa amekuwa akifunga katika uwanja wowote iwe ugenini na hata nyumbani na kufanikiwa kwenda sambamba na Okwi kwa kuwa na umuhimu mkubwa katika ubora wa safu ya ushambuliaji.

Miezi sita na unahodha juu

Kizuri au chenye ubora hakijifichi, huu ni msimu wa kwanza wa Bocco akiwa Simba, lakini ndani ya miezi sita tu tayari ameteuliwa kuwa Nahodha akimrithi Method Mwanjali aliyempoka kitambaa Jonas Mkude aliyeondolewa cheo akiwa ugenini Afrika Kusini.

Bocco anakitendea haki kitambaa alichovalishwa, alishakizoea tangu akiwa Azam.

Nidhamu bora nje, ndani

Ni vigumu kusikia Bocco amekutwa kalewa au matukio mengine ya utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja. Amekuwa akifanyiwa mambo ya ajabu uwanjani, lakini hajawahi kukata tamaa ama kumchafulia heshima yake.

Bocco amekuwa ni mchezaji mwenye mfano wa kuigwa katika sera ya mchezo wa kiungwana (Fair Play) kwa kujua kusamehe kwa haraka, imetokea mara kadhaa anafanyiwa michezo ya kinyama akiwa uwanjani lakini hajawahi kuweka kitu rohoni.

Yanga walimkataa, wanajuta

Wakati Bocco anaondolewa Azam taarifa zinaonyesha hatua ya kwanza jina lake lilitua Yanga, lakini kigogo mmoja alimkataa akidai ni mzee, lakini ghafla jina hilo likatua Simba wakamsajili na sasa wanafurahia kazi yake anaibeba timu.

Kule Yanga sasa baadhi wameanza kumkumbuka wakiona kama angekuwa na msaada kwao, lakini kinachofanya wamkumbuke ni wakati huu ambao Yanga inateseka na straika raia wa Zimbabwe Donald Ngoma ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu akifanikiwa kucheza mechi zisizozidi tano akifunga mara tatu tu.

Yanga wanaona bora ya Bocco kuliko Ngoma ambaye Zlatan Ibrahimovic wa Manchester United aliumia kabla yake akafanyiwa upasuaji na sasa amerudi uwanjani lakini yeye bado yuko hoi.