Mambo ni Salah

Tuesday May 15 2018

 

LIVERPOOLENGLAND

NDIYE Mwanasoka Bora wa Ligi Kuu England msimu huu. Msimu bora kwa upande wake, umemfanya azoe tuzo zote.

Ni Mohamed Salah. Liverpool wenyewe wanamwita ‘Egyptian King’. Pale Anfield ndiyo wimbo unaoimbwa siku hizi. Ni hivi, Mo Salah, amefunga mabao mengi katika msimu wake wa kwanza Liverpool, hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo kwenye historia ya klabu hiyo. Amefunga mabao 44 na kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu England kufunga zaidi ya mabao 40 kwa msimu mmoja katika michuano yote tangu Cristiano Ronaldo alipofanya hivyo wakati huo akiwa Manchester United msimu wa 2007-08. Salah, amenyakua Kiatu cha Dhahabu kwa kufunga mabao 32, ambayo ni mengi kuwahi kufungwa kwenye mechi 38.

Kitu kingine kitamu kuhusu Salah ni ule mguu wake wa kushoto. Ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwa kutumia mguu wa kushoto kwa msimu mmoja pale England, mabao 25.

Msimu huu, Salah amefunga dhidi ya timu 17. Hakuna mchezaji mwingine aliyewahi kufanya hivyo ndani ya msimu mmoja. Katika mechi dhidi ya Watford, Salah alifunga mara nne kwa mashuti yake manne aliyopiga golini.

Hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo tangu msimu wa 2003-04. Mchezaji mwingine aliyewahi kufanya hivyo, ni Andrey Arshavin kwenye mechi dhidi ya Liverpool, Aprili 2009 kipindi hicho akiwa na kikosi cha Arsenal.