Makocha wetu wa Bongo dhidi ya Micho wa Yanga

Muktasari:

  • Kuna Watanzania wengi ambao wamesoma vizuri, wana elimu nzuri tena katika kiwango cha Chuo Kikuu, lakini tatizo kubwa ni kujiamini.

KUNA tabia ambayo Watanzania inatutafuna. Tuna ugonjwa unaoitwa ‘kutojiamini’. Wengi hawajiamini tena bila sababu yoyote ya msingi.

Kuna Watanzania wengi ambao wamesoma vizuri, wana elimu nzuri tena katika kiwango cha Chuo Kikuu, lakini tatizo kubwa ni kujiamini.

Ukiondoa wachache ambao wanajiamini, bado ukweli unabaki palepale kuwa wengi wa Watanzania hawana ujasiri, iwe katika mashindano ya biashara, ajira au hata kazi za kawaida tu.

Na hilo limewafanya wengi kuendelea kulalamikia maisha kuwa ni magumu, lakini kuna fursa nyingi zimeachwa kufanywa na watu wa mataifa ya nje.

Mwaka 2000, katika klabu ya SC Villa ya Uganda aliajiriwa Kocha kutoka Serbia, anaitwa Sredojevic Milutin ‘Micho’.

Wakati huo alikuwa na miaka 30 tu, lakini miaka 17 baadaye hakuna asiyejua kuwa kocha huyo amejiongeza kiasi kwamba anaweza kufundisha klabu au timu yoyote Afrika.

Kwa miaka 17 aliyokaa katika bara la Afrika, Micho aliyekwenda Uganda akiwa si maarufu, licha ya Villa SC amewahi kufundisha Saint-George ya Ethiopia, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Yanga ya Dar es Salaam, Al-Hilal Omdurman ya Sudan, timu ya taifa ya Rwanda, timu ya taifa ya Uganda na sasa amerudi tena Orlando.

Ukiangalia timu alizozifundisha unajifunza kitu kikubwa kimoja; kuwa Micho ni mtu anayetaka kujaribu, ni jasiri, anajiamini, anapenda kujifunza na zaidi anafahamua kupambana.

Kwa mara ya kwanza nilipofanya naye mazungumzo mwaka 2003, alikuwa hawezi kuzungumza sentensi mbili za Kiingereza, lakini sasa anazungumza utadhani anatoka Uingereza.

Anatumia maisha yake uwanjani kuangalia mechi, na ugonjwa wake mkubwa ni kusoma mitandao mbalimbali kujua habari za soka, wachezaji, mbinu mpya za soka na kuzijua klabu na timu za taifa.

Ukimuuliza uimara na udhaifu wa klabu yoyote inayoshiriki ligi kuu katika nchi za Afrika atakwambia, anawajua wachezaji wa kila nchi kwa majina, udhaifu wao na uimara wao.

Anawafahamua waandishi wa michezo wa kila nchi za Afrika, anawajua makocha wa kila nchi na klabu zao katika bara la Afrika. Ni mtu anayejifunza.

Ukiangalia maisha yake anavyoyatumia katika mpira, utagundua kuwa ameamua kuwa hakuna kitu kingine duniani kinachowezesha maisha yake zaidi ya soka.

Sitashangaa nikisikia siku mmoja akiteuliwa kuwa kocha wa klabu yoyote ya England, inaweza isiwe leo wala kesho, lakini ninaamini kuna siku atafika huko.

Kwanini namuelezea Micho? kwa sababu ninataka makocha wetu wajifunze hata kwa asilimia kumi tu kutoka kwa kocha huyo.

Makocha wa Tanzania wameridhika sana, hawataki kukaa kwenye kompyuta kujisomea, hawataki kuongeza ujuzi, badala yake wamebaki kulalamika.

Tumewahi kujiuliza kwanini hatuna makocha wa Tanzania wanaofundisha klabu za nje? Kama iliwezekana kwa Boniface Mkwasa na Sunday Kayuni wakati huo, nini kinashindikana sasa.

Hakuna sababu kwa makocha wa Tanzania kuendelea kuvizia kufundisha Mtibwa au Ruvu Shooting, ni wakati wa kutoka nje ya mipaka na kutafuta timu nyingine za kufundisha.

Mambo hayo hayaji vivi hivi tu, yanahitaji kusoma, kujitolea kikamilifu na zaidi kuufuatilia mpira kwa muda mwingi zaidi kuliko kustarehe.

Tatizo la makocha wa Tanzania wanafanya ukocha huku wakifanya biashara ya kuuza mahindi kutoka mikoani. Hakika bado hawajajitambua.

Wakati tukiwa tunasema wachezaji wetu wanatakiwa kutoka kutafuta timu za kuchezea nje ya nchi, tusisahau kuwa hata makocha wanatakiwa kufanya hivyo.