Majembe ya Guardiola na Mourinho haya hapa

Muktasari:

  • Katika kuelekea mechi hiyo ambayo itatoa taswira halisi ya ubingwa wa Man City kama watashinda, inatazamiwa kuwa kali kutokana na makocha hao kuwa na upinzani mkali.

MANCHESTERENGLAND


LEO kitapigwa kitu cha Manchester Derby huko Etihad.Ni bonge la mechi, Manchester City dhidi ya Manchester United.

Ni bonge la mechi, Pep Guardiola dhidi ya Jose Mourinho.

Makocha hao wawili ni watu wenye upinzani mkali sana ndani ya uwanja.

Katika kuelekea mechi hiyo ambayo itatoa taswira halisi ya ubingwa wa Man City kama watashinda, inatazamiwa kuwa kali kutokana na makocha hao kuwa na upinzani mkali.

Ubora wa makocha hao ndio maana kuna mastaa kibao wa maana wamewahi kucheza chini ya makocha hao wawili.

Alexis Sanchez

Guardiola: Barcelona

Mourinho: Man United

Supastaa wa kimataifa wa Chile ni mchezaji wa 12 kuingia kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kucheza chini ya makocha wawili wenye upinzani mkali, Guardiola na Mourinho.

Sanchez alimtumikia Guardiola wakati alipokuwa Barcelona kabla ya kuondoka hapo kwenda Arsenal, mahali ambako alinyakuliwa na Mourinho ili akaichezee timu yake ya Man United.

Jambo hilo limemfanya Sanchez kucheza chini ya makocha wote hao wawili wapinzani.

Xabi Alonso

Guardiola: Bayern Munich

Mourinho: Real Madrid

Kiungo fundi wa mpira kutoka Hispania, Xabi Alonso ni moja ya wachezaji walioingia kwenye rekodi ya kuwatumikia makocha wawili bora kabisa duniani kwa sasa.

Alonso baada ya kuondoka Liverpool alikwenda Real Madrid na alikutana na Kocha Mourinho, akimnoa staa huyo kwa mafanikio makubwa.

Baadaye, Alonso alipoachana na Los Blancos alikwenda Bayern Munich kukutana na Kocha Guardiola, akivuna mbinu tofauti za makocha hao matata kabisa.

Samuel Eto’o

Guardiola: Barcelona

Mourinho: Inter Milan

Mshambuliaji matata wa Cameroon, Samuel Eto’o ni mmoja wao aliyewahi kucheza chini ya makocha wawili hao wawili wenye upinzani mkali ndani ya uwanja.

Eto’o alianza kuwa chini ya Guardiola huko Barcelona kabla ya kwenda Inter Milan kukutana na Mourinho na kupata mafanikio makubwa, wakibeba mataji matatu makubwa mwaka 2010.

Baadaye, Eto’o alikwenda kuwa tena chini ya Mourinho huko kwenye kikosi cha Chelsea na kufanikiwa alichofanikiwa.

Zlatan Ibrahimovic

Guardiola: Barcelona

Mourinho: Inter Milan

Straika Zlatan Ibrahimovic hana tofauti na Eto’o kwa kucheza chini ya Mourinho kwenye timu mbili tofauti.

Zlatan kwanza alikutana na Mourinho kwenye kikosi cha Inter Milan na baadaye walikwenda kukutana tena katika kikosi cha Man United. Lakini, katikati ya hapo, supastaa huyo wa Sweden alikwenda kuwa chini ya Guardiola huko Barcelona.

Maisha ya Zlatan chini ya Guardiola hayakuwa mazuri na ndiyo maana wawili hao hawaelewani kabisa.

Bastian Schweinsteiger

Guardiola: Bayern Munich

Mourinho: Man United

Kiungo wa Kijerumani, Bastian Schweinsteiger akiwa katika miaka yake ya mwisho mwisho kwenye soka alipata bahati ya kuwa chini ya makocha hao wawili.

Bastian alikutana na Guardiola alipokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich kabla ya kwenda kukutana na Mourinho huko Man United.

Bastian atakuwa na kitu cha kuzungumza kuhusu uzoefu wake wa kuwa chini ya makocha hao wawili, ambao mara zote wamekuwa na upinzani mkali sana wanapokutana.

Kevin De Bruyne

Guardiola: Man City

Mourinho: Chelsea

Kwa sasa, supastaa wa Kevin De Bruyne anacheza soka matata kabisa kwenye kikosi cha Man City na kuwasogeza karibu kabisa na ubingwa wa Ligi Kuu England. Ukimuuliza KDB kwa sasa atakwambia kocha bora kati ya wawili hao ni Guardiola kwa sababu ndiye aliyempa nafasi ya kuonyesha uwezo wake ndani ya uwanja tofauti na alivyokuwa chini ya Mourinho huko Chelsea ambako hakumpa nafasi ya kutosha kuonyesha makali yake na kumtoa kwa mkopo mara kadhaa.

Cesc Fabregas

Guardiola: Barcelona

Mourinho: Chelsea

Cesc Fabregas ni mmoja wao kutoka kwenye ile orodha ya wachezaji wa maana waliopata bahati ya kuwa chini ya makocha wawili wenye mafanikio makubwa ndani ya uwanja, Mourinho na Guardiola.

Baada ya kuondoka Arsenal, Fabregas alikwenda kujiunga na Barcelona ambayo ilikuwa chini ya Guardiola na kuwa mpinzani wa Mourinho kwenye La Liga kabla ya kwenda kuwa chini ya Mreno huyo wakati alipomnasa akacheze chini yake kwenye kikosi cha Chelsea. Fabregas amevuna mbinu tofauti za makocha hao wawili.

Arjen Robben

Guardiola: Bayern Munich

Mourinho: Chelsea

Kabla ya kwenda kuwa chini ya Guardiola huko Bayern Munich, supastaa wa Uholanzi, Arjen Robben alikuwa chini ya Mourinho wakati alipokuwa katika kikosi cha Chelsea.

Robben alicheza soka maridadi alipokuwa chini ya Mourinho huko Stamford Bridge kabla ya kutimkia Real Madrid, ambako hakudumu kwa miaka mingi sana na kwenda Bayern Munich, alikokwenda kuwa chini ya Guardiola alipohamia katika Ligi ya Bundesliga akitokea Barcelona.

Wachezaji wengine

Kwenye orodha hiyo ndefu ya wachezaji waliowahi kucheza chini ya makocha wawili wenye upinzani mkali ndani na nje ya uwanja, Mourinho na Guardiola ni Maxwell, aliyekuwa chini ya Mourinho alipokuywa Inter Milan na Guardiola huko Barcelona.

Eidur Gudjohnsen alikuwa chini ya Mourinho alipokuwa Chelsea na alikwenda kuwa chini ya Guardiola huko Barcelona, huku mchezaji mwingine ni Pedro, aliyekuwa chini ya Guardiola kwenye kikosi cha Barcelona na kwenda kumtumikia Mourinho kwenye kikosi cha Chelsea, wakati mchezaji wa mwisho kwenye orodha hiyo ni Claudio Pizarro, aliyekuwa na Mourinho huko Chelsea na Guardiola kwenye kikosi cha Bayern Munich.