HISIA ZANGU: Maisha yetu yana haraka, washambuliaji nao wana haraka

Muktasari:

Amelaumu kweli kweli. Kitu kimoja hakukijua. Wachezaji wetu wameiga tabia zake.

RAFIKI yangu mmoja kanitumia meseji akiwa na hasira. Analaumu washambuliaji wa Simba kukosa mabao katika pambano dhidi ya Azam.

Amelaumu kweli kweli. Kitu kimoja hakukijua. Wachezaji wetu wameiga tabia zake.

Kuna wachezaji wachache sana watulivu nchi hii. Sio watulivu wa nje ya uwanja. Ni watulivu wa ndani ya uwanja. Hawaendeshwi na hisia za mashabiki. Mmojawapo ni Mbwana Samatta. Mabao yake mengi anayofunga yanatokana na utulivu tu na sio maajabu mengine.

Sehemu ambayo mashabiki wanaungana kihisia kufikiria atapiga yeye hapigi. Sehemu ambayo mashabiki wanafikiri atatuliza, yeye anapiga. Anaamua mwenyewe anachofikiri akiwa ndani ya boksi.

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ni mchezaji mwingine mtulivu. Habutui. Anacheza kwa jinsi anavyotaka yeye sio wanavyotaka mashabiki. Mara nyingi mashabiki wengi wamekuwa chanzo cha wachezaji wetu kukosa utulivu. Kuanzia mechi za mchangani hadi za Ligi Kuu.

Maisha yetu yana haraka sana. Mabao mengi yanayokoswa na wachezaji wetu yanatokana na papara zao. Hawatulii wanapokaribia lango. Miguu inakuwa kama vile inakanyaga moto. Inatokana na hisia za mashabiki wetu.

Mashabiki wetu wanataka mpira ukianza ufike katika lango la adui. Unafikaje? Hawataki kujua. Na mshambuliaji anapofika katika lango wanataka apige. Mashabiki wanamharakisha kwa hisia na kwa kelele. Na kwa sababu mchezaji amekulia katika mazingira hayo naye anafanya hivyo hivyo.

Yatazame mabao ambayo Obrey Chirwa alikuwa anafunga katika mechi za mwisho za msimu uliopita. Alikuwa anatumia akili ya peke yake ndani ya boksi. Wakati mashabiki wakifikiri anapiga, yeye huwa anafinya na kutafuta nafasi nzuri zaidi.

Bao la pili la Gabriel Jesus wa Manchester City katika mechi dhidi ya Liverpool lilitokana na utulivu wa Sergio Aguero. Alikuwa anatazamana vizuri na kipa wa Liverpool, Simon Mignolet lakini akaamua kumpasia Jesus aliyekuwa anatazama na wavu.

Aguero angeweza kucheza kamari ya kupiga mwenyewe na angeweza kufunga, lakini alitulia zaidi. Katika uwanja uliojazwa mashabiki 55,000 wa Kitanzania sidhani kama Aguero angekuwa Mtanzania angempasia Jesus. Jukwaa lingempigia kelele afunge.

Katika soka la Tanzania, hata kama uwanja ni mzuri ni nadra sana kuona timu ikipiga pasi 10 ndani ya eneo lao. Lazima mashabiki watataka mpira upelekwe mbele hata kama hatuna uhakika sana na mipango ya mbele.

Ukiona timu inapiga pasi nyingi ndani ya eneo lao basi ujue wanaongoza kwa idadi inayozidi mabao mawili. Kama wanaongoza bao moja bado mashabiki hawatataka kuona mchezo huo wanaouona wa hatari kwa sababu wanahisi mpira utanyang’anywa na timu yao itafungwa.

Asikudanganye mtu. Maisha yetu ya haraka haraka yanawaponza hata wezi serikalini na kampuni mbalimbali nchini. Mtu anakabidhiwa kitengo ambacho kina mihanya mingi ya kupata pesa na ndani ya mwaka tu anajenga nyumba nne, ananunua magari sita na anahama nyumba aliyokuwa anaishi. Mnataka washambuliaji wetu wawe vipi?

Tanzania ndio nchi pekee niliyotembelea ambayo abiria wa usafiri wa umma huwa hawapangi foleni. Basi likisimama ni vita ndogo. Wakati mwingine Basi linakuwa tupu, lakini abiria kumi waliokuwepo kituoni wanagombea kuingia ndani. Mnataka washambuliaji wetu wawe vipi?

Huku katika soka maisha yetu ya haraka kutoka kwa mashabiki yameanzia mbali. Yameanzia kwa kutosubiri kuandaa vijana. Ndio maana klabu zetu haziji na mipango ya muda mrefu. Viongozi na makocha wanaogopa kutukanwa wakati timu ikijiandaa kwa programu ya muda mrefu.

Leo wachezaji wa kigeni ndio wanatamba zaidi katika Ligi yetu wakati ukifuatilia kwa karibu ni kwamba waliandaliwa vema katika nchi zao wakiwa wadogo. Waliandaliwa kutokuwa na haraka wakifika langoni. Sisi hatuwaandai wachezaji wadogo na tunategemea miujiza pindi wanapokuwa watu wazima. Ndio maana sio ajabu leo nusu ya timu za Ligi Kuu, zina washambuliaji kutoka nje ya nchi katika nchi hii ya dunia ya tatu.Bado tuna safari ndefu. Kama unabisha chunguza jinsi Mtanzania wa kawaida alivyo na haraka.